Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Dr. Josephat Mathias Gwajima

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kawe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii na mimi kuchangia katika Wizara hii. Kwanza kabisa nimshukuru Mheshimiwa Mashimba Ndaki ambaye ni Waziri wa Wizara hii pamoja na rafiki yangu, Mheshimiwa Abdallah Ulega ambaye ni Naibu Waziri wa Wizara hii. Ingawa siku ya futari ya Waziri Mkuu alisoma Dua mbaya mvua ikanyesha tukashindwa kula vizuri futari, lakini namshukuru hivyo hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi kama Mbunge wa Jimbo la Kawe, jimbo lile limezungukwa na Bahari ya Hindi. Kata za Msasani, Kawe, Kunduchi, Mbweni, Mikocheni na Bunju zote hizi ziko kati ya Bahari ya Hindi na kwa sababu hiyo, kwa uzito sana nalazimika kuchangia hii hoja ya Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama yalivyo majimbo mengine ambayo yana shughuli kubwa za kilimo, ndivyo ilivyo katika Jimbo la Kawe, shughuli kubwa ya wenyeji wa eneo hilo hasa wale wazawa wanaoishi mwambao wa bahari ni uvuvi. Kwa hiyo, huwezi kuwatenga na uvuvi; ili wale, wanywe, wasomeshe watoto, wajenge nyumba au wafanye shughuli yoyote, maisha yao ni uvuvi. Kwa hiyo ninapojadili kwa habari ya uvuvi kwenye Jimbo la Kawe, ni uti wa mgongo wa wenyeji wa Jimbo la Kawe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri, nilipofika ofisini kwake kwa sababu kule Jimbo la Kawe tulikuwa na shida ya uvuvi, wavuvi walikuwa wamezuiwa kutumia ring net wakati wa mchana, kwa hiyo, wavuvi wengi walikuwa wameshindwa kuvua kabisa kwa sababu uvuvi wao wanahitaji kuvua mchana na ili kuvua mchana wanahitaji kutumia ring net.

Mheshimiwa Spika, lakini nikafika kwenye ofisi ya Waziri pamoja na Naibu wake, nikazungumza nao na wakaagiza kwamba wavuvi wote wa Jimbo la Kawe waachwe watumie ring nets mchana wakati Serikali inaendelea kutafakari sheria hiyo na leo wavuvi wangu wanaendelea kufanya vizuri, wanaendelea kuvua murua kabisa, nimshukuru kwa sababu hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni ile sheria ambayo tulijaribu kui-discuss na Naibu Waziri pamoja na Waziri ya kwamba wavuvi wanatakiwa kuvua kwenye mita 50 chini. Mimi ni mdau wa aviation, kwenye aviation kuna kitu kinaitwa transponder ambacho ni chombo chenye uwezo wa kuangalia kina cha maji, nimesafiri siku moja pamoja na meli kutokea Dar es Salaam kwenda Zanzibar tukiwa na chombo hicho kinaitwa transponder ambacho kinaangalia kina cha bahari kutokea kwenye surface ya bahari mpaka chini.

Mheshimiwa Spika, kusafiri kutoka Dar es Salaam mpaka Zanzibar, kina kirefu kuliko chote tulichokipata ni mita 52. Sasa ni ajabu kweli mtu akisema wavuvi wavue kina cha bahari mita 50, maana yake wasafiri kwenda mpaka zaidi ya Zanzibar wakawapate hao samaki, hicho kitu hakiwezekani na kama Waziri akiendelea nacho, basi nitamuondolea shilingi kwenye bajeti yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia nimshukuru kwa sababu nilipofika ofisini kwake nikajadiliana na yeye akasema kwamba wavuvi waendelee kuvua mahali ambapo wanataka kuvua mpaka hapo Serikali itakapoangalia namna ya kuitengenezea hii sheria mchakato mzuri ili watu waruhusiwe kuvua na wawe na maisha salama zaidi.

Mheshimiwa Spika, nataka nishauri Wizara hii, katika nchi zinazozungukwa na bahari duniani kama ilivyo Japan na nchi zingine, uvuvi pamoja na shughuli za bahari ni ajira kamili inayowasaidia wananchi kupata mapato yao. Kwa mfano, kwenye Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi tumesema kwamba tuta-create ajira milioni nane, na kama Wizara hii itakuwa na ubunifu wa kubuni na kuikuza industry ya uvuvi kwenye maeneo yetu ya Jimbo la Kawe na sehemu zingine, inaweza kuchangia sehemu kubwa sana kwenye kutengeneza ajira za kutosha na kufanya hizi ajira milioni nane zilizoahidiwa na Chama cha Mapinduzi zitokee mara moja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuongeza pato la Taifa, ni muhimu sana kama Serikali ikiwekeza si tu kwenye uvuvi, bali kwenye michezo ya bahari pia na shughuli mbalimbali za bahari na kuitumia bahari sawasawa. Hili linaweza kutusaidia sana kuongeza pato la Taifa na hapo hapo kuwasaidia wavuvi wetu kupata fedha ya kutosha na wakati huo huo kuisadia nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Ahsante sana. (Makofi)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Askofu Josephat Gwajima. Mlipokuwa mkisema kwamba kina kirefu kati ya Dar es Salaam na Zanzibar ni kama mita 50 hivi, nilikuwa naangalia pale juu pale hadi hapa chini, hapa si fifty meters? Haifiki eeh?

MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Spika, haifiki hapo, hapo inaweza kuwa 38 hivi. (Kicheko)

SPIKA: Point yangu ni kwamba inaelekea siyo mbali sana, inaelekea Dar es Salaam – Zanzibar kina cha bwawa tu kama la Hombolo pale. (Kicheko)