Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Soud Mohammed Jumah

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Donge

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii kuweza na mimi kutoa mchango wangu katika Wizara ya Mifugo na Uvuvi, lakini kadhalika ningependa kwanza kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu wake Ndugu Ulega, kwa kazi nzuri ambayo wanafanya katika Wizara hii. (Makofi)

Ningependa kuwapongeza watendaji wa Wizara hii kwakweli wamefanya kazi nzuri na ndiyo maana sasa hivi maeneo mengi yameanza kuimarika hasa yale ambayo yamezalia samaki hasa katika masuala ya matumbawe au coral leaves. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ningependa kuelekeza mchango wangu katika maeneo mawili makubwa; la kwanza ni kuhusu suala la usafirishaji wa biashara ya dagaa ambayo jana niliuliza swali langu, lakini la kwanza ningependa kumpongeza vilevile Mheshimiwa Ulega kwa kweli toka jana ameanza kulifuatilia hili suala na imenitia moyo sana na huu ndiyo uwajibikaji haswa wa Serikali hii ya Awamu ya Sita. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ningependa kusisitiza tu kwamba tusiwategemee tu sana watendaji wetu wakati mwingine wanakuwa wanatuangusha kwa sababu wanaporipoti inakuwa sivyo wanavyofanya, kwa hiyo nashukuru hili ambalo tulikuwa tunalifanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, lakini pia ningependa tu kuwaomba wenzetu watendaji hawa wakajaribu kuwasaidia hawa wafanyabiashara na dagaa kwa sababu ni nieneo ambalo linaajiri watu wengi sana na hasa wanawake, na hivi sasa biashara hii imekuwa inafanywa sana na wageni ambao wanakwenda mpaka kwenye madiko na kununua dagaa; ingekuwa vyema kama tukawapa-incentives watu wetu wakaweza kufanya biashara wao moja kwa moja na wakasafirsha dagaa badala ya wageni kuja moja kwa moja kwenye mwalo na kununua dagaa.

Mheshimiwa Spika, eneo la pili ningechangia kuhusu masuala mazima ya maeneo ya mazima ya maeneo ya mazalia ya samaki hasa masuala ya mikoko au mangroves yaani mikandaa kwa jina lingine. Kuna uharibifu mkubwa sana katika maeneo ya mikoko au mikandaa, ukaenda Rufiji na maeneo ya kanda mbalimbali za fukwe za bahari, mikoko imekuwa ikiathirika sana na nimaeneo ambayo ni mazalia makubwa ya samaki. Sasa hapa ningewaomba wenzetu wa uvuvi mkashirikiana na Wizara na Maliasili kwa sababu ingawa mikoko au mikandaa ni miti, lakini ni mazalio na ni malisho ya samaki.

Mheshimiwa Spika, sasa tukiwaachia wenzetu wa Maliasili peke yao, sisi tukaendelea zaidi kwenye masuala ya uzalishaji wa samaki au uvunaji na biashara moja kwa moja basi tutakuwa tunaacha eneo muhimu ambalo linaweza likasaidia. Kwenye Mradi wa MANCEP ulifanya kazi nzuri ya kuendeleza mikandaa, lakini Mradi wa SWIOFish bahati mbaya umeliacha hili eneo haukuliendeleza, kwa hiyo hizi resources tunavyozipata tuangalie maeneo haya kwa sababu nayo ni maeneo muhimu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Semesi katika mwaka 1992 alifanya utafiti wa mikoko au mikandaa na akaandaa management plans ikiwemo uzalishaji na ulishaji au malisho ya samaki. Lakini bahati mbaya hizi management plan zote ziko kwenye ma-shelf, hazikufanyiwa kazi toka mwaka 1992 mpaka hii leo. Ningeomba wenzetu wa uvuvi mkaziangalia hizi management plans na tukaangalia tukazi-review ili kuona uwezekano kuziendeleza tujue tunaanzia wapi katika kuendeleza mikandaa au mikoko iwe ili iwe ni sehemu salama zaidi ya kuweza kuwasaidia kuzalisha samaki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho ningependa kugusia vilevile suala zima la mabadiliko ya tabia nchi. Mabadiliko ya tabia nchi yanaathiri sana wafugaji na kipindi cha ukame maeneo mengi ya maji na malisho yanaathirika na kuna miradi kama Mradi wa Decentralize Government Finance ulianzishwa ili kuzisaidia Halmashauri kuweza kusimamia maeneo ya malisho na kuzitafuta fedha kwa ajili ya kuwasaidia wafugaji. Sasa mradi ule umemalizika mpaka hii leo zile jitihada hatukuziendeleza, kwahiyo miradi hii inakuwa ni mizuri lakini sasa stability inakuwa haipo. Kwa hiyo ningeliomba tu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH: Mheshimiwa Spika, ahsante sana naunga mkono hoja naomba kuwasilisha. (Makofi)