Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Tunza Issa Malapo

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi, awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa zawadi ya uhai.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati napitia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi nimepata mshituko wa moyo, kwa nini nimepata mshituko, ukiangalia kwa miaka mitano mfululizo wanatenga pesa za maendeleo, lakini haziendi. Kwa mfano nakupa ya miaka mitatu huko nyuma sitaki kurudi, mwaka 2017/2018 walitengewa bilioni nne haikwenda hata sumni, mwaka 2018/2019 Sekta ya Uvuvi peke yake ilitengewa bilioni saba ikapewa bilioni nne, 2019/ 2020 ilitengewa bilioni 14 ikapewa bilioni tatu, mwaka huu ambao tunaumaliza kesho kutwa 2020/2021 walitengewa bilioni 13 mpaka leo wamepewa bilioni nne.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kilichonishtua nini? leo wametengewa bilioni 99, ikiwa bilioni nne, bilioni 13 zinawashinda kupeleka, hizi bilioni 99 wanazitoa wapi? Ndio maana nakwambia nimeshituka, sasa Mheshimwa Waziri atakapokuja kuhitimisha atueleze mkakati wao, kutengwa kwa pesa nyingi maana yake tunaraji tukapate maendeleo makubwa kwenye hizo sekta kwa sisi ni furaha yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, furaha hii inakwenda kuingia huzuni kwa sababu walikuwa wanatengewa kidogo, lakini haziendi mpaka huu mwaka tuliopo sasa hivi tupo mwezi wa tano tunaumaliza wamepewa asilimia 31 tu katika bilioni 13, leo wanapata wapi courage ya kutenga bilioni 99, nataka akija hapa atueleze ni kitu gani hicho kilichowapelekea wao kufikiria watapata bilioni 99, hatutaki maneno, maneno tunakata vitendo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mshtuko wangu wa pili, sisi Watanzania tuna maziwa makubwa, tuna Ziwa Victoria, tuna Ziwa Nyasa, tuna Ziwa Tanganyika, sisi watanzania tunaukanda mrefu sana wa bahari, sisi Watanzania tuna deep sea, bahari kuu maana yake. Unaamini kwamba kwa mwezi tunaagiza samaki tani 24,000 zinaingia nchini kwetu, pamoja na kuwa na hivyo vitu vyote, nimepata mshituko kwa sababu safari hii wakati naelekea kuchangia Wizara hii niliamua nijipe muda kidogo nisome, kwa hiyo huo mshituko wangu wa pili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeshtuka kwa sababu sisi kama Taifa tunatumia takribani bilioni 58 kwa mwezi kuagiza samaki nje, tuna Bahari ya Hindi, tuna Ziwa Victoria, tuna Ziwa Tanganyika, tuna Ziwa Nyasa. Mheshimiwa Waziri akija kuhitimisha atupe majibu tunakwama wapi? na kwa nini tunakwama? Mwenyezi Mungu atupe nini? kwa kiasi cha maji tuliyokuwa nayo sisi na hivyo nimekutajia makubwa, tunayo madogo karibia kila mtu kwao hapa utakuta kuna bwawa, ukienda Morogoro bwawa Mindu sijui huko wanavua, sijui nini, kuna mito midogo midogo watu wanavua, nimekutajia haya makubwa. Tuna sababu gani ya kuagiza Samaki wengi hivyo kutoka nje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati naendelea kutafuta baadhi ya sababu ndiyo hizi zingine kwa sababu hela haiji, hela kama haiji wizara inashindwa kuwekeza, ama wizara haina mikakati thabiti kwa sababu gani, binafsi yangu sifikirii mpaka leo wavuvi wetu waingie baharini wakatafute Samaki wakati, yaani wakienda na ile kwamba Mungu akipenda nitapata. Kuna vifaa vya kisasa vinavyotambua tu kwamba ukiingia baharini sehemu fulani ndiyo Samaki wapo wengi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unamwomba Mungu, lakini Mungu huyo ndiyo katupa sisi maarifa, Mheshimiwa Ulega wewe hii ni taaluma yako na unaijua, unatakiwa uwe serious my brother sasa hivi tunatakiwa twende kwenye uvuvi wa kisasa, jamani Samaki tunawaacha huko baharini kama mnakumbuka ile meli iliyokuwa inaitwa meli ya Magufuli hivi wale walivua Samaki kiasi gani? wenye ukubwa gani? nyinyi wote hapa ni mashahidi, lakini leo sisi tunavua Samaki ndio hao wanakujaga kupimwa na ruler hapo kwenye kantini. Maana yake hata kile kimo hajafika kwa sababu gani, kwa sababu ya kukosa zana bora za uvuvi, Serikali iwekeze hapo ndipo tunapofeli haya matatizo yote yanatokea hivyo, leo mwenzangu hapa jirani yangu wakati anachangia alikuwa anasema matumbawe yanaharibiwa, lazima yataharibiwa si wanatafuta mabomu, akipiga pale anapata samaki wake anarudi nao nyumbani, hana zana bora unategemea atavuaje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, twendeni tukawekeze hapo. Uchafuzi huu wote watu kuhangaika kukimbizana na samaki wadogo wadogo hakuna mtu anayetaka apate samaki kidogo ama apate samaki wadogo ni kwa sababu anakosa dhana bora za uvuvi. Badala ya kukimbizana kuchoma nyavu fanyeni jitihada za makusudi mwambie mtu nyavu hii usivulie, vulia kifaa hiki, hakuna mtu anayependa maisha magumu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie kwa jambo moja dogo, lakini lina umuhimu wake. Sisi wanawake tuliowengi ndio wafugaji wa kuku, tuliowengi, iwe wale wa kisasa iwe wa kienyeji hata mwenyewe nafuga kwa kiasi kidogo, lakini nafuga. Kuna changamoto kubwa sana kwenye sekta hiyo na wanawake wengi ndio wanaponea huko, hiyo mikopo ya halmashauri ya asilimia kumi sijui nini wengine wanachukua kwenda kufuga. Hata hivyo, tunapata changamoto, kwanza upatikanaji wa vifaranga siyo wa uhakika, unaweza kutafuta kifaranga leo mwezi wa tano ukaambiwa order utaipata mwezi wa tisa, jiulize tangu leo mpaka mwezi wa tisa hapo hiyo hela unaifanyia nini. Ukipata kifaranga chakula bei juu, ukipata chakula chanjo hazieleweki, unaweza kuweka kuku bandani umewapiga chanjo zote wakaja kufa usitoke hata na kuku mmoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Serikali iweke mkakati wa makusudi wa kunusuru wanawake na hata wanaume ambao wanafuga kwa kuhakikisha wanapata huduma bora za usaidizi, wanapata chakula kwa bei nzuri ili kusudi iendane na soko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo mengi yenye umuhimu, nakushukuru sana. (Makofi)