Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Twaha Ally Mpembenwe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibiti

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi kuweza kuchangia katika Wizara hii muhimu sana.

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa, nichukue fursa hii kuipongeza Wizara kwa wasilisho zuri ambalo wameliwasilisha mbele yetu na sasa hivi tunalijadili. Kipekee nimshukuru Mheshimiwa Waziri kwa unyenyekevu mkubwa sana aliokuwa nao na ushirikiano ambao anauonesha kwa Wabunge wote ambao tunazungukwa na maeneo haya ya uvuvi.

Mheshimiwa Spika, vilevile nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri. Mheshimiwa Rais alivyoweza kumpa nafasi hii tena kwa kumtoa kwenye sehemu ya michezo, Mheshimiwa Rais alifanya maamuzi yaliyokuwa asilia. Kwa sababu Mheshimiwa Naibu Waziri yeye ni mzoefu na ni institutional memory katika Wizara hii. Ana uzoefu mkubwa sana na ni mtaalam katika sekta hiyo. Kwa hiyo, ni mategemeo yangu kwamba anakwenda kushirikiana na Mheshimiwa Waziri pamoja na wataalam katika Wizara husika ili kuweza kuleta mabadiliko makubwa zaidi kwa maslahi mapana ya wananchi wa Tanzania na bila kuwasahau watu wa Jimbo lake la Mkuranga pamoja na wajomba zake wa pale Kibiti.

Mheshimiwa Spika, naomba nichangie Wizara hii katika eneo moja tu la uvuvi. Mchango wangu utakuwa umegawanyika sehemu kubwa mbili, sehemu ya kwanza nitachangia kitaifa zaidi lakini sehemu ya pili nitarudi kule katika Jimbo langu la Kibiti pamoja na wajomba zangu wa Mkuranga ambao tuna adha kubwa sana kuhusiana na suala zima la mambo ya kamba.

Mheshimiwa Spika, ni ukweli ulio wazi kabisa kwamba rasilimali tulizonazo sisi Tanzania katika maeneo yetu ya uvuvi ni rasilimali tosha kabisa kuonesha kwamba pato letu la Taifa linaloweza kuchangiwa na Wizara hii au na sekta hii liwe linakwenda juu siku hadi siku. Mheshimiwa Waziri katika hotuba yake ametuambia kwamba katika GDP tumepata asilimia 1.7 mwaka 2020 na amesema kwamba sekta hii imeongeza uzalishaji imekua kwa asilimia 6. Sasa sielewi tafsiri pana mimi niliyokuwa nayo katika watu wa uchumi tunasema ongezeko hili lime-increase katika decreasing rate.

Mheshimiwa Spika, nasema hivyo kwa sababu mwaka 2013 sekta hii katika suala zima la GDP lilichangia kwa asilimia 2.4, lakini leo tuko mwaka 2020 limechangia kwa asilimia 1.7. Mheshimiwa Waziri katika hotuba yake ametuambia kwamba kuna ongezeko zuri sana la uzalishaji katika sekta hii, sasa huu uzalishaji ongezeko lake liko very questionable.

Mheshimiwa Spika, Ziwa Victoria sisi tuna asilimia 51, tafiti zilizokuwa zimefanywa na wataalam zinatuambia kwamba tani za samaki zilizokuwa pale ni 3,495,914. Katika Ziwa Tanganyika sisi tuna asilimia 41, tafiti zilizokuwa zimefanywa na wataalam zinatuambia kwamba tani za samaki zilizoko pale tunazungumzia 295,000.

Mheshimiwa Spika, tukienda mbele zaidi kule kwa wakwe zangu katika Ziwa Nyasa sisi tuna asilimia 18.5 katika eneo la uvuvi, tafiti zilizokuwa zimefanywa na wataalam zinatuambia kwamba tani za samaki zilizokuwa pale ni 168,000. Hatujaishia hapo tukienda mbele zaidi kwenye territorial area yetu kule, tafiti zilizokuwa zimefanywa na wataalam tunaambiwa tuna tani 100,000 za samaki. Kule ndani zaidi hatukuweza kufika kwa sababu utafiti bado haujafanyika. In totality tani zote za samaki zilizopo Tanzania tunazungumzia 3,598,914. GDP tunaambiwa kwamba tumechangia kwa asilimia 1.7 hapa kuna shida tena kuna shida ya msingi.

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu kwa Serikali, Mheshimiwa Waziri ametuambia hapa kuna mambo makubwa ambayo wanakwenda kufanya, mojawapo wanatuambia kwamba kuna meli tunaitegemea itapatikana kwenda kule deep sea. Hii iko very questionable kwa sababu tunachokifanya hapa tunanunua mbeleko wakati bado hata mtoto hajazaliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika hotuba hii Mheshimiwa Waziri ametuambia kwamba tunakwenda kutengeneza bandari pale Bagamoyo. Sisi ni wageni utatuvumilia vijana wako kwa sababu tunajifunza mambo mengi sana, mwaka 2012 kuna fedha ziliweza kutolewa katika Bunge lako hili karibia milioni 500 za kufanya tafiti jinsi ya kuweza kujenga bandari. Kutokana na taarifa tulizokuwa tumezipitia library huko inasemekana kwamba kule Kilwa Masoko ndiyo bandari ilikuwa inakwenda kujengwa, nini kilichotokea mimi sijui.

Mheshimiwa Spika, leo Mheshimiwa Waziri anatuambia tunakwenda kujenga pale Mbegani safi sana mimi natokea Pwani na nina interest hiyo kwa Pwani lakini na Taifa kwa ujumla wake. Hata hivyo, tunaambiwa kwamba katika bajeti imetengwa shilingi bilioni 50 na sisi tunakwenda na mfumo wa cash budget system pale tunapokuwa tunakusanya ndipo tunapokwenda kutumia, sasa napata shida tunaagiza meli, halafu tunaambiwa tunakwenda kujenga kule Mbegani, tumetenga bilioni 50, where are we going to get the money from? Hapa mimi napata shida. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi ni mhubiri mkubwa sana wa suala zima la PPP. Tukubali, tusikubali Serikali tusiwe tunaingia moja kwa moja kichwa kichwa katika mambo haya. Ni vizuri tukawa tuna-regulate, lakini tunajua kabisa kwamba kuna baadhi ya maeneo katika suala zima la tafsiri ya kiuchumi inaweza ikawa ni controlled economy ikawa mixed economy. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Serikali lazima tuwe tunaangalia jinsi ya kuweza kuingia pale. Ili tuweze kuwekeza jinsi inavyopaswa katika sekta nzima hii ya mambo ya fishery, ni lazima twende katika suala zima la PPP. Mheshimiwa Waziri na wataalam mkae kitako kuishauri Wizara kwamba twendeni kwenye PPP tuwaite watu waweze kwenda kujenga bandari. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunavyozungumza kujenga bandari ya uvuvi hiki siyo kitu cha masihara tunazungumza bandari iwe na infrastructure zote zinazoweza kukubalika, ikiwemo suala zima la kutengeneza viwanda, meli inavyokuja inapaki pale, samaki zinaondolewa, kama utumbo unatolewa, watu wanaweka kwenye cold room mambo mengine yanaendelea. Sasa tunakuja kuzungumza kwamba tunakwenda kujenga Mbegani tumetenga shilingi bilioni 50, this is a joke!

SPIKA: Mheshimiwa unayetoka rudi kwenye kiti chako kwa sababu umekatiza kati ya mzungumzaji na mimi. Kwa hiyo, rudi ukae kwenye kiti chako. Nazidi kuwakumbusha kama mzungumzaji anazungumza usikate kati ya mstari wake na Spika. Mheshimiwa Mpembenwe endelea. (Makofi)

MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Spika, kwa tafsiri hiyo hiyo maana yake ni kwamba sisi ili tuweze ku-move kutoka hapa tulipo kama alivyosema senior wangu pale, kaka yangu Mheshimiwa Mwijage, ni lazima twende katika concept hii ya PPP.

Mheshimiwa Spika, narudia mara kwa mara na nitaendelea kulirudia kwa sababu kubwa moja, sheria ililetwa hapa. Sasa kama hii sheria ilikuwa imekuja kuja tu katika mazingira ya kuja, mimi napata shida. Sheria hii ilikuja hapa na ikafanyiwa amendments, lazima sasa tuweze kutumia sheria hii tuweze kuwaita wawekezaji ili sasa kwa namna moja ama nyingine twende tukajenge bandari na tuweze kuona sekta hii inakwenda kuchangia vile inavyopaswa sio tu asilimia 1.7 twende mbele zaidi. Mheshimiwa Waziri unatuambia kwamba kuna growth ya 6 percent katika production lakini Growth Domestic Product yenyewe imekwenda 1.7 wakati 2013 ilikuwa 2.4, hii ni increase katika decreasing rate, we cannot be able to move in that way. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa tafsiri hiyo hiyo, naomba tena niishauri Serikali, ili tuweze kufanya vizuri zaidi katika eneo hili basi hakuna budi na sisi vilevile katika Wizara hii tutengeneze jeshi letu, kama kule TANAPA mifugo inaibiwa, watu wanachukua kila kitu. Kuna watu wanaitwa DCA, wanachokifanya wao hakuna kitu kingine zaidi ya kutoa tu certificate watu wa Spain au Malabar na meli kubwa kubwa wanatoa tu taarifa tunataka kuja kuvua kule kwenu. Watu wanachokifanya wanaambiwa bwana lipa ada akilipa ada meli inakuja inavua inaondoka. Sasa kuna zile meli nyingine haziwezi zikaja kufunga hapa, hatuna ports ya kuweza kufanya hawa watu waje kwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mambo yako mengi, lakini naomba niende Jimboni kwangu sasa. Jimboni kwangu kuna shida ya msingi sisi tunavua kamba na hapa Tanzania wanavyozungumza suala zima la kuvua kamba wanapatikana pale. Mimi najua baba yangu mzee Mpembenwe siku moja aliwahi kuniambia, yule mnayemuona pale Spika wenu yule aliwahi kuwa Rufiji huku anaijua Rufiji vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niseme tu kwamba pale Kibiti na Mkuranga sisi tuna shida na Wizara hii, kikubwa wanachokifanya ni kuweka tu mambo ya kitaalam mengi, ma-scientist wanakuwa wengi. Mwaka 2017 wamezuia pale uvuvi wa kamba katika kipindi fulani, hivi ninavyozungumza kamba pale wanavuliwa katika kipindi siyo rafiki. Wakati sisi wananchi wanaomba kuvua kamba katika kipindi cha mwezi Desemba mpaka Mei wao wanatuambia tuanze kuvua kuanzia mwezi Juni kwenda mbele, kipindi hicho wale kamba wanakwenda bahari kuu, wanavyokwenda bahari kuu wananchi wetu hawana vyombo vya kwenda kule. Tafsiri yake ni nini? Tunawaweka wananchi wa Mkuranga na Kibiti katika maisha magumu. Kule ni delta, vile ni visiwa, hatuna zao tunaloweza kuzalisha sisi zaidi ya kamba wale kuweza kutusaidia. Kwa hiyo, hivi vitu lazima tuviangalie kwa upana wake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine la kusikitisha zaidi, Mheshimiwa Waziri wiki iliyopita wakati nauliza swali hili Serikalini alisema kwa mapana marefu zaidi, katika kipindi cha miaka mitano mwaka 2015-2020 kamba waliopatikana katika Wilaya ya Mkuranga pamoja na Kibiti ni tani 1,200. Fedha zilizopatikana shilingi bilioni 16 Serikali walipata tozo shilingi milioni 600. Wilaya ya Mkuranga hawakupata senti tano, Wilaya ya Kibiti hatujapata senti tano, sasa mnatusaidia sisi watu wa Kibiti na Mkuranga? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niseme tu kwamba, Wizara lazima iweze kufikiria kutusaidia watu ambao tunaishi katika maisha ya delta, hatuna shughuli nyingine yoyote ya kilimo. Kule mimi niliko nina Kata 5 za Kiongoroni, Mbochi, Mapoloni, Msala na Salale na kule kwa Mheshimiwa Waziri kuna Kata moja ya msingi sana kuleā€¦

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na naunga mkono hoja. (Makofi)