Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Ilemela

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumshukuru Mungu kwa fursa ambayo tumeipata leo hii kuweza kushiriki vizuri katika Bajeti yetu ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Aidha, imani huzaa Imani. Napenda kumshukuru sana Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuniamini na kuendelea kunipa ridhaa ya kuwa katika Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nawashukuru sana wananchi wote wa Jimbo la Ilemela ambao pia wameniwezesha kuingia katika Bunge lako hili kwa kipindi cha pili. Kwa uwakilishi, nawashukuru sana Waheshimiwa Madiwani ambao leo tuko nao hapa na wameshuhudia jinsi Mbunge wao anavyomenyeka hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru pia Waziri wangu kwa malezi mazuri katika Wizara, anatuelekeza na kutuongoza vyema. Sifa zote zinazosemwa hapa, zinatokana na uongozi shirikishi ndani ya Wizara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nawashukuru sana watumishi wote wa Wizara ya Ardhi kwa ushirikiano, pia nawashukuru sana Wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hususan Kamati ambao wametupa ushirikiano mzuri sana katika kuhakikisha tunatenda kazi zetu vyema. Nakushukuru wewe pamoja na Spika na uongozi wote katika Bunge hili wakiwemo Wenyeviti kwa namna ambavyo tumeshirikiana.

Mheshimiwa Naibu Spika, nawashukuru sana viongozi wa dini ambao wameendelea kututia moyo kwa sala na dua zao, wanazidi kututia nguvu hata pale tunapokutana na magumu mengi yakiwemo ya magonjwa ya Covid na mengine, lakini wametuweka imara na tunaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho lakini siyo kwa umuhimu, naishukuru familia yangu, David na Sandra, Jacqueline na James, Diana na Emmanuel pamoja na Dorothy, kwa jinsi wanavyoweza kunivumilia katika hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kushukuru, basi nianze tena kwa kuwapongeza Wabunge wote waliochangia. Jumla ya Wabunge 33 wamechangia; 24 wamechangia kwa kuongea na tisa wameleta kwa maandishi, lakini pia kuna wengine wanane nilikuwa nimewasahau hapa, walichangia wakati ule wanachangia Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano. Hoja zao tumezichukua na wote waliochangia, hata kama sitaisema hapa na Waziri hataisema, tutazijibu kwa maandishi na tutawaletea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto nyingi zinazozungumzwa zinatokana pia na uelewa pengine mdogo wa wananchi wetu lakini pia na lile suala zima la kutojua haki zao na wajibu wao katika suala zima la sekta hii ya ardhi. Hayo yote tutakwenda kuyafanyia kazi kutokana na miongozo mbalimbali ambayo tunaendelea kuitoa, elimu kupitia vipindi mbalimbali na vijarida tunavyovitoa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze sasa kwa kujibu hoja ambazo ziko nyingi, nitajitahidi kadri nitakavyoweza. Kamati imetoa hoja nyingi, zaidi ya 30 ambazo wamezileta na sisi kama Wizara tumezipokea. Ya kwanza ilikuwa inaongelea habari ya Serikali kubuni mfumo endelevu ambao utahakikisha fedha za Serikali zinaletwa kutoka Serikali Kuu. Niseme ushauri umezingatiwa na ndiyo maana Wizara inaendelea kupata fedha na kuendelea katika kuweka kwenye vipaumbele ambavyo tumejiwekea. Kwa hiyo, zinakuja japo katika utaratibu ambao upo, unaeleweka.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuhusu Wizara kuelimisha wananchi, katika suala zima la ulipaji kodi, naomba niseme, Sheria ya Ardhi Na. 4 katika kile kifungu cha 33(1), kila mwananchi anayemiliki ardhi anao wajibu wa kulipa kodi ya pango la ardhi, lakini watu wanasubiri kusukumwa. Naomba tu Watanzania kwa ujumla tutii sheria, tuzingatie sheria zinasemaje? Kwa sababu mapato pengine yanapungua kwa sababu watu hatutii sheria zetu, lakini ukiangalia kile kifungu kinasema, “kila anayemiliki.”

Mheshimiwa Naibu Spika, pia mwaka 2020 hapa Wabunge wametupitishia mabadiliko ya sheria. Kifungu Na. 24A na Na. 33 kifungu cha 13 na cha 14, pale ambapo tayari upimaji unakamilika na surveys zinapita, tayari ana siku 90 tu yule mwananchi kuomba kumilikishwa. Asipomilikishwa ardhi ile, anaanza kutozwa kodi ya pango ya ardhi. Ile ni sheria ipo ambayo tunahitaji kuendelea kuwaelewesha wananchi ili waweze kujua.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hili linafanyika, lakini watu wanapuuzia sheria. Nasi tumeshaelekeza, basi kwa sababu tayari Kamati imeona kuna upungufu katika makusanyo, lakini pengine inatokana na wananchi kutozingatia sheria, tutaendelea kukaza buti ili tuendelee pia kuhakikisha kwamba madeni yote au kodi zote zinalipwa. Mheshimiwa Hawa pia kazungumzia hili, nadhani yale yote yanayodaiwa kwa Serikali, yaani hayabagui; uwe ni ardhi uwe ni nani unadaiwa, lakini tunawadai fedha nyingi sana, ndiyo maana tunasema tutazidi kuzifuatilia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wamesema pia Wizara iagize wamiliki wote wa ardhi waingizwe kwenye mfumo. Tunaendelea kwa kutumia mfumo wetu unganishi wa ILMIS ambao sasa hivi unatumika kwa asilimia zote Dar es Salaam na mwaka huu wa fedha tunakwenda kuanza hapa Dodoma. Kwa hiyo pia itarahisisha kuweza kuwatambua wamiliki wote na kuweza kujua.

Mheshimiwa Naibu Spika, wanaongelea pia Wizara kuandaa mikakati madhubuti ya kusimamia Maafisa Ardhi katika Halmashauri zetu. Naomba tuseme tu kwamba pamoja na kwamba Serikali imehuisha muundo wa ajira kwa Watumishi wa Sekta ya Ardhi na kuwaleta katika Wizara ya Ardhi kwa maana ya ajira pamoja na nidhamu, bado majukumu yao kama watendaji wako chini ya Halmashauri zetu. Kwa hiyo, ni jukumu la Halmashauri, hasa Wakurugenzi, kuhakikisha kwamba watumishi hawa wanawatumia katika kazi za upangaji, kupima na kumilikisha ili kasi iendelee kuwa vilevile. Kwa sababu kuletwa huku wengi wamekuwa pia wakijisahau, wanafikiri kwamba sasa wametolewa majukumu yao kwenye Halmashauri na wameletwa Wizarani. Wizarani tunasimamia suala zima la ajira na nidhamu, lakini kiutendaji, operational-wise ni a hundred percent wako chini ya Halmashauri.

Mheshimiwa Naibu Spika, wamezungumzia suala la gawio stahiki kwa wakati liende kwenye Mamlaka za Mitaa. Naomba niseme tu, bahati nzuri Mheshimiwa Mabula amezungumza; retention ya 30 percent ilishaondolewa, na mliondoa hapa hapa Bungeni 2016/2017. Kwa hiyo, sasa hivi tunachofanya kama Wizara, ili kuzifanya Halmashauri zifanye kazi, ndiyo hiyo mikopo ambayo haina riba tunaipeleka na tumeendelea kutoa katika Halmashauri mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama taarifa mmeiona, tulitoa kwa Halmashauri 24. Pendekezo la Kamati linasema walau twende kwenye asilimia 50. Nasi tunasema tumelipokea kama Wizara na wenzetu wa fedha wanasikia kwa sababu tuko Serikali moja. Kwa hiyo tutaliona hili, kwa sababu tunajua huku ukiwekeza unakusanya pesa nyingi zaidi na kwa Halmashauri wanapata own source ya kutosha kutokana na pesa wanazopewa ambazo hazina riba, wanauza viwanja vingi na bado wanabaki na akiba ya kuweza kufanya maendelezo mengine. Kama ambavyo tumeona Mbeya, Ilemela, Kahama, Geita DC, Bariadi – wote haoa wamefanya. Wengine wamezitumia vizuri, baada ya kuwa wameuza viwanja wameweza kununua vitendea kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano Geita DC wamenunua gari; Mbeya wameongeza wigo wa kupima maeneo; Ilemela vivyo hivyo wameongeza wigo. Kwa hiyo, tutafanya kila jitihada kuhakikisha hili linatekelezeka ili tuziwezeshe kwanza Halmashauri zetu kwa kupanua wigo wa kipato cha ndani lakini pia kuhakikisha tunaongeza kasi ya upimaji. Hata hivyo, hii haiondoi wajibu au jukumu kubwa la Halmashauri la kupanga, kupima na kumilikisha. Sisi tunakwenda tu kama ku-support, tunafanya hizi interventions ili kufanya wigo wa upimaji uende kwa kasi na kupima maeneo mengi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna lingine limeongelewa kwamba Wizara ielekeze Halmashauri kupitia Ofisi ya TAMISEMI kutenga bajeti. Hatuielekezi TAMISEMI, isipokuwa tunafanya kazi kama Serikali kwa pamoja. Kwa hiyo, ni jukumu la Halmashauri kutenga bajeti zao na kuhakikisha kwamba hasa kupitia mapato ya ndani, watenge ili waweze kuongeza kasi katika suala zima hili la upimaji. Haya yote yanawezekana iwapo tutafanya kazi kwa kushirikiana ili kuongeza kasi hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni Wizara kuzijengea uwezo Halmashari zetu. Kazi hii tumeshaianza. Kati ya hizo Halmashauri nadhani ni kama 184, tayari Halmashauri 102 tumeshazijengea uwezo wa kuweza kufanya kazi zake vizuri. Kwa hiyo, kazi tumeshaianza na tunaendelea, tutazifikia Halmashauri zote 184. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine ya Kamati ilikuwa inasema Wizara iendelee kuwekeza nguvu kwenye kupanga na kupima. Nimeshalizungumzia, ambapo tunashirikiana nao kama Halmashauri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala lingine linasema; kusimamia Halmashauri katika suala zima la marejesho ya mikopo iliyopewa. Katika hatua hii, naomba kwa dhati kabisa tushukuru Kamati zetu mbili, Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira pamoja na Kamati ya Utawala na Serikali za Mitaa na mikoa ambao wameweza kukaa kwa pamoja na kuweza kuyaunganisha majukumu haya na kuweza kuangalia kipi kinaweza kufanyika katika suala zima la ukusanyaji wa madeni? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ambacho tumekubaliana na tunaendelea kuweka mikakati ya pamoja ya kuweza kuona jinsi gani tutasimamia zoezi hili, ni kwamba wale wote wanaodaiwa waliitwa na walipewa taratibu za kulipa wakapewa muda, lakini bado sasa katika kuwapa Halmashauri nyingine tutaweka utaratibu kwa kushirikiana na TAMISEMI ili hata vile vigezo basi vifahamike. Siyo suala tu la kuandika labda proposal analeta halafu anapewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna wengine wameandika proposals nzuri, na ndiyo hao wanadaiwa mpaka leo hawajaleta. Kwa hiyo, bado pia inahitaji kusimamiwa kwa karibu. Nami namshukuru sana Mwenyekiti wa Kamati ya USEMI ambaye alizungumza kwamba hili wanalibeba na wanakwenda kulisimamia kwa nguvu zote ili waweze kwenda sambamba na hilo.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, kengele imeshapiga, lakini mambo yako mengi kweli. Ngoja nijaribu kuona nita-cover yapi, mengine itabidi tuwaletee kwa maandishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, limeongelewa suala la National Housing hapa, hasa kwenye ule mradi wa Kawe ambao wanasema ni Kawe Seven Eleven, kwamba haujakamilika na pengine National Housing walipewa mkopo wakafikia ukomo sasa hawapewi tena.

Mheshimiwa Naibu Spika, habari njema kwa Mbunge wa Kawe pamoja na Mbunge aliyeuliza swali, Mheshimiwa Halima Mdee, ni kwamba sasa hivi Serikali inafanya utaratibu wa kuweza kuwapa pesa waweze kumalizia mradi ule wa Kawe Seven Eleven. Pia Jengo la Morocco Square limeshafikia asilimia 94 ambapo ni uwekezaji mkubwa sana. Pale kuna vyumba zaidi 100 ambavyo vyote vinaingiza pesa, lakini kuna vyumba vingine katika mahoteli viko 80, kuna square meters 120,000 ambavyo vitawekewa maduka. Hivi vyote ni kitega uchumi kwa National Housing. Kwa hiyo, wakimaliza hiyo maana yake ni kwamba wataweza kujitegemea.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia alizungumzia suala la kutoingizwa kwenye bajeti. Suala la National Housing haliingizwi kwenye bajeti ya Wizara kwa sababu ile ni taasisi inayojitegemea, ina bajeti yake na haipati ruzuku kutoka Serikalini. Kwa hiyo, haiwezi kuwa sehemu ya bajeti ya Wizara ya Ardhi, isipokuwa Wizara ya Ardhi ni wasimamizi wa National Housing. Kwa hiyo, shughuli zote zinaofanyika, sisi kama Wizara lazima tuzisimamie na tuziripoti hapa kwenu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna Wabunge pia walitoa hoja zao kwa maandishi ambao sasa nitajibu kiasi kulingana na muda uliobaki. Wamezungumzia suala la ajira za kudumu kwa wenyeviti wa mabaraza. Ni kwamba Serikali kupitia Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa mwaka 2021, imewasilisha Mapendekezo ya Marekebisho ya Sheria ambayo yataleta utatuzi wa migogoro katika sheria hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, marekebisho haya yatarekebisha mfumo wa ajira kwa Wenyeviti wa Mabaraza kwa mikataba yao ile ya miaka mitatu mitatu waliyokuwa wanafanya. Sasa tunataka kuwaweka wawe kwenye ajira za kudumu ili wawe na confidence pia hata wanapofanya kazi zao. Kwa hiyo, hili tumelichukua.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la wazee kutolipwa na nini, nadhani kipindi kilichopita walikuwa chini ya idara nyingine, walikuwa chini ya Kamishna Msaidizi wa Mkoa, lakini sasa hivi wametengewa bajeti yao zaidi ya shilingi bilioni sita. Kwa hiyo, sasa hivi wana kasma yao ambayo inakwenda kuhudumia idara hiyo. Kwa hiyo, haitakuwa na shida tena kama ambavyo ilikuwa hapo mwanzoni.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika suala zima la mabaraza, kila Mbunge aliyechangia alisema habari ya kuwa kwake baraza halipo, ni Wilaya mpya. Tuseme tu kwamba ni mabaraza 111 ambayo yapo kati ya Wilaya karibu 139 ambazo zipo. Sheria inatutaka kila wilaya iwe na baraza lake, lakini Waziri alishaandikia Ma-RAS katika mikoa yote kuleta majina ya Wazee wa Baraza wa kila Wilaya ili wale wachache tulionao kabla hatujapata ajira ya wengine basi waweze kuwa wanakwenda kule kwenye maeneo kusikiliza kesi kwenye wilaya husika, badala ya watu kuja pengine anatoka labda Chemba au wapi kuja Dodoma, basi itabidi Mwenyekiti wa Baraza amfuate yule wa Chemba kule kule kwa sababu kutakuwa na Wazee wa Baraza.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunachoomba katika Halmashauri zetu na wilaya, waandae ofisi ambazo zitatumika kama mabaraza, kwa sababu sisi kama Wizara hatujengi, tunatumia majengo ya Serikali yaliyopo kwenye wilaya husika. Kwa hiyo, hilo nalo tutalitekeleza kwa namna hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, wamezungumzia suala la migogoro katika Jimbo la Newala ambalo limezungumzwa. Naomba niseme migogoro hii inashughulikiwa kwa kutumia Kamati ya Usalama ya Mkoa. Ni wazi kweli viongozi wa Newala hawakushirikishwa, lakini hata hivyo Wizara inajipanga kupitia watalaam wake kwa mwaka huu 2021 watakwenda kutatua suala hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, masuala ya madai ya fidia kwa Mamlaka ya Maji ya Masasi tuseme Wizara inaongea na mamlaka ile ili kuhakikisha hiyo fidia inalipwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la Property Tax ambalo limezungumziwa ya kwamba nyumba zimejengwa ambazo pengine ni za watu masikini, lakini zinadaiwa Property Tax. Nataka tu niseme kwamba Wizara inafanya mawasiliano ya karibu na Ofisi zetu za TAMISEMI ambayo inaratibu kodi hiyo ya majengo ili kuona namna bora ya kushughulikia suala hili. Limeleta kelele kwa sababu hiyo kwamba watu wanaona ni kitu kipya, lakini kwa kawaida majengo yanalipiwa. Sasa ni majengo ya namna gani? Basi utaratibu unafanyika kuweza kujua ni jinsi gani tunaweza kuwafikia hawa na kuweza kuwadai wale wanaostahili.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, hoja zipo nyingi, lakini nashukuru tu. Baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Haya yote yaliyochangiwa tutayatolea maelezo kwa maandishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsanteni, nashukuru. (Makofi)