Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. Hawa Subira Mwaifunga

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia hoja ya Wizara hii ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Kwanza napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema kwa kunijalia afya tele, nimeweza kusimama hapa tena na kuchangaia hoja ya Wizara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa napenda kumpongeza Kamshna wetu wa Mkoa wa Tabora kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuhakikisha kwamba Wana-Tabora na maeneo mengi wanaweza kufanikiwa kupima ardhi na kupata hati zao. Kamashna huyu ametoa ushirikiano mkubwa kwa Wana-UWATA, yaani Umoja wa Wana-Tabora chini ya Mwenyekiti wetu Bwana Othuman Mahango, amefanya kazi kubwa sana. Leo watu wengi sasa katika Manispaa ya Tabora wana hati zao mikononi ambazo zitawawezesha hata kwenda kupata mikopo katika taasisi mbalimbali za kifedha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie kwenye zoezi la urasimishaji. Zoezi hili limekuwa na changamoto nyingi sana, pamoja na kwamba linakwenda lakini limekuwa likienda ndivyo sivyo katika maeneo mengi. Tatizo kubwa liko kwenye baadhi ya makampuni haya yaliyopewa kazi ya kufanya zoezi hili. Kwanza wengi makampuni yao hayana uwezo, hayana vifaa na pia wamekuwa hawana wataalam wa kutosha, hivyo kusababisha zoezi hili kuendelea kusuasua na kuwa zoezi ambalo halionyeshi manufaa kwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa sababu ameliona hili jambo, lakini ameelekeza kwamba angalau haya makampuni yawe yanashirikiana na watendaji katika Halmashauri mbalimbali, lakini kwa masikitiko makubwa, huko ndiko kubaya zaidi kwa makampuni haya, hasa yanayofanya vizuri. Wamekuwa wakidaiwa ten percent sana. Nimwambie Mheshimiwa Waziri, hili linakuwa ni changamoto kubwa sana kwa makampuni haya, inafika mahali wanashindwa kabisa kuelewana na mwisho wa siku hii kazi inakuwa haifanyiki kwa ufanisi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuishauri Wizara, zoezi hili wanapolitoa kwenye haya makampuni angalau waweke deadline ili basi wakati wanaingia ile mikataba, wawaambie kwamba unapopewa hii kazi wahakikishe mpaka muda fulani kazi hii iwe imeshakamilika. Bila hivyo malalamiko yataendelea kuwa mengi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia wakati wa zoezi hili la urasimishaji tungeiomba sana Wizara ifanye utaratibu wa kuhakikisha wanawafikia wananchi, kuwashawishi na kuwaeleza umuhimu wa zoezi hili la urasimishaji kama ambavyo ilivyofanyika katika Jiji la Mbeya; tumefika pale sisi kama Kamati na tumekuta wamefanyiwa urasilimishaji na hakuna changamoto zozote baina ya wananchi na Wizara. Kwa hiyo, niseme tu kwamba zoezi lile limeenda vizuri; na maeneo mengine Mheshimiwa Waziri tunaomba yafanye hivyo ili kupunguza hizi kele na changamoto ambazo zinaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Tabora ni moja kati ya Mikoa ambayo imezungukwa na mapori mengi ya akiba na hifadhi nyingi. Naomba sana Wizara itusaidie katika mkoa wetu kwenda kuainisha mipaka ya maeneo haya ili kuondoa migogoro baina ya Wizara ya Maliasili na wananchi. Kwa kweli naongea kwa masikitiko makubwa kwa sababu moja kati ya migogoro inayosikitisha ni mgogoro uliopo katika Jimbo la Kaliuwa; mgogoro baina ya Hifadhi pale Isawima na wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba sana Mheshimiwa Waziri atusaidie, twende katika Jimbo la Kaliuwa akasaidie kuainisha mipaka ili mipaka ya hifadhi ijulikane na mipaka ya mwisho ya wananchi ijulikane ili wananchi wale waweze kuwa na amani pamoja na Askari wa Hifadhi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie kuhusu hizi fedha ambazo Wizara inazitoa kwa Halmashauri mbalimbali kwa ajili ya kupima, kupanga na kurasimisha. Hizi Halmashauri ambazo zimepata fedha ziko Halmshauri zimefanya vizuri na niseme kuwa nazipongeza ikiwepo Halmashauri ya Mbeya Mjini, lakini zipo Halmashauri ambazo zinafanya masihara na hizi fedha, wanadhani kwamba fedha hizi wamepewa kama bakshishi ama za kwao. Fedha hizi Halmashauri mbalimbali zimepewa ili wapime, Halmashauri nyingine zimepima, zimepata fedha na faida juu, lakini wameshindwa kurejesha fedha hizi ili ziweze kusaidia Halmashauri nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana Wizara, wakati inataka kutoa fedha hii iangalie uwezo wa hizo Halmashauri husika, ili wazipe fedha Halmashauri ambazo zinaweza kupima na kuuza ili waweze kurejesha fedha na Halmashauri nyingine ziweze kupata fedha hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, huu mradi ni mzuri sana, unasaidia sana kupima maeneo mengi. Serikali kupitia Wizara ya Fedha iweze kuongeza fedha katika eneo hili ili Halmashauri nyingi ziweze kupima na kurejesha fedha na kupata fedha katika Halmashauri zao za kuendeleza upimaji wa siku hadi siku. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie eneo la National Housing. Kwa masikitiko makubwa, Halmashauri mbalimbali zimekuwa zikiomba kujengewa nyumba za gharama nafuu kwenye maeneo yao, lakini ulipaji wa fedha hizi umekuwa ni wakusuasua na wakukatisha tamaa kabisa. Tumekwenda Momba kweli, tulijionea hali halisi ya zile nyumba, lakini niseme pamoja na kwamba mkataba wao ulikwisha, lakini bado wameendelea kulipa na tumeona bado wana moyo wa kulipa ili waendelee kuzitumia nyumba zile.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo kuna Halmashauri nyingine yaani wala hawana hata wasiwasi, kuna wengine National Housing wameamua kuchukua Nyumba zao, wameamua kuzipangisha na mwisho wa siku wamepata hasara tofauti na walivyotegemea, ikiwepo Halmashauri ya Uyui.

Mheshimiwa Naibu Spika, naona Mheshimiwa Naibu Waziri ananikumbusha kwamba Uyui; niseme tu ni ukweli kwamba Halmashauri ya Uyui katika Mkoa wangu wa Tabora na yenyewe ni moja kati ya Halmashauri iliyojengewa nyumba 32, lakini Halmashauri ile imeshindwa kuzilipa, mpaka sasa wamelipa shilingi milioni 200 peke yake katika shilingi bilioni 1.8.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni jambo la kusikitisha sana, lakini naomba nishauri kwenye eneo hili, National Housing kupitia Wizara ya Ardhi wana maeneo mazuri katika maeneo ya Miji, ikiwemo katika Jimbo la Tabora Mjini, wana eneo zuri, liko nyuma pale ya TRA, eneo lile lina miundombinu yote, lina barabara, kuna umeme, kuna maji, yaani hakuna shida kabisa. Waende wakawekeze pale, fedha ipo, haina matatizo yoyote. Vile vile kuna maeneo kama Kawe, Bunda Mjini, Tarime Mjini na maeneo mengine ambayo yanaweza kuuzika kwa hizi nyumba kwa haraka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa masikitiko makubwa sana naomba nizungumzie suala zima la madeni ya Serikali katika Wizara hii. Ni aibu kuona Serikali inawadai wananchi wa kawaida, taasisi za kawaida mpaka wanafikia kuwapeleka Mahakamani watu hawa kwa sababu ya madeni, lakini Idara, Taasisi na Wizara za Serikali zina madeni makubwa na ya aibu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiiuliza Wizara wanakwambia wanashindwa kuwapeleka Mahakamani kwa sababu na hiyo ni Serikali. Ningependa kushauri kwenye eneo hili, kama Wizara inashindwa kuwadai wakiwepo wao wenyewe Wizara ya Ardhi, wanadaiwa zaidi ya shilingi milioni 324, wanatakiwa wazilipe, wanashindwa kuzilipa na wao wana deni, kwa hiyo, ningeomba sana fedha hizi kama inashindikana kwa Serikali kupelekana wenyewe kwa wenyewe Mahakamani, basi watusaidie madeni haya ili yapelekwe CAG na CAG aweze kuziita Wizara hizi na Taasisi za Serikali ili tujue hizi fedha zitaletwa lini?

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba sana waweze kutuambia hata Waziri atakapokuja ku-wind-up hapa, atuambie hizi fedha za Serikali zikiwepo kwenye Wizara yake lini zitalipwa? Kwa sababu tunazihitaji hizi fedha, tunahitaji tukapimie watu wetu, tunahitaji hizi fedha kwa matumizi mbalimbali, zilipwe. Watu binafsi wanapelekwa mpaka Mahakamani kwa sababu ya madeni haya, inakuwaje? Wenyewe wa Serikali tuwafanye nini?

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nishauri jambo la mwisho, kumekuwa na Idara ya Mipango Miji katika Wizara hii, lakini bado ujenzi holela umekuwa ukiendelea katika maeneo ya miji mbalimbali. Tungetaka kufahamu idara hii inafanya kazi gani kuzuia ujenzi holela katika maeneo mbalimbali ya miji yetu?

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. (Makofi)