Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. Soud Mohammed Jumah

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Donge

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nami naomba nitoe shukrani zangu za dhati kwa kunipa hii nafasi kuweza kuchangia katika Wizara hii muhimu ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Pia naomba niwashukuru kwa dhati Mheshimiwa Waziri Lukuvi pamoja na Mheshimiwa Naibu Waziri Angelina Mabula na timu yake ya Watendaji ikiongozwa na Ndugu Mary Makondo pamoja na Ndugu Nicholous, Naibu Katibu Mkuu pamoja na timu nzima ya watendaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli, hii timu imefanya kazi nzuri sana katika kipindi cha miaka mitano iliyopita na halikadhalika wanaendelea kufanya vizuri. Napenda kuelekeza mchango wangu katika maeneo mawili na kama muda utaruhusu, basi nitaongeza na mawili madogo. Sehemu ya kwanza kabisa napenda kuelekeza mchango wangu katika masuala mazima ya upimaji na umilikaji wa ardhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama unavyofahamu, wenzangu wengi wamechangia hapa kuhusu umuhimu wa kufanya haraka kupima ardhi yetu ya Tanzania na kuimilikisha ili kuweza kupunguza changamoto ambazo zinakabili ardhi yetu. Kila tukichelewa basi changamoto zinaongezeka na kuna uwezekano, kwa kuwa sasa hivi tuko katika uchumi wa kati wa kiwango cha chini, basi itakuwa Tanzania ni nchi ya mfano ya kuwa na squatters ambao wako katika uchumi wa kati katika daraja la juu. Kwa hiyo, ni vyema tukafanya haraka kuweza kuipima ardhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, takwimu zinatuonesha kwamba kuanzia mwaka 2007 mpaka mwaka 2021 tumeweza kupima ardhi vijiji 2,204 tu. Katika kipindi chote hicho, ni sawa sawa kwamba tumepima vijiji 169 kwa mwaka mmoja na kama trend itaendelea hivi, basi tujue kwamba tunahitaji miaka 58 ili tuweze kukamilisha kuipima ardhi yote ya Tanzania. Yaani ni mwaka 2079 ndiyo tutakuwa tumepima ardhi yote ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bahati nzuri Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020 imeelekeza kwamba tuhakikishe tunaongeza wigo wa upimaji wa ardhi ya Tanzania ili angalau kwa kila mwaka tuweze kupima vijiji 826 ambapo kama tutakwenda na trend hiyo, basi itatuchukua miaka 12 kuweza kupima ardhi yote ya Tanzania. Kwa hiyo, tutakuwa tumepiga hatua kubwa kama tutakuwa tumefanya hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri Lukuvi amefanya kazi nzuri sana. Nami nafikiri hatuna zawadi ya kumpa zaidi ya kumsaidia kuweza kufikia lengo la kuipima ardhi ili atakapoondoka katika Wizara hii ionekane kwamba ameacha legacy ya kumaliza au angalau kupunguza tatizo la upimaji na umilikaji wa ardhi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wenzetu wa ardhi wamefanya kazi kubwa ikiwa ni pamoja na kuwajengea uwezo wenzetu wa Halmashauri. Kuna Halmashauri 102 zimejengewa uwezo kati ya Halmashauri zote 135. Ni kazi kubwa. Halikadhalika wameweza kutenga fungu la shilingi bilioni 3.5 na hizi fedha kuzikopesha Halmashauri na Manispaa ili kuweza kuharakisha au kuchochea upimaji wa ardhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, jambo la kusikitisha, wenzetu wa TAMISEMI nafikiri hawakufanya kama ni core function yao hii ya upimaji na umilikaji wa ardhi. Sasa napenda tuwanasihi sana, tuwaombe na tuwa-task wenzetu wa TAMISEMI waone kwamba suala la upimaji na umilikaji wa ardhi ni core function yao badala ya kuiacha Wizara ya Ardhi kufanya shughuli hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, halikadhalika katika bajeti ambayo amewasilisha Mheshimiwa Waziri hapa, kuna mpango wa kuajiri vijana ambao watakwenda kuongeza wigo wa upimaji wa ardhi. Naomba sana katika ajira hizi, basi tuzingatie sana vyuo vyetu ambavyo vipo Tanzania. Bahati nzuri, namshukuru Mheshimiwa Jafo ameniteua kuwa Balozi wa Mazingira, nashukuru sana kwa nafasi; kwa hiyo, nitumie nafasi hii katika mchango wangu kuweza kunasihi sana Wizara ya Ardhi kwamba wahakikishe kwamba katika upimaji wa ardhi, basi wazingatie masuala ya mazingira kwa sababu ni suala muhimu sana. Bila kuzingatia hilo, inawezekana upimaji huu ukaacha ombwe kubwa sana katika umilikaji na upimaji wa ardhi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wenzetu wa Chuo cha Mipango hapa Dodoma wameshatusaidia kazi, kwa sababu nimeangalia ile content yao ya curriculum ya masomo ya certificate, diploma pamoja na degree na masters degree ya kozi ya Chuo cha Mipango wanatoa Urban Planning and Environmental Management Course kuanzia Cheti mpaka Masters Degree. Hawa vijana hawa tukiwatumia, tayari hii kozi imekuwa well contented kwa sababu, masuala ya mazingira yamo ndani humo; watapima, watamilikisha na watazingatia masuala ya ardhi humo ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nimesikia kwamba hawa vijana wetu wa kozi ya Mipango katika ajira hizi za Wizara ya Ardhi wanaonekana wao ni kama hawahusiki sana, kwamba wao labda ni sehemu ya daraja la pili au la tatu na zaidi wanazingatia vile vyuo vya ardhi. Napenda tu kuiomba Wizara ya Ardhi, nimeangalia course content yao kwa makini, iko vizuri, imeshiba, mpaka remote sensing imo ndani. Kwa hiyo, nafikiri tutakuwa tunafanya makosa makubwa kama hatutawatumia vijana hawa wanaomaliza Chuo cha Mipango Dodoma katika ajira.

Mheshimiwa Naibu Spika, nasikia vilevile kuna tatizo la Scheme of Service kwamba hawakutajwa huko. Kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Waziri wa Utumishi akaliangalia hilo kwa haraka kwa sababu tutakuwa tunasomesha watoto kwa gharama kubwa, chuo kile kina walimu zaidi ya 150, tunawalipa Serikali, tunapoteza pesa, halafu itakuwa hatujawafanyia haki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, haraka haraka kuna suala la wenzetu hawa wanaokwenda kupima visiwa. Naomba tu, visiwa 289 ambavyo vimepimwa, vimekuwa identified, basi hiyo ni step ya kwanza, naomba tuendelee na hatua ya pili kwa kuweza kutayarisha Mpango Kazi na vilevile kutayarisha utaratibu wa kuangalia resource mapping ili tuweze kuona tunaviendeleza vipi kwa sababu kuna uharibifu mwingi wa mazingira katika hivi visiwa vidogo vidogo ambavyo vimo katika maziwa na vilevile katika maeneo ya bahari.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia napenda kuzungumzia jambo moja kumalizia mchango wangu.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kuwasilisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)