Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. Issa Jumanne Mtemvu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibamba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia kwenye Wizara hii muhimu. Kwanza ninayo kila sababu kumpongeza Mheshimiwa Waziri, baba Mkwe wangu Mheshimiwa William Lukuvi, maana nimeoa Ilula pale, Semkinywa, kwa hiyo kwangu Mheshimiwa Waziri ni baba Mkwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze pia Mheshimiwa Naibu Waziri, Dkt. Angeline Mabula, bila kuacha kuwapongeza Watendaji Wakuu wakiongozwa na Bi. Mary Makondo akisaidiwa na Naibu Katibu Mkuu Kaka yangu Nicholas Mkapa. Nawapongeza sana pamoja na wasaidizi wao kwenye Wizara, kwa kweli mnaendelea kufanya kazi vizuri katika ujumla wake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, binafsi nitajielekeza katika maeneo mawili. Hotuba ya Mheshimiwa Waziri ukurasa wa 87 hadi 89 inaeleza sana juu ya urasimishaji, kwa maana ya upangaji, upimaji na umilikishaji wa hati eneo hili, lakini eneo B nitajiekeleza kidogo kwenye mgogoro mdogo uliopo katika Hospitali yetu ya Mloganzila na sio mgogoro ni jinsi ya utatuaji wa jambo lile kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye eneo la urasimishaji baada ya kumpongeza Mheshimiwa Waziri, lakini nimpongeze kimahsusi sana baada ya kukubali maana ni mtiifu sana, kukubali maelekezo ya Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli tarehe 24 mwezi Februari pale Kibamba wakati anazindua ile Stendi ya Magufuli alitoa maelekezo ya kukabidhiwa hati wananchi wa Jimbo la Kibamba na Wilaya ya Ubungo hati ya takribani ekari 52.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa heshima na unyenyekevu mkubwa wa Mheshimiwa Lukuvi alituletea baada ya kufufua mipaka ile hati yenye ukubwa wa ekari 75.2 nampongeza sana, sana Mheshimiwa Waziri. Aliileta ndani ya siku mbili tarehe 26 nikiwepo pale pamoja na Wakurugenzi na Mheshimiwa DC tuliipokea na maelekezo yake. Tumwahidi Waziri tutatekeleza vile ambavyo wanatarajia, hakuna mtu atakula kipande kwa ajili ya kujenga nyumba yake na makazi yake na mkewe au dada yake, tunapeleka maslahi mapana ya wananchi katika eneo lile. Namshukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumze juu ya urasimishaji nimekuwa nikisema hapa na juzi tu tarehe 18 nilikuwa na swali la msingi katika eneo hili na niliongea, lakini leo niseme kwa kuweka vitu sawa, hali ya upimaji ndani ya Wilaya ya Ubungo, lakini hususani Jimbo la Kibamba, ndani ya mitaa yote 43 iliyopo pale, nirudie kusema hali bado si shwari sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, nia yetu ya upangaji, upimaji na umilikishaji tuone wananchi wanaenda kujiinua kiuchumi ndiyo dhamira kubwa na niliwahi kusema hapa hata kauli ya Mheshimiwa Waziri ile ya mwaka 2017 mwezi wa 10 tarehe 23 juu ya kusema jambo hili liende vizuri aone wananchi wanajiinua kiuchumi halijafikia kwenye lengo. Kama sasa tuna hali hii ambayo takribani wananchi 153,000 ambao tayari viwanja vyao vimefikia katika hatua ya upimaji tu wa awali, karibu watu 53 lakini kwa haraka juzi hapa nilijibiwa kwamba takribani viwanja 1,925 tayari vina maombi ya hati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vina maombi 1,900 tuseme 2,000 kutoka 53,000 ambao wameanza au vimeanza kupimwa kwa awali, unaitafuta asilimia hapa huioni ya utija. Taarifa ambazo ninazo kama Mbunge, hati kuandaliwa ni jambo moja, zilizoandaliwa 1,900, lakini hati ambazo zimetoka ni 845 na hii leo niirudie tena, maana Hansard ilikaa vizuri kwenye majibu ya msingi, lakini sio katika maswali yangu ya nyongeza. Hati 845 ndiyo zilitoka kwa wananchi katika mitaa 43 ukigawanya kawaida ukawapa tu kila mtaa hati
19 na point kwa sisi wahasibu tunasema hati 20 kwa kila mtaa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kweli takribani mradi ambao umeanza 2013 wa miaka kumi hadi 2023 tumeambiwa leo asubuhi hapa mradi utaenda kuisha 2023, kwa Kibamba pale umeanza 2017 baada ya kauli ya Mheshimiwa Waziri mpaka 2023 tutakuwa na miaka mitano tu, leo tupo chini ya asilimia 10 ya utoaji hati, yale malengo mahsusi yatafikia? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sina shaka juu ya uwajibikaji wa Mheshimiwa Waziri, lakini najua na nitamwambia anaangushwa sehemu gani. Hali hii ina changamoto nyingi sana, lakini kwenye hili ndiyo maana hawafiki ni kwa kuwa pia kuna shida moja ya mashamba limezungumzwa hapa. Yapo mashamba ambayo kama bado tunaendelea kuchelea kuyafuta hati zake maana yake tutashindwa kufanya upimaji wa jumla wa viwanja vingine ambayo yapo karibu na maeneo hayo. Kwa hiyo nimwombe Mheshimiwa Waziri na hilo pia anaweza akaja kulizungumza juu ya mkakati, kwa sababu nimeona maelezo yake yapo vizuri kabisa, nia njema ya kupima mashamba, lakini pia na kufuta mashamba ambayo yatakuwa hayana tija.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hili eneo, tunazo changamoto karibu tatu, nne na nitazisema na nilieleza hapa. Huu mpango ni mzuri, sina shaka nao, yenyewe program na nia yake ni nzuri, dhamira yake kwa wananchi ni nzuri sana, lakini bado ipo shida juu ya usimamizi wake. Jukumu la Serikali, jukumu la Wizara wala siyo kupanga, wala siyo kupima, wala siyo kuthamini zile ardhi, siyo jukumu lao kimsingi au kisheria, hili ni jukumu la Mamlaka za Miji pamoja na Sekta Binafsi na wameeleza vizuri kwenye hotuba ya Waziri.

Mheshimiwa Naibu Spika, jukumu la Wizara ni kusimamia na kuratibu mambo haya yaende vizuri, lakini lao moja kwa moja ni kuona hati zinatoka ili ile dhima kuu ya jambo hili iweze kufikiwa. Tulivyoanza hili jambo maelekezo ya Wizara kwenye kuratibu yalieleza akaunti zote za urasimishaji zifunguliwe kwa ushirika baina ya mkandarasi na Kamati ya Urasimishaji, kuna shida ikatokea hapo, alivyohusishwa mkandarasi kwenye akaunti zile ndiyo upigaji wa fedha kwenye akaunti za benki ulifanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilieleza juzi tukashindana kwenye figure, hela zimepigwa nyingi leo wananchi wa Jimbo la Kibamba wanalia, lakini wanalia kwa sababu wamekosa majibu. Msimamizi na mratibu akisaidiwa na halmashauri zetu kule hawezi kutoa majibu kwa wananchi waliotoa hela zao. Katika hii hatua ya awali tu, nieleze ukweli, malipo yale ni kati ya 150,000 mpaka 200,000. Ilianza 200,000, mratibu na msimamizi akaona ni nyingi akasaidia 180,000 ikaenda hadi 150,000, watu wamejitahidi kulipa, wapo wanaolipa kidogo kidogo wapo wamelipa kwa ukamilifu, lakini hizi hela zilizolipwa awamu ya kwanza zimepotea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baadaye baada ya Mheshimiwa Waziri kuliona, ndiyo maana namsifia sana, akaja akawaondoa wakandarasi akaacha timu ya Kamati ya Urasimishaji, sasa mambo yanaenda vizuri na najua hata majibu yale ya msingi ni watu 30,000 tu ambao ndiyo wamelipia ni wale baada ya utaratibu umekaa vizuri. Hoja yangu ilikuja hawa kabla wakati wamehusishwa wakandarasi na wakapiga zile hela, thamani ya fedha za wananchi wa jimbo lile zimekwenda wapi? Tunazionaje? Maana hati hamna na hela zao hawajui zilipokwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niliomba juzi hapa kama kweli yule Mtaalam wa Fedha, Mkaguzi wa Fedha na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali kama anaweza kuingia hapa, maana nao wana taratibu zao, lakini nafikiria hizi hela ni za wananchi, wananchi wa Serikali hii na hii hapa ni Kamati yetu ya Ukaguzi, I mean Mdhibiti Mkuu (CAG) apewe nafasi kama siyo yeye nani jicho la tatu, kati ya Serikali na wananchi juu ya hela zilizopigwa, ndiyo nia yangu jicho la tatu liende. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa haraka sana hizo ni fedha, Mheshimiwa Waziri atatwambia mkakati wa Serikali juu ya jicho la tatu kwenye eneo hili. Hata hivyo, kuna makampuni yanasemekana yamefilisika, makampuni kati ya makampuni 162 ambao walitwambia kwenye taarifa zao wameyasajili kama nchi, lakini yapo makampuni 32 yameingia kwenye mchakato huu ndani ya Jimbo la Kibamba, haya makampuni ni ukweli hayafanyi kazi, lakini yapo makampuni yasiyopungua manne, matano mengine yametamkwa yamefisilika na Mheshimiwa Waziri anajua hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimsifie Waziri amewahi kufika kwenye vikao vyake ndani ya mkoa, ndani ya wilaya na akachukua hatua. Zipo hatua amechukua, hatua mojawapo aliyochukua, nishukuru sana na taarifa yake imesema amechukua hatua, ndiyo maana amefuta leseni za kampuni tatu, lakini amechukua hatua kwa kusimamisha kwa muda makampuni tisa, amechukua hatua kwa kuyapa onyo makampuni 41, lakini amezisimamisha kampuni 15, nampongeza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hili la ziada, hayo tu hayatoshi na mengine amewapeleka TAKUKURU wafanye kazi, hakuna majibu kwa wananchi nini mpaka leo na hapa tunaambiwa mwaka mmoja na nusu ujao mradi unaisha, tusije tukawa kama benki tuambiwe, mlango ukifungwa tunapotaka kwenda kuchukua hela ndani ya benki, je, zikiwa nje tunatolewa? Waliokuwepo ndani wamefungiwa huduma itawaishia watu wa ndani? Watuambie au huo mwaka 2023 Mheshimiwa Naibu Waziri jana amezungumza hapa ikiisha ndiyo tunarudi kwenye utaratibu wa kawaida kule kwa furaha, naomba tupate majibu hapa, huu unaishajeishaje na hela zetu hatujui zilipokwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kumaliza kwa sababu siwezi kumaliza yote na hata lile la Mloganzila…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Kengele imeshagonga hata hivyo.

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikushukuru, kwa haya machache niliyosema lakini najua dhima itakuwa imeeleweka na Mheshimiwa Waziri atasema vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja kwa kiwango kinachofaa. Nakushukuru sana. (Makofi)