Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. Jafari Chege Wambura

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Rorya

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwanza kwa kunipa nafasi. Nianze tu kusema kwa kuchangia Wizara ambayo binafsi nimeitumikia kwa zaidi ya miaka kumi. Naweza nikasema tu kwa wepesi kwamba nimepata nafasi ya kuchangia Wizara ambayo imenilea kabla ya kuwa mwanasiasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nitumie nafasi hii kuwashukuru; wa kwanza kabisa Mheshimiwa Waziri, ndugu yangu, mzee wangu, Mheshimiwa William Lukuvi; Naibu Waziri, mama yangu, Mheshimiwa Dkt. Angeline Mabula. Pia nitumie nafasi hii kumshukuru Katibu Mkuu wa Wizara hii, dada yangu Mary Makondo na Naibu wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sitawashukuru wafanyakazi na watendaji wote wa Wizara hii walioko ndani ya Wizara na wale ambao wanafanya shughuli kama wadau, kwa maana ya private sector. Haya mafanikio ambayo tunayaona ya Wizara hii, mimi kwa sababu nimekuwa kule natambua mchango mkubwa wa watu wote kwa ushiriki wao kwa pamoja ili kuhakikisha angalau tunaisukuma Wizara yetu hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitakuwa na maeneo matatu, nafasi ikiniruhusu nitakuwa na eneo la nne la kuchangia kwenye Wizara hii. La kwanza niombe nichangie kwenye ushiriki wa private sector kwenye Wizara hii ya Ardhi. Nianze kwa kusema kwamba ili mwananchi aweze kumilikishwa ardhi, maana yake kuna vitu vitatu au vinne vinakuwa vimefanyika; cha kwanza ni lazima ardhi iwe imepangwa; maana yake katika kupangwa ndiyo kutaainisha matumizi bora ya ardhi ile.

Mheshimiwa Naibu Spika, cha pili, ardhi lazima iwe imepimwa. Kwenye kupimwa ndiyo tunapata ukubwa wa ardhi na maboresho mengine ili mwishoni mwananchi aweze kumilikishwa ardhi ile. Kwa haya matatu tokea Uhuru, toka mwaka 1961, ardhi ambayo imepangwa mpaka sasa tunavyozungumza ni zaidi ya viwanja milioni sita peke yake. Kati hivyo milioni sita, viwanja ambavyo vimepimwa kwa maana ya kwamba sasa vinakwenda ili viweze kupewa ardhi, ni milioni 2.5. Viwanja ambavyo mpaka sasa tunazungumza kwa maana ya umiliki wa mwananchi mmoja mmoja ni milioni 1.5.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushiriki wa private sector kwa mwaka 2015 kwenda 2020 ndiyo tumeanza kufanya shughuli ya urasimishaji kwenye maeneo yetu. Hawa watu, hizi private sector unaweza ukaona katika hiyo milioni sita ambayo ni miaka zaidi ya sitini katika kupanga matumizi ya ardhi, wao wameweza katika urasimishaji peke yake, katika milioni sita maana yake kuna viwanja milioni 1.6, hizi private companies, makampuni ya watu binafsi wameweza kuisaidia Serikali, kwa miaka mitano.Kwa miaka mitano wameweza kupima, kupanga ardhi viwanja zaidi ya milioni 1.6. Lakini total zaidi ya miaka sitini ni zaidi ya viwanja milioni 60; hilo ni la kwanza tu peke yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, katika kupima peke yake kwa miaka mitano toka 2015 hadi 2020, zaidi ya viwanja 557,000 ambavyo vimepimwa katika kazi ya urasimishaji na hizi private companies.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe Mheshimiwa Waziri, kwa kutambua mchango huu pamoja na kwamba amezungumza yapo makampuni ambayo hayafanyi kazi vizuri, tukae nao tuone yale makampuni katika makampuni 163, yale manne ambayo mwanzoni amekuwa akiyasema hayafanyi kazi vizuri, yale 159 twende nayo. Tukiwaweka pembeni hawa tutambue kwamba hawa ndio wana kazi kubwa sana ya kutusaidia sisi. Unaweza kuona kwa miaka mitano namna gani wmaeingia katika shughuli ya kupanga, kupima na mwishoni wakaenda kwenye kurasimisha, namna ambavyo wamefanya kazi kubwa sana. Tusiwahukumu wote kwa pamoja, twende kwenye yale makampuni mengi ambayo yamefanya kazi vizuri tuweze kwenda nayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, juzi nilikuwa namsikiliza Mheshimiwa Waziri wa Kenya, siyo vizuri kusema lakini naomba nitoe kama mfano, alikuwa anazungumza kwa miaka mitano (2015-2020) wao kwa kutumia private sector wameweza kupima viwanja zaidi ya milioni tano. Unaweza ukaona wao wamejikita sana kutumia private sector kwa miaka mitano wamepima viwanja milioni tano. Sisi toka Uhuru bado tuna milioni sita peke yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukiziacha hizi private companies zote tukazihukumu katika mfumo huo maana yake ni kwamba Serikali peke yake ndiyo itaingia kufanya hiyo kazi. Sisi wote tunatambua Waheshimiwa Wabunge, watumishi kwenye halmashauri hawatoshi. Kwa mfano Rorya nina mtumishi mmoja tu Afisa Ardhi. Maana yake sina Mpimaji wala sina mtu wa Mipango. Maana yake tukiwaachia wao wafanye kazi hizi hatutaweza kufikisha malengo, lakini pia hatutatimiza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi katika ukurasa wa 119 ambao umesema kwa muda mchache ili twende na kasi ya kupima maeneo yote.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tutambue kwamba kampuni hizi zimetoa ajira kwa vijana wetu. Kampuni hizi ambazo leo hii tukiziacha pembeni zimekopa mikopo, tukiziacha pembeni zisifanye shughuli hii tutakuwa hatuwatendei haki na yawezekana tukaanzisha mgogoro mkubwa sana kwenye sekta ya ardhi huko mbeleni tunakoelekea.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili ni ushiriki wa halmashauri. Kwa mujibu wa sheria mwenye mamlaka ya upangaji nchi hii ni halmashauri. Hata hivyo, twende mbele turudi nyuma, kazi hii tumeona imebaki ikifanywa sana na Wizara ya Ardhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, juzi wakati tunapitisha bajeti ya Wizara ya TAMISEMI tuliona ndani mle, nilikuwa naona moja ya vipaumbele vyake ni kuhakikisha ardhi yote inapimwa. Hata hivyo, ulikuwa ukienda kwenye bajeti kuona kwamba namna gani wanakwenda kufanya kazi hiyo kama Wizara ya TAMISEMI, hakuna fedha iliyotengwa kwa ajili ya kazi hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo tukirudisha kwamba halmashauri peke yake kwa sababu kwa mujibu wa sheria ndiyo wana mamlaka ya kupanga na kupima wafanye kazi kwa kupitia mapato yao ya ndani, mathalani mimi Rorya nakusanya milioni 800 tu kwa mwaka. Milioni 800 nichukue asilimia 40 iende kwenye shughuli za maendeleo, bado niitoe iende kwa ajili ya kupima ardhi. Hawatakwenda na kasi tunayoizungumza ya miaka mitano ya utekelezaji wa Mpango na Ilani ya Chama chetu Cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii kumwomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha aone namna gani anaiongezea fedha Wizara ya Ardhi, hasa kwenye kipengele hiki cha upimaji ili hizi halmashauri huko chini ziingie kwenye uratibu na kutafuta namna ambayo wanaweza wakapima ardhi kuendana na kasi ya Wizara namna inavyotaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii kuomba sana kwa sababu kama kweli dhamira yetu ni ya pamoja, kwamba angalau sasa zaidi ya eneo la kilometa za mraba 883,000 tumepima asilimia 25 peke yake, tukiiachia Wizara peke yake iendelee na huo mfumo na kwa kutoa maelekezo kwa halmashauri zitafute fedha zenyewe ziende kupima, hatutakuwa tumewatendea haki hawa wananchi wetu. Lakini pia hata Serikali bado tutakuwa tunaimba wimbo uleule na inawezekana tusifikishe malengo yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, la tatu ni ushiriki wa Tume ya Taifa ya Mipango na Matumizi ya Ardhi. Moja ya majukumu ya Tume hii ni kuwezesha mamlaka zote za upangaji wa matumizi ya ardhi katika kutambua mipango ya matumizi ya ardhi, zikiwemo halmashauri zote. Ukienda kwenye bajeti unaweza ukaona tume hii, ndiyo maana miaka yote watu wengine wamekuwa wakisema hatuoni tija ya tume hii, lakini inafanyaje kazi? Unaweza ukaona kwenye fedha ya maendeleo imetengewa bilioni 1.5 peke yake, namna gani itaweza kufanya kazi hii?

Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana nilikwenda mbele nikashauri kwamba kama kweli tuna mpango tumejikita kama Serikali na nchi kwa ujumla tunataka tuhakikishe tunapima ardhi kwa muda mfupi, ni lazima tutengeneze agency. Agencies kama ilivyo TBA, lazima tuwe na wakala ambaye anahusika na shughuli zote za kupanga na kupima ardhi. Ili tunapokwenda kumpangia fedha kwa muda mfupi awe na fedha nyingi lakini utekelezaji wake utakwenda kwa kasi kama ilivyo TBA ambayo ni utekelezaji wa nyumba.

Mheshimiwa Naibu Spika, zipo agencies, wapo mawakala wengi ambao wanafanya kazi kwenye maeneo mengine. Ili tuondokane na hili na ili tuendane na mpango wa miaka mitano kwa kasi, ni lazima tutafute namna ambayo tutaiongezea fedha Tume ya Taifa ya Mipango, lakini tutengeneze agency, shughuli ya kupanga na kupima ardhi isibaki kwenye kurugenzi moja tu peke yake ndani ya Wizara, tujaribu namna ya kuipanua ili iendane na kasi hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, naomba nizungumzie kuhusiana na makazi. Wabunge wengi tumekuwa tukitoa mawazo na michango mingi sana inajikita kwenye ardhi, lakini hatuendi sana kutafuta namna ambavyo tunaweza tukapata suluhu ya upande wa nyumba ili hiyo concept ya Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi iweze kujaa vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii kushauri na pia niweze kuunga mkono maoni ya Kamati kwamba angalau kwa mwaka huu kama ikipendeza, Wizara iweze kukamilisha Housing Policy, Sera ambayo itaratibu shughuli za ujenzi wa nyumba. Hapa Wabunge wengi tumekuwa tukisema namna ambavyo mashirika, kwa mfano, Shirika la Nyumba na Taasisi nyingine, zinajenga nyumba kwa bei kubwa sana. Hata hivyo, leo tukiulizana humu ndani bei elekezi ya ujenzi wa nyumba, mfano Rorya, hatuitambui. Kama tukiwa na Housing Policy maana yake ni nini? Itakuwa na maelekezo ya ujenzi wa nyumba kuanzia ngazi ya mkoa, wilaya na maeneo yote ili hawa wanaojenga nyumba watakuwa wanajenga kwa kutambua bei elekezi iliyopangwa kwenye maeneo yote.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe Mheshimiwa Waziri, kwa mwaka huu angalau sasa tuwe na policy ambayo itatuongoza sote kama Taifa ili tukizungumza Sera ya Nyumba tuwe na Sera ya Nyumba kama zilivyo sera za nyuki na nyingine. Hili litakuwa ni jambo zuri ambalo kimsingi naamini yale maoni mengi ambayo tumekuwa tukiyasema hapa Bungeni namna ya ku-regulate bei za ujenzi wa nyumba itakuwa vizuri na tutakuwa tumei-control vizuri sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, tumekuwa tukiongea naye mara kwa mara; kuna wananchi wangu kule walifanyiwa uthamini toka 2011 Rorya, nafikiri hili analifahamu. Niombe atakapokuwa anakuja kufanya majumuisho angalau na wao wapate jibu. Toka 2011 wamefanyiwa uthamini ili kupisha huduma za umeme, lakini mpaka leo ninavyozungumza kama ambavyo huwa nakwambia wale wananchi hawajalipwa fidia. Ni zaidi sasa ya miaka kumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri, anajua kwa mujibu wa sheria baada ya miezi sita, valuation ile ilitakiwa ipitwe na wakati. Nitumie nafasi hii kumwomba sana Mheshimiwa Waziri atakapofanya majumuisho alizungumzie hili ili na wao waweze kusikia.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)