Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo

Hon. Condester Michael Sichalwe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Momba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi hii naomba kupitia Bunge lako Tukufu kwa heshima na taadhima niombe sana Serikali yangu Sikivu ya Chama Cha Mapinduzi ninaomba kwenu sana sana tunaiomba Serikali yetu tuwatazame wakulima walioko vijijini.

Mheshimiwa Spika, kwa kusema hayo simaanishi kwamba labda wakulima ambao wako mjini hawastahili kuombwa lakini Serikali yangu ya Chama Cha Mapinduzi wakulima hawa ambao wako vijijini ndiyo ambao wamekuwa ni waaminifu kwetu mno katika kutupa kura na sehemu zingine hawaamini hata vyama vya upinzani wanaelewa ni CCM tu. Kwa hiyo, fadhila ya kuwalipa wakulima hawa ni sisi kuwatazama wakulima hawa jamani Benki ya Kilimo haiwafikii huko vijijini Benki ya Kilimo haiwafikii ndiyo maana wamegubikwa na wimbi la hawa watu ambao wanaitwa AMCOS. AMCOS mmewapa watu wa vijijini wawasaidie spidi ya watu wa vijijini hawafanani kabisa na spidi ya watu wa AMCOS, AMCOS ni waongo samahani Waheshimiwa wengine wametumia lugha na kusema ni matapeli. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwenyewe nimehusika katika kusimamia kuendelea kuwaombea mkopo wapiga kura wangu wa Jimbo la Momba ambao walikuwa wameomba AMCOS nimepiga simu kwa mameneja kadhaa wa Branchi husika za wilaya mpaka kwa mameneja wa kanda kwa ajili ya kuendelea kuomba mkopo wananchi wameahidiwa kupewa mkopo kuanzia mwezi wa 12 mpaka sasa wanaendelea kuomba kilimo kinaanza kulimwa kuanzia mwezi wa 11 mpaka wa 12 watalima nini? Hivyo Serikali yangu naomba kwa kuwa iko Benki ya Kilimo ambayo riba yake ni nafuu kwa wapiga kura hawa waaminifu wa Chama Cha Mapinduzi ambao tukienda tunapiga magoti na kugaragara kwao kuwaambia Serikali ya Chama Cha Mapinduzi ni Sikivu basi tuwape kitu ambacho kinafanana na uelewa wao ambao ni Benki ya Kilimo na inatoa riba nafuu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ukisikia mchele mzuri ambao unalimwa Kamsamba unalimwa ndani ya Jimbo la Momba achilia tu kwamba tunalima na kusambaza kwenye mikoa mingine ambayo iko hapa Tanzania lakini mchele ambao tunalima ndani ya Jimbo la Momba tunasambaza mpaka nchi ambazo ziko SADC. Lakini cha kushangaza ndani ya Jimbo la Momba ikiwa kama lilivyo jimbo lenyewe tuna bonde kubwa kabisa ambalo linabeba na mto wa Momba lakini cha kusikitisha tuna skimu moja tu ya umwagiliaji na ambayo na yenyewe haifanyi kama ambavyo inatakikana. Skimu ya umwagiliaji ya Naming’ong’o.

Mheshimiwa Spika, lakini Pamoja na hayo Serikali imeshawahi kutoa kwenye skimu nyingine ya umwagiliaji ambayo iko Iyendo, Kata ya Kapele Zaidi ya pesa milioni 800 na Wizara ya Kilimo wakaunda Tume kwa ajili ya kwenda kukagua skimu hii lakini mpaka sasa tunavyoongea hatujawahi kupewa hata majibu na hatujui nini kinaendelea kuanzia niko Form four na mpaka sasa ni Mbunge, jamani Serikali tunaomba wananchi hawa na wapiga kura hawa ni waadilifu na ni wachapakazi tunaomba tuwawezeshe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini skimu ya umwagiliaji Naming’ong’o kaka angu Bashe nimekufuata mara kadhaa hii skimu Serikali imetoa hela nyingi Zaidi ya bilioni 4.7 ina matatizo kadhaa farm layout kuna shida designing na drawings zina changamoto leveling farm roads mwenyewe nimeitembelea ile skimu mara kadhaa mara nyingi nimeitembelea hakuna mifereji ambayo inaonyesha inatoa maji na inaingiza maji, zile njia zote za kupitishia maji kwenye skimu zimejaa matope basi tunaomba mtupe excavator ili hata wataalamu ambao wako kule tuweze kukwangua wenyewe ile mifereji tunaomba sana.

Mheshimiwa Spika, lakini bonde hili lina zaidi karibu hekta 100,000 za kulima mpunga pamoja na mazao mengine ya umwagiliaji na mbogamboga. Lakini cha kushangaza ndiyo skimu hizo ambayo hata iliyopo yenyewe ni mbovu tunaomba kabisa tupate skimu ya umwagiliaji Kamsamba tupate skimu ya umwagiliaji Msangano, tupate skimu ya umwagiliaji Kasinde, tupate skimu ya umwagiliaji kubwa zaidi kwenye Mto Tesa tunaomba mtuongezee. Kwa sababu mazao yote ambayo tunayazalisha pale kwenye Jimbo la Momba ni tija kwa Mkoa ni tija kwa mikoa mingine lakini Taifa linakusanya mapato ya kutosha kwenye zile nchi za Jirani ambazo tunazitegemea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimekuwepo Zambia muda mrefu wanatumia mchele wa kutoka Tanzania tu na kama Jimbo la Momba ndiyo tuko pale mpakani Kongo wanatumia mchele wa Tanzania tu lakini hata nchi zingine ambazo ziko huko Kusini wanatumia mchele wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini siyo hayo tu kama ambavyo ameongea Mheshimiwa Deus Sangu tunalima pia mahindi yamkini tungeweza kulima hata mara tatu kwa mwaka lakini tutafanyaje mkopo hatupewi tumepewa matapeli AMCOS. Umwagiliaji hakuna sasa huyu mkulima huyu tunamtazamaje aliyepo vijijini? Tunamtazamaje.

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, jambo la mwisho tunaishukuru sana Serikali kwa kutupa soko la mifugo na mazao pale Kakozi lakini tuna vijiji 72 na jiografia jamani ni ngumu. Jiografia ya Jimbo la Momba ni changamoto wapo Waheshimiwa Wabunge ambao wamefika hapo wanaijua ile vijiji 72 ghala moja tu. Mtu aliyoko kule Kamsamba Usoche ili atoe mazao yake kabla yajafikisha kule juu Kakozi hayo maghala hakuna tuna maghala mawili tu na lingine hili halijakamilika liko toka kipindi hicho. Tunaiomba Serikali tunaomba kuongezewa maghala hata kama hayatafika 72 kwenye kila Kijiji lakini angalau basi yafike hata 26 kwa kuanzia tunaiomba sana Serikali ili tuweze kupandisha mazao yetu kufika pale Kakozi.

Mheshimiwa Spika, na jambo lingine la kumalizia tunaomba Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi tuwekewe mkakati mzuri namna gani hawa wakulima hawa wapimiwe ardhi zao ili wawe wanakopesheka na kwenye benki wenyewe wakienda peke yake ardhi ni potential tuko mpakani tunaishia tu kugawa ardhi kwa wazambia na Watanzania kwa sababu hakuna muundombinu mzuri ambao Serikali imeweka kwa wapiga kura hawa, naunga mkono. (Makofi)