Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo

Hon. Saashisha Elinikyo Mafuwe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Hai

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii niweze kuchangia na nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri kwa kuteuliwa na Mheshimiwa Rais, pongezi zangu za kazi nitawapa baada ya kumaliza matatizo ya Ushirika.

Mheshimiwa Spika, pia, ninawashukuru wataalam wakiongozwa na Katibu Mkuu, kwa kweli nimepita kwenye hotuba hii kuna mambo nimeyaona mazuri mazuri hasa ujenzi wa skimu, kwa hiyo, kuna msemo mmoja wa Machame wanasema nyamnya mwishanyo hufoo angalau kuna mambo tumeyaona.

Mheshimiwa Spika, naomba nizungumze kuhusu Ushirika, lakini naomba nizungumze taratibu kabisa leo Mheshimiwa Waziri kaka yangu na Naibu Waziri, wanielewe kwamba huku kuna shida. Katika maeneo yana majizi ni kwenye Ushirika na hao ndio wanaoturudisha nyuma, hao ndio wanafanya kilimo nchi hii kisiendelee. Ukisoma Ilani ya Chama Cha Mapinduzi, imeeleza vizuri nia njema ya chama na Serikali kuhakikisha Ushirika unabadilisha maisha ya watanzania. Naomba kwa ruhusa yako uniruhusu nisome mistari michache tu, kwenye Ilani hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukienda kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi ukurasa wa 30 pale wanasema, Chama Cha Mapinduzi kinaamini kuwa, Ushirika ni njia ya uhakika ya kuwezesha wanachama kuwa na uwezo mkubwa wa kutatua matatizo yao ya kiuchumi, kijamii kwa kutumia juhudi zao za pamoja katika kufikia malengo, hiyo ndio Imani ya Chama Cha Mapinduzi lakini ndio imani ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, uhalisia ni kinyume kabisa na hiki kilichoandikwa hapa, haya Maushirika sasa hivi sio Ushirika tena Mheshimiwa Waziri na wewe unajua, ni watu wachache 7 wanaitwa Bodi za Ushirika ndio wanaoendesha mambo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hawa wanaingia mikataba ya ovyo duniani hujapata ona, anakuja mtu anaitwa mwekezaji, anapewa shamba kwa bei ya kutupa, humo ndani yaliyoandikwa kwenye mikataba ni mambo ya hovyo, ukijaribu kuwaambia naomba tuone wanakuambia sheria ya Ushirika ya mwaka 2013 haimruhusu Mbunge kujua kinachoendelea, haimruhusu Mkuu wa Wilaya, haimruhusu Mkuu wa Mkoa, haimruhusu Mwenyekiti, haimruhusu Diwani, hii kitu gani hii! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, bahati nzuri majuzi nilienda ziara ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii. Tumekwenda kwenye ziara ile na Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii na Naibu Waziri, kwenye chama kimoja cha Ushirika cha Makoa Waziri alipofika kule akaniambia Saashisha sasa nimekuelewa. Ule mkataba ni aibu, vitu vinavyofanyika pale havifai kusema hapa, maana duniani wanatusikiliza watatushangaa kwamba, Tanzania kuna kitu cha namna hii.

Mheshimiwa Spika, mtu anapewa mkataba miaka 60, miaka 30 halafu kwenye ule mkataba kuna madalali zaidi ya saba. Nilisimama pale namueleza Naibu Waziri yuko hapa, dada yangu nilikuwa naye Masanja, nawaambia hebu niambieni ninyi wataalam mmesomeshwa kwa fedha za nchi hii hiki ni nini?

Mheshimiwa Spika, mtu amepewa vibali vya kwenda kuhudumia wanyama hana document yoyote na Vyama hivi vya Ushirika, bado hapa tunasema watu wanaona sijui vitu gani? Ukizungumza kule Hai moja ya kero na iliyosababisha umasikini ni vyama hivi vya Ushirika. Kihistoria nilishasema nia ya Serikali ilikuwa ni nini na sisi kwenye mashamba haya kupitia Ushirika huo huo. Sisi Ushirika wetu kule unachukua Kijiji kizima wanakuwa ni sehemu ya Ushirika. Tulikuwa tunalima kwenye haya mashamba sisi hatuna ardhi ya kutosha kwa hiyo, kwetu sisi nusu heka ni kitu kikubwa mno. Kwenye nusu heka ile tulikuwa tunalima tunapata mahindi, tunapata maharage, tunapata alizeti, tunapata chakula cha ng’ombe.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu, mazingira yetu ya kulima eneo letu limegawanyika kuna sehemu makazi ya watu, lakini kuna sehemu maalum ya kulima. Kule wanapolima watu ndipo ambapo mashamba haya yameshikwa na Ushirika. Asilimia 78 ya mashamba yetu yako chini ya Ushirika, yanaamuliwa na watu saba tu kitu hiki ni hatari. Ni hatari kubwa kwa sababu wao ndio wanaoamua, leo hii tunazungumza mashamba, shamba kama la silver day amepewa mtu pale hajalipa miaka mitatu. Lakini yumo ameshikilia na sisi hatuna pa kulima, ndio maana ilifika mahali nikasema sisi tutaenda kugawana kazi yangu rahisi sana kwasababu, mashamba tunayaona Mheshimiwa Waziri wewe unajua yaani ukifungua moyo wako unajua matatizo yaliyoko kwenye Ushirika tutaenda kugawana mashamba yale sisi wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niwape mfano mmoja, Jumapili moja nilikuwa naingia kanisani tena bahati mbaya nimeingia kwa kuchelewa. Nimefika katikati mama mmoja bibi akanishika shati nikamcheki huyu mama vipi! Ikabidi nitoke naye nje akaniambia Saashisha sikiliza, mimi nimeshiriki kwenye vita ya Uganda niko tayari kupigana tunataka shamba letu la Silver Day. Huyo ni mwananchi wa kawaida tena bibi halafu mnataka Mbunge nije hapa niwasikilize, mimi kuna siku mtaniweka ndani kwenye mambo haya ya Ushirika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, maana kama mashamba tunayaona si tunaenda kugawana tu, hatua 20 nusu heka Masawe chukua, Kimaro chukua tunagawana halafu mtakuja kukutoa na polisi. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, haiwezekani namna hii watu wachache wanafanya maamuzi kwa sababu yetu, tunawaambia hapa fedha zinazolipwa kule hiyo heka moja inakodishwa kwa shilingi 65,000 dola. Tena wanatuwekea viingereza vigumu vigumu, ili kuwababaisha watu dola 65 yule mtu anaenda kumpangisha tena mwananchi kwa shilingi 300,000/= mpaka 350,000/= kwa hiyo, fedha yake aliyokuja nayo inarudi pale pale na mengine yako tupu.

Mheshimiwa Spika, hiyo fedha yenyewe dola 65 haifiki kwa mwananchi, hata kama inafika kwa mwaka kwa mfano, analipwa shilingi 45,000,000/= zinapigwa, zinapigwa mpaka kufika kwenye kile kijiji kinachohusika, inafika shilingi 5,000,000/= unaambiwa ikajenge choo cha shule. Kweli leo tunabadilishana mahindi, maharage, chakula cha ng’ombe na kuondoa ujinga maana mtu asipofanya kazi atakuwa mjinga. Vyote hivi tunabadilishana kwa kujengewa choo cha shule ya msingi! Hapana. Niiombe sasa Serikali ikubali na Mheshimiwa Waziri hili unalimudu kwani hivyo Vyama vya Ushirika kuna miungu si ni watu! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwani ukitamka kuanzia leo Mkoa wa Kilimanjaro nasimamisha viongozi wote wa Ushirika tuunde upya. Nimekaa na Mrajisi nikapita naye document hii hapa nikamuambia Mrajisi hebu tazama yeye mwenyewe anaumia kama mimi. Nimekaa na wewe Mheshimiwa Naibu Waziri na wataalam wako unaumia kama mimi, wale wataalam wako uliosema wakachunguze kule nimekaa nao wanalia kama mimi, hivi kwa nini hatuchukui maamuzi? Kama wote tunaona tuna majizi! Hebu ifike mahali niiombe Serikali iingilie kati, tufanye na sio kwamba nachukia Ushirika napenda Ushirika. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Saashisha muda, unga mkono hoja. (Kicheko)

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa naunga mkono hoja kwa sababu, ameniwekea fedha za umwagiliaji, ahsante. (Makofi)