Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo

Hon. Vita Rashid Kawawa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Namtumbo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo

MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii ili niweze kuchangia katika Wizara yetu hii ya Kilimo. Nawapongeza Waziri, Naibu Waziri na Katibu Mkuu na watalaam wote wa kilimo wa Wizara hii.

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa naomba nijielekeze katika malengo ya kimkakati ya Wizara ya Kilimo ambayo yapo tisa. Moja ya lengo la Wizara ni ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya umwagiliaji, masoko na miundombinu ya uhifadhi wa mazao. Naomba nianze kuzungumzia hili la ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya umwagiliaji.

Mheshimiwa Spika, miradi ya umwagiliaji iliyofanyika ilikuwa ni kukusudia kuongeza uzalishaji kwa wananchi na kwa Taifa zima, lakini ilikuwa haijafanyika tathmini ya miradi hiyo ipoje kwa sasa na je, miradi hiyo ilikamilika? Je, iliyokamilika ina-perform vipi? Uzalishaji wake ukoje? Naona hii tathimini ilikuwa haijafanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunapopeleka fedha za maendeleo katika maeneo kama haya ya kilimo kwenye umwagiliaji tunaenda kujenga fixed asset na fixed asset yoyote lazima tupime wakati inajengwa na inapokamilika, utekelezaji wake baada ya kukamilika, je, kile tulichotarajia kinaleta tija au la?

Mheshimiwa Spika, leo tunawashukuru Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imetuletea dodoso, Wabunge wote tumesambaziwa humu ndani, lakini dodoso hili tulilosambaziwa katika ukurasa wa pili, paragraph ya mwisho, mstari wa tatu kutoka mwanzo, paragraph ya mwisho, inasema:

“Aidha, Tume imeambatanisha orodha ya skimu za umwagiliaji zilizopo katika jimbo lako kutoka katika kanzidata kwa ajili ya rejea yako.”

Mheshimiwa Spika, ukimuuliza Mbunge yoyote humu hakuna list hiyo ya kanzidata humu. Sasa sisi tutajuaje hiyo miradi iliyopo katika kanzidata ambazo wamesema humu. Sasa hata tukijaza humu, tunajaza ile tunayoifahamu, kama mimi nimejaza ile ambayo haifanyi kazi na fedha nyingi zimeingia. Tuna Mradi wa Liyuni umeingia zaidi ya bilioni moja, lakini mradi haujakamilika mpaka leo. Nimekaa katika Ubunge miaka kumi, nikaenda likizo bila malipo miaka mitano ya ubunge, lakini ule mradi nimeukuta vilevile, haujakamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna Mradi wa Likonde, nao umeingia zaidi ya milioni 900, haujakamilika. Kuna Miradi ya Mwangaza, Mbecha na Mahoka, miradi hii haijakamilika, maana yake ilikuwa haijafanyika tathmini miradi ile imekamilika na inafanyaje, ina-perform au hai-perform. Kwa hiyo naomba sana tunapoelekeza fedha hizi lazima kweli tuwe tunaenda kufanya tathmini na ufuatiliaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nawashukuru sana Tume leo wametuletea, lakini tunaomba, naomba na mwongozo wako kwamba tupatiwe hiyo list ya miradi ya kanzidata za Serikali walizonazo ili tuweze ku-compare na tuone hiyo ni miradi ipi iliyokuwepo kule na sisi tuliyonayo ni ipi ambayo fedha nyingi za Serikali zimeingia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo kuna jambo lingine sisi kwetu kule Namtumbo tuna kituo…

T A A R I F A

MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Taarifa, endelea.

MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Spika, nataka nimtaarifu msemaji kwamba kiambatanisho hicho kipo katika hiyo bajeti iliyopo sasa hivi kipo, kinaonekana. Ahsante.

SPIKA: Ukurasa wa ngapi?

MBUNGE FULANI: Kipo Ukurasa wa ngapi?

MHE. ISSA A. MCHUNGAHELE: Mheshimiwa Spika, kipo separate yaani kimekuwa kiko peke yake.

MBUNGE FULANI: Wapi?

MHE. ISSA A. MCHUNGAHELE: Kwenye sehemu ya bajeti, kwenye kishikwambi pale..

SPIKA: Wanasema kwenye kishikwambi, hiyo orodha inapatikana.

MHE. ISSA A. MCHUNGAHELE: Ndiyo kwenye kishikwambi pale, zipo attachment tatu.

SPIKA: Ahsante sana. Endelea Mheshimiwa Vita.

MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na nashukuru kwa taarifa, nitaangalia kwenye kwishikwambi kwa sababu hotuba tumewekewa leo, ila humu hamna. Hili dodoso hili hatuwezi kulifanya leo tukalimaliza leo, kwa sababu kuna ekari humu zinatakiwa tuandike kuna ekari ngapi, maeneo yanayofaa kwa kilimo cha umwagiliaji, kijiji, kata na ekari za maeneo hayo. Kwa hiyo, lazima tupeleke kwa wataalam wetu wa kilimo katika halmashauri zetu, kwa hiyo lazima watupe muda na hili pia na hiyo tutaangalia kwenye vishikwambi vyetu hiyo taarifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kuendelea. Sisi kule Namtumbo tuna Kituo kilichokuwa kinaitwa Shirika la Kilimo Uyole, Suluti au SKU Suluti, Namtumbo. Kituo hicho kilikuwa ni kwa ajili ya uzalishaji na utafiti wa mbegu ambazo zinafaa kwa ajili ya mazingira ya Nyanda za Juu Kusini na hususani Mkoa wa Ruvuma. Kilifanya kazi yake vizuri sana kituo kile, kilikuwa kinazalisha na mbegu za mahindi na mazao mengine mchanganyiko, lakini kituo kile kimekufa. Toka nilipopumzika Ubunge miaka mitano na nimerudi sasa hivi kimekufa kabisa. Majengo yake ni magofu, sisi kwetu kule tunaita mang’oa au mang’oani. Mang’oani ni mahali ambapo waliishi mababu zetu halafu wakahamishwa kwenda kwenye vijiji au kwa jina lingine mahameni.

Mheshimiwa Spika, ukitaka kupajua hapa waliishi watu utakuta miembe mikubwa na yale magofu, mahameni. Sasa hicho kituo ni kama mahame tu, kule kwetu tunaita ling’oa na ni kituo cha Serikali kilichofanya kazi vizuri sana mpaka Mkoa wa Ruvuma ukawa unaonekana ni moja ya big five katika nchi hii kwa kuzalisha mazao ya mahindi, lakini kituo kile kimekufa…(Makofi)

T A A R I F A

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Nimekuona Mheshimiwa, toa taarifa.

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kuniona. Nataka nimpe taarifa Mbunge anayezungumza sasa kwamba na ni suala la mang’oa ni eneo ambalo walikuwa wanaishi watu na watu wale wameshaondoka, inakuwa kama ni eneo ambao ni zama zamadamu, zile kumbukumbu za kale ndivyo ilivyo, ndiyo tafsiri yake. Ahsante sana.

SPIKA: Wote mnaongea lugha moja wote.

MHE. VITA S. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, Ndiyo, tunaongea lugha moja na nashukuru.

SPIKA: Ahsante. Mheshimiwa Vita. Wote Wangoni hawa. (Kicheko)

MHE. VITA S. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, sasa kile kituo kimekuwa kama kumbukumbu tu ya watu wa kale na wakati kilikuwa kinatusaidia na kipo pale na ni ardhi ambayo imehodhiwa na Serikali, lakini ipo ndani ya Mji wa Namtumbo, Kijiji cha Suluti. Tunaiomba Serikali ituambie inapokuja kujibu, kituo kile watakifufua au waturudishie Suluti tuendelee kuifanyia shughuli zingine za kilimo au pale tujenge shule. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili, tuna shamba kubwa lililokuwa linaitwa NAFCO, nalo vilevile limekufa miaka mingi kabisa na hakuna chochote kinachoendelea.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru wamenikatiza, lakini naunga mkono hoja. (Makofi)