Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo

Hon. Masache Njelu Kasaka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lupa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo

MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kupata nafasi niweze kuchangia katika bajeti hii ya Wizara ya Kilimo. Kwanza nimpongeze Waziri pamoja na Naibu Waziri na Wizara kwa ujumla kwa wasilisho zuri lakini pia kwa mwelekeo mzuri kwamba sasa tunaanza kuona dira namna nzuri ya kilimo chetu tutakavyokwenda kukupeleka.

Mheshimiwa Spika, nianze kuchangia kwa kuongelea zao la tumbaku. Zao la tumbaku sasa hivi limekuwa halina tija tena kwa mkulima, wakulima wetu sasa wanalima kwa mazoea maana yake hawanufaiki nalo tena. Kama tunataka kuwakomba wakulima wetu hawa lazima tujielekeze kwenye masoko ya uhakika. Makampuni ya ununuzi yanapokuja huwa yanaweka makisio ya kununua na kulima. Kwa hiyo, huyu mkulima wetu hata alime vipi kama atakuwa amelima zaidi ya yale makisio aliyowekewa maana yake tumbaku yake haiwezi kununuliwa.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa hivi kwa wakulima wetu hawa wadogowadogo kwa mkulima mmoja wao wanaruhusiwa kulima heka mbili tu pekee lakini kwa gharama anayotumia kulima kwa heka mbili hana uwezo wa kulima heka tatu. Shida ni kwamba hata akilima kwa heka tatu maana yake ni kwamba tumbaku yake ambayo itanunuliwa ni ile ya heka mbili. Huyu mkulima ili kumsaidia maana yake lazima aweze kulima zaidi ya heka mbili kwa msimu ndiyo aweze kupata kipato cha kumtosheleza na aweze kupata faida. Namna pekee na tuishauri Serikali ili kuwasaidia wakulima wetu hawa ni kutafuta masoko ya uhakika, makampuni yawepo mengi ili makisio ya hawa wakulima yaweze kuongeza. Hii ndiyo njia pekee ambapo tunaweza tukawasaidia hawa wakulima wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini jambo lingine kwenye suala hili la tumbaku ni haya madaraja yanayopangwa na makampuni kwa ajili ya wakulima wetu. Wakulima hawa wanapokuwa wamelima tumbaku yao wao wenyewe huwa wanai-grade sasa makampuni yanapokuja na yenyewe yanakuja tena kui-grade upya tumbaku ile. Kitengo hiki huwa kinapelekea sasa hapa katikati wale wanaokuja ku-grade kule kwetu wanaonekana kama Mungu amefika, akifika siku hiyo mkulima lazima umnyenyekee, umlishe kuku vizuri ili sasa aweze kui-grade tumbaku yako vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, bila kufanya hivyo tumbaku yako inaweza ikawa kwenye grade nzuri lakini yeye akai-under grade. Bahati mbaya sana kwenye zao letu hili ukishindwa kuuza kwenye kampuni ile maana yake huwezi kuuza tena. Kwa hiyo, tunaishauri sana Serikali ione namna nzuri sana ya kukaa na makampuni haya au wanao-grade tumbaku wawe na watu wao lakini sisi kama Serikali pia tuwe na watu wetu waweze kuhakikisha kwamba hiki ndiyo kiwango ambacho kinatakiwa.

Mheshimiwa Spika, kwenye suala hili la tumbaku pia wafanyakazi wa haya makampuni na wenyewe wanajiingiza kwenda kulangua tumbaku hii. Wanachofanya ni kwenda kununua tumbaku hii kwa wakulima kwa bei ndogo ili baadaye na wao waweze kuja kuuzia makampuni ambayo wanafanyia kazi. Hawa wakulima wasipowauzia tumbaku hii wale wafanyakazi ndiyo baadaye wanashindwa kupata grade bora zaidi na wengine hawapati kabisa masoko katika kununua. Kwa hiyo, naishauri Serikali iweze kuangalia jambo hili.

Mheshimiwa Spika, nizungumze kidogo kwa Wilaya Chunya, lilianzishwa zao mbadala la tumbaku la korosho. Zao hili lililetwa miche, kwa maana Serikali ilitoa ruzuku kuleta miche hii, lakini ilikuja tu awamu ya kwanza baada ya hapo ile miche tena haikuja. Baadaye halmashauri na yenyewe ilijitahidi kutoa fedha zake kununua miche na kuwapatia wakulima wetu hawa lakini na wao wamefika hatua nao wameshindwa. Sisi wakulima wetu wa Wilaya ya Chunya wanashindwa kuipata hii miche mizuri zaidi ili wawekeze kwenye zao hili la korosho.

Mheshimiwa Spika, lakini pia kwenye zao hili la korosho kwa kuwa ni zao jipya Maafisa Ugani wetu ambao wapo kule Wilaya ya Chunya bado na wao hawajaweza kupata elimu ya kutosha kuhusu zao hili la korosho. Mimi niishauri Wizara kupitia TARI-Naliendele waweze kuleta wataalam wao mara kwa mara kwa Maafisa Ugani wetu hawa ili waweze kuwapa hii elimu na wao Maafisa Ugani wetu kwa kuwa ndiyo wanakaa kulekule na wakulima hawa waweze kuwapa hii elimu ya mara kwa mara. Hii itaweza kutusaidia sana na hili zao liweze kwenda vizuri zaidi. Sisi tunaamini zao mbadala la tumbaku ni korosho, kwa hiyo, lazima tuwekeze kwa kiasi kikubwa ili hili zao liweze kuwasaidia wakulima wetu.

Mheshimiwa Spika, pia nizungumizie suala la umwagiliaji. Wilaya yetu ya chunya tulipata bahati ya kuwa na skimu ya umwagiliaji katika Kata ya Ifumbo. Skimu hii ilianza zaidi ya miaka kumi iliyopita, ilianza kwa za ufadhili wa nje baadaye Serikali ikaja kutoa fedha zake lakini mara ya mwisho Serikali kutoa fedha mwaka 2013, fedha zilizowekezwa pale ni zaidi ya bilioni moja lakini mpaka leo tunasema zile fedha tulizitupa pale. Niiombe Serikali kupitia Wizara ya Kilimo iweze kuipitia hii miradi ambayo ilisimama kwa muda mrefu, ione tatizo lilikwamia wapi ili baadaye waweze kuweka fedha na lile dhumuni kubwa ambalo lillikuwa limekusudiwa kwa ajili ya kujenga hizi skimu liweze kuwasaidia wananchi wa maeneo husika.

Mheshimiwa Spika, Kata ya Ifumbo tunaitegemea sana kwa Wilaya ya Chunya kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji. Skimu ile ikiweza kupata fedha za kutosha na ikianza kufanya kazi maana yake mbogamboga na vyakula vyote vinavyozalishwa kwenye skimu za umwagiliaji tutaweza kupata kutoka Kata hii ya Ifumbo. Wilaya ya Chunya ambayo tunaona kama kame nako tutaweza kupata mazao mengi.

Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)