Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo

Hon. Conchesta Leonce Rwamlaza

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo

MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia machache juu ya hoja iliyopo mbele yetu ya bajeti ya Kilimo.

Mheshimiwa Spika, niende kwenye huduma za ugani katika nchi yetu. Tunapofikiria kilimo na hasa kwa wanakijiji huku ngazi ya chini, tunahitaji Maafisa Ugani ili wananchi, hawa wakulima waweze kufundishwa na ni tabia ya wanadamu kwamba kila wakati wanapenda kufundishwa kupewa utaalam. Kuna uhaba mkubwa wa Maafisa Ugani. Kwa mfano, nchi nzima mpaka sasa hivi imeajiri Maafisa Ugani 6,700. Kwa hiyo, kuna upungufu mkubwa wa zaidi ya 14,000 na ushee ya Maafisa Ugani katika nchi yetu. Kwa hiyo, ukija kuangalia waliopo ni kama asilimia 36 tu.

Mheshimiwa Spika, hatutegemei kilimo chetu kitakua hasa kwa ngazi ya chini kama hatuna wataalam wa kusaidia wakulima. Mambo ya zamani hayawezi kwenda wakati huu, lakini tunaweza kuchukua mambo mazuri ya zamani tukachanganya na mambo ya sasa hivi. Hebu tuchukue Awamu ya Kwanza ya Nchi yetu ilikuwa inapelekaje kilimo. Tuangalie miaka hiyo na sasa tuchukue yale mazuri. Kwa mfano, sisi ambao tuna umri wetu tulishuhudia ni namna gani Mabwana Shamba walikuwa wanafika katika mashamba ya wazazi wetu kufundisha kilimo cha migomba kwa mfano Mkoa wa Kagera, kilimo cha kahawa na mambo mbalimbali. Kwa hiyo, tuna haja ya kuhakikisha kwamba tunaajiri Maafisa Ugani ili waweze kusaidia wakulima wetu, tuone kama kilimo hiki kinaweza kuleta tija na wakulima wanaweza kuzalisha vizuri zaidi.

Mheshimiwa Spika, nasema hivi kwa sababu tunajua mashamba tuliyonayo siyo mashamba makubwa na nchi hii imeweza kutunzwa na wale wakulima wadogo ambao wanaitwa small scale farmers, wamelima wemeweza kulisha nchi hii, kwa hiyo wanahitaji utaalam, wanahitaji Maafisa Ugani katika kila kijiji kama mwongozo wa ugani ulivyo katika nchi yetu. Kwa hiyo, tunahitaji pia maafisa ugani hawa wafundishwe mbinu za kisasa. Kwa sababu kilimo tunachoendesha kipindi hiki ni owner’s risk, kila mtu anafanya anavyoona. Haya mashamba darasa aliyoyataja Mheshimiwa Waziri hapa hayapo na kama yapo yanafanya kazi kwa wakati ule na yanatumia pesa nyingi.

Mheshimiwa Spika, mimi nalima migomba siyo mingi, lakini nina shamba la migomba sijawahi kabisa katika kijiji changu kuona Afisa Ugani hata mmoja. Kwa hiyo kila mtu anafanya anavyotaka na anavyoona inafaa. Kwa hiyo natoa ushauri kwamba, Serikali ijitahidi kuhakikisha kwamba tunapata ugani, tunapata wataalam, wapo vyuo ni vingi, watoto wetu wanasoma, hata kule Bukoba ukienda kwenye Chuo cha Maruku pale watu wanamaliza kila mwaka, lakini hawana mahali pa kwenda na wale walio na kazi sasa hawana vitendea kazi. Hawana hata zile kit wanazozisema zile za kupima udongo hawana. Hawana usafiri, wamekaa maofisini, hata hawa 6,000 tunaowasema wapo maofisini kule kwenye kata, hawaendi vijijini kwa sababu hawana usafiri.

Mheshimiwa Spika, nije kwenye ushirika; nimesoma ukurasa wa 11 ya hotuba ya Waziri, ametaja idadi ya watu walioingia kwenye ushirika kutoka milioni tano kwenda milioni sita. Hoja yangu ni kwamba, hapa tusiangalie idadi ya wananchi ambao wanajiunga katika ushirika, tuangalie kazi ya ushirika ni nini na ufanisi wake.

Mheshimiwa Spika, ushirika wa sasa hivi kazi yake ni kununua mazao na kuuza, hawasaidii katika kuhakikisha wakulima wanapata production. Nategemea kwamba ushirika kama ulivyokuwa wa zamani ungeweza kuwa wa mashamba ya miti, ungeweza kuwa na Maafisa Ugani pia.

Mheshimiwa Spika, naangalia Chama cha Ushirika cha Kagera by then BCU, kilikuwa na Maafisa Ugani, kilikuwa na nyenzo zake, Serikali huku na ushirika huku. Kwa hiyo, ina maana kama ushirika wenyewe utafanya kazi ya kununua na kuuza, hawasaidii hata kidogo katika production kwamba, je, wakulima hawa ambao wanatuuzia mazao wanalima na wanapata mazao mazuri? Kwa hiyo, naishauri Serikali kwamba ushirika pamoja na Wizara ya Kilimo wafanye kazi kwa pamoja ili watakaposhindwa kuajiri Maafisa Ugani, ushirika uajiri Maafisa Ugani wake. Pia ushirika utafute masoko, huko nyuma ushirika ulikuwa unatafuta masoko, masoko hatuwezi kuwaachia Serikali peke yake.

Mheshimiwa Spika, nilikuwa natazama leo, kwa mfano, sisi Mkoa wa Kagera tunauza kahawa au tuseme wakulima wanauza kwa Sh.1,200 sasa hivi, lakini kwa bei ya leo ninapokwambia Uganda wanauza kahawa au wananunua kahawa ya kulima kwa Sh.1,500/= mpaka Sh.1,700/=. Je, nani anaangalia everyday exchange, kwa sababu ukiangalia wao sasa hivi kwa bei ya leo ni 0.67 dola, mpaka 0.7 dola. Sasa kama Serikali haiwezi kutafuta masoko, basi na ushirika na wenyewe wawajibike katika kuhakikisha kwamba wakulima wanapewa bei nzuri.

Mheshimiwa Spika, leo Mheshimiwa Anatropia aliuliza swali kuhusu masoko ya Mkoa wa Kagera, lakini walituambia kutokuwa na masoko katika mipaka kwa mfano, Mtukula pale, nani anawajibika, ni Serikali, ni Wizara ya Kilimo au ni Wizara ya biashara? Kwa hiyo, wote kwa pamoja wanaweza kuliangalia hilo. Kwa mfano, ukienda Mtukula tunavuka sisi watu watu wa Kagera kwenda kununua bidhaa Uganda, lakini hatuna Waganda wanaokuja kununua huku kwetu.

Mheshimiwa Spika, ina maana kungekuwa na soko pale mpakani ni kwamba tungekuwa tunapeleka michele pale pale, halafu Waganda wenyewe wanakuja kule kule kwetu wanakuja kununua, lakini tuna ndizi. Ukienda Uganda, ukienda Entebe Airport pale unakuta ndizi zinasafirishwa kwenda Arabuni, lakini sisi Mkoa wa Kagera hatuna soko kwa hiyo, tunaomba Wizara ya Kilimo isaidie katika kutafuta masoko, ushirika usaidie katika kutafuta masoko kuonyesha kwamba hata sisi katika mkoa wetu tuna uwezo wa kupeleka ndizi zikaenda kuuzwa katika nchi za Uarabuni, Oman, Saudi Arabia na nyinginezo.

Mheshimiwa Spika, ninachotaka kusema kingine ni kilimo chetu hiki katika nchi yetu kina mtazamo gani yaani perception yake. Je, kizazi hiki kilichopo kinaonaje kilimo, kizazi hiki kilichopo kinaona kilimo kama adhabu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)