Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo

Hon. Aloyce Andrew Kwezi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kaliua

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo

MHE. ALOYCE A. KWEZI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Binafsi nakushukuru wewe kwa hekima na busara zako za kuongoza Bunge letu. Pia nichukue nafasi hii kuwapongeza sana Waziri, Naibu Waziri na timu nzima ya watendaji kwenye Wizara ya Kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimesimama hapa kwa niaba ya wananchi wa Wilaya ya Kaliua hususani Mkoa wetu mzima wa Tabora kuhusiana na zao la tumbaku. Naomba Wizara hii itusaidie, kwanza kabisa kwenye zao la tumbaku kumejitokeza changamoto kwenye soko. Bei elekezi ya zao la tumbaku Serikali imetoa ni dola 1.61 lakini pia gharama ya mkulima kuzalisha anatumia dola 1.4, wanunuzi walipokuja wamenunua chini hata ya gharama ya wakulima; wamenunua chini ya dola 1.2. Haya yametokea siyo kwenye Jimbo la Kaliua peke yake pia yametokea kwenye maeneo ya Usimba, Kasungu, Kaliua Rural, Kamsekwa, Igwisi na maeneo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, zao hili la tumbaku limekuwa na changamoto, ambaye ananunua vizuri kabisa ni kampuni ya GTI, lakini kampuni ya Alliance One wamenunua tofauti kabisa wakati wale ma-valuer wa Serikali wamefika wakatathmini bei ikaonekana ni nzuri walipofika GTI wakanunua kwa bei nzuri lakini walipokuja kununua hawa Alliance One wamenunua kwa bei ya chini sana ambayo inaumiza wakulima. Naomba Wizara iingilie kati kuhakikisha masoko ambayo yamefanyika katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita bei ya wakulima iweze kupanda kama tathmini ya Serikali ilivyokuwa imesema. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niongelee CSR kwenye kampuni hizi, kampuni ya GTI hii imetusaidia sana inatoa CSR, tunajua madhara pia ya tumbaku, wanatu-support madarasa, zahanati, vituo vya afya, hata mimi kwangu Usinge wameleta milioni 500. Huyu Allowance One ambaye ananunua sana tumbaku kule hata CSR kwa maana ya huduma za jamii ha-support. Sasa kwa nini yeye anakuwa tofauti na wanunuzi wengine? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna kampuni ya Grand Tobacco Limited pamoja na Majestic, wamenunua tumbaku msimu wa 2019/2020 mpaka sasa hawajalipa wakulima wa tumbaku. Pale kwangu kuna chama kinaitwa Mwamko kinadai shilingi milioni mia moja na moja mpaka sasa hawajawalipa. Kibaya zaidi wamerudi kwenda kufunga mkataba yaani unamdai, hajalipa, halafu umefunga mikataba na vyama vya msingi. Naibu Waziri alikuja akatuahidi kulishughulikia lakini muafaka bado, naomba Bunge litusaidie kwenye zao hili la tumbaku. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye zao hili hili la tumbaku nashangaa sana tumewekewa ukomo wa kulima yaani wewe unaambiwa zalisha kilo mia mbili wakati wewe una uwezo wa kuzalisha zaidi ya kilo mia mbili, hii limit kwa nini wanaiweka? Ni kwa nini Wizara isiingilie kati na kuhakikisha tunapata masoko? Lazima tusimame pamoja kupata masoko ya kutosha. Naomba hii limit iondolewe kwa wakulima wazalishe kadri ya pembejeo wanazopata na uwezo walionao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba pia Wizara itusaidie kuhusiana na kilimo cha alizeti katika Mkoa wa Tabora. Tabora alizeti inakubali, Singida na Tabora unaitofautishaje, hali ya hewa ya Kaliua, Urambo, Igalula, Nzega na Igunga inafanana na alizeti tunalima. Hizi mbegu ambazo zimesambaza kwenye mikoa mitano kama alivyokuwa analia wa Kilimanjaro tunaomba zifike Tabora. Kwa heshima zote nawaomba waingilie kati watusaidie. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini niwapongeze kwa jambo kubwa sana, jiografia ya Kigoma inafanana na ya Tabora, mmetusaidia kwenye Jimbo la Kaliua mmetuletea michikichi miche karibu laki moja na nusu. Naomba sambazeni miche ile katika mkoa wote wa Tabora kwa sababu haya mazao yanakubali kwenye Mkoa wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nizungumzie suala la pembejeo na nina ushauri; CRDB Bank na mabenki mengine yanatusaidia lakini Benki yetu ya Kilimo kwa nini isitusaidie kwa sababu riba ya pembejeo ikitoka kwenye TADB itakuwa ni ya chini kuliko ambavyo ipo kwenye mabenki mengine. Asilimia nane ni kubwa, naamini hata kule wanako-support kama TADB akisimama vizuri tutakuwa na mchango mzuri sana na wananchi watanufaika sana kwa sababu asilimia 80 ni wakulima na sisi tumesimama hapa leo tumesomeshwa na wakulima, kama siyo alizeti basi ni kahawa, kama siyo tumbaku basi ni zao lingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu wa mwisho uende kwenye kilimo cha umwagiliaji. Yapo maeneo tunapoteza maji, mafuriko yanatokea hivi tumeshindwa ku-design mabwawa ya kutosha ili kila kiangazi tuzalishe nyanya, vitunguu na mazao mengine ya umwagaliaji. Hatuna sababu ya kudharau kilimo cha umwagiliaji. Nawaomba Kata ya Zugimlole tuwekeeni bwawa pale, Igwisi tumesha design bwawa tunaomba mtuletee fedha, lakini Igagala Namba Tano tume-design bwawa, tunaomba mtuletee fedha hizo ili ziweze kutusaidia.

Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa kuwapongeza Wizara hii kwa umakini, unapowapa taarifa wanakuja haraka na wanatusaidia kutatua migogoro mbalimbali. Kwa hiyo, mimi nikuombe Mheshimiwa Waziri Profesa wangu na Naibu wako makini kabisa Mheshimiwa Bashe, msilale, hiki kilimo ndiyo kinatufanya sisi tuonekane tumetekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa siyo kwa umuhimu CSR nyingi sisi tunazipata kupitia mazao ambayo yanapatikana kwetu na hususani tumbaku. Halmashauri zetu mapato ya ndani zinategemea kwenye tumbaku, naomba hawa watu muwabane walipe, wanapolipa Halmashauri zikapata mapato ndiyo tunaweza kusaidia Serikali Kuu kwenye ujenzi wa vituo vya afya, barabara, kununua mitambo ya barabara na mambo mengine ya msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema haya, nashukuru kwa hekima na upendeleo ambao umenipatia mimi. Nakushukuru sana, Mungu akubariki, naunga mkono hoja asilimia mia moja. (Makofi)