Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo

Hon. Njalu Daudi Silanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Itilima

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo

MHE. NJALU D. SILANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuchangia hotuba hii muhimu sana ya Mheshimiwa Waziri wa Kilimo. Na kwa maelezo yake mazuri sana tunaanza kupata matumaini sisi wakulima wa pamba na wakulima wa mazao mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitazungumzia kwenye suala la uzalishaji, uzalishaji wetu unaenda sambamba na masoko, kama mchangiaji mwenzangu alivyozungumza. 2019/2020 soko lilipokuwa zuri tulizalisha tani 348, mwaka 2021 tukashuka tukazalisha tani 122, sasa ndio utaanza kujiuliza kwamba, katika Mpango wa Bajeti ya Serikali wanapopanga mambo ya kiuchumi na Mheshimiwa Waziri ametuelezea vizuri sana kwamba, tunategemea kupata fedha za kigeni, tunategemea kupata ajira kwa vijana wetu, ni vitu vingi vinavyojumishwa kwenye suala la kilimo na kuwa na fedha nyingi kwenye nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, sasa nilitaka Serikali watusaidie fedha hizi tunazozitenga kila mwaka kwa ajili ya kilimo, lakini fedha hizi hazifiki kwa muda unaotarajiwa, matokeo yake fedha hizi na taasisi kama bodi hizi na nimpongeze tu Mheshimiwa Waziri Bashe jinsi walivyohangaika kupata fedha kwa ajili ya kusaidia wakulima. Na inasababisha taasisi tunazozipa mamlaka hizi zinakuwa na changamoto kubwa sana kwenye suala la kuhamasisha uzalishaji wa mazao ya kimkakati, hususan zao la pamba. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tukisimamia vizuri kwenye kilimo, pamba, alizeti, korosho, hasa mazao mawili hapa, tunakuwa na changamoto ya kulalamika mafuta. Alizeti ikizalishwa kwa wingi na pamba tukizalisha kwa ekari ambazo kwenye takwimu zao wameziorodhesha kilo milioni moja laki tano na hamsini na sita, ukifanya tu wapate kila ekari moja kilo mia nane-mia nane au mia tano-mia tano tutazalisha mwaka mzima. Tutakuwa na mzunguko wa mwaka mzima wa fedha, tutakuwa na mzunguko wa mwaka mzima wa ajira, lakini na train zetu nazozijenga zitasafirisha mzigo kutoka Mwanza kuja Dar-es-Salaam. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, yote hii Mheshimiwa Waziri wa Kilimo tunakutegemea na Ofisi yako na Bodi zako. Na ikienda mbali tunapozungumzia maafisa ugani hawa wanapoendelea kubaki kwenye halmashauri zetu, ni diwani kwenye halmashauri yangu na wote Wabunge ni madiwani, bila kuwa na mkakati mahususi hawa maafisa ugani tunaowatarajia kuwaajiri wakawajibika moja kwa moja kwenye mabodi yetu na ukawapa mikakati na takwimu, tutapiga hatua na tutafika mbali sana, lakini ngonjera hizi za kuzungumza kila siku hatutafika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini suala la pili kuhusiana na dawa. Dawa zetu hizi mnazozileta wataalamu wetu watafiti, umeelezea hawa TARI, n.k., hayauwi wadudu. Hadi mkulima ambaye yuko kijijini kule hajui mambo ya utafiti anakwambia nimepulizia, nimechanganya hiki na hiki, lakini yule funza hafi. Matokeo yake tunarudi kwenye uzalishaji wa chini. Lakini yote haya mukiyawekea utaratibu mzuri naamini kabisa tunaweza tukapiga hatua na Taifa letu likaendelea kupata mapato ya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la mbegu, ningeendelea kuishauri tu Serikali kwamba, tunayo mabwawa ambayo yamechimbwa, tusisubiri sana kila mwaka mpaka msimu wa mvua uanze, lakini huku tuna mabwawa. Bora tuwekeze kwenye mabwawa haya, kwangu jimboni kwangu nina mabwawa karibu manne, Bwawa la Habia, Mwamapalala, Nobola, Sawida na Mwasuguya kule Bariadi, mabwawa makubwa kabisa. Mkiwekeza kwenye suala la mbegu hususan kwenye upande wa pamba na pamba inakamilika kwa miezi minne; ukilima mwezi wa sita mwezi wa kumi na moja unavuna, tayari utakuwa umepata mbegu iliyo bora. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini hivi sasa tunakwenda kwenye uzalishaji unaokuwa chini na sababu zinakuwa ni nyingi, unaweza ukakuta mbegu zilishapitwa na wakati. Sisi kule kwenye pamba tuna mbegu UK91 ya mwaka 91, leo tuko mwaka 2021 ni miaka 20, jambo hili wataalamu mnalifahamu, lakini kwa sababu tunakaa hapa kutimiza wajibu tunabaki kusimama hivyo bila kuzisimamia taratibu na kanuni za uzalishaji bora. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tukiendelea kusimamia hivyo viwanda vyetu tunavyovizungumzia tayari tutapata malighafi ya kuviendesha vile viwanda, lakini tumewekeza sana kwenye miundombinu na mengine, lakini ningeshauri sana Serikali kwa ujumla fedha hizi kwenye suala la kilimo zitoke ili ziweze kufanya kazi nzuri zaidi. Ikishindikana Serikali mwaka uliopita ilikuja na sera, tulikuwa na bodi na taasisi zetu mifuko hii ya kuendesha mazao mbalimbali ikazichukua, changamoto ikaanzia hapo tukashuka kwenye uzalishaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ningeomba kama Serikali kama kuna changamoto humo basi, taasisi hizi za wadau ziruhusiwe kulingana na mifumo iliyokuwa ikiendeshwa ili tuondokane na matatizo haya ambayo yunayapata. Kwa sababu, unakuta dawa inaenda mwezi wa tatu, sasa mwezi wa tatu unaenda kupulizia nini? Tayari na Serikali inaingia kwenye madeni ambayo hayalipiki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunaiomba sana Serikali chini ya Mheshimiwa Waziri na umesema umeunda timu inayoshughulikiwa na Mheshimiwa Bashe, nina imani inaweza ikaleta majibu yakutosha, lakini kubwa zaidi tunalohangaikanalo sisi ni uzalishaji kuwa wenye tija, lakini na masoko yakiwa yenye tija, naamini tunaweza tukazalisha uzalishaji mkubwa tukapata mafuta yakutosha, lakini tukapata ajira za kutosha na tukapata fedha za kigeni za kutosha kwenye maeneo yetu haya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na mzunguko wa kilimo, pale ambapo kilimo kinapokuwa kimezalisha kwa wingi zaidi mzunguko unakuwa ni mkubwa wa fedha kwenye maeneo mbalimbali. Bila kuwa na mzunguko wa kuwasaidia wakulima hatuwezi kupiga hatua hata tufanyaje kwa sababu, hata hizi ndege tunazozinunua watu wanahitaji kupanda, train za mwendo kazi tunazozijenga hizi zinahitaji watu wapande. Nani atapanda hizo train kama watu hawana vyanzo kwenye maeneo yao mbalimbali kwa ajili ya kupata nanilii? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niendelee tu kusisitiza kwamba, ninaendelea kuiunga Serikali mkono kwa maana ya Wizara kwa kazi kubwa ambayo wanaendelea kuifanya chini ya bodi zetu hizi. Naamini tutafanya vizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)