Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

Hon. Sophia Hebron Mwakagenda

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, asante sana na mimi kupata nafasi ya kuchangia katika Wizara hii muhimu. Mimi nitazungumzia suala la hati za kambi za jeshi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninavyojua mimi kwa uzoefu mdogo kwa sababu nilikuwa mtoto wa quarter ninajua kambi nyingi za jeshi zilianza kuwepo, lakini kwa kutokuwa na hati za kumiliki ile ardhi watu wanaingia, mwisho wa siku inaonekana kwamba, jeshi limewavamia wananchi au wananchi wamelivamia jeshi. Kwa hiyo, mimi nilikuwa ninaomba Serikali iweze kujipanga na ninajua pale jeshini kuna wasomi waliosomea wanaweza kujipimia wenyewe bila kutegemea Wizara ya Ardhi, mambo mengine yakafanywa baadaye, lakini angalau wakajipimia wakajua maeneo yao ni yapi wanayoyamiliki, ili iweze kuondoa migogoro mbalimbali ambayo inaonea majeshi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunafahamu kwamba jeshi siku zote lilikuwa linakaa mbali na wananchi na linakuwa na square meter nyingi, lina square meter nyingi kwa ajili ya kumiliki lile eneo, lakini usipopima mtu akaja akajenga mwisho wa siku mwenye hati ndio mwenye mali. Hivyo basi, tunaomba Wizara na ninajua Mheshimiwa Kwandikwa kwa kuja kwako unaweza ukahahakikisha mnapata fedha za kupima kambi za jeshi nchi nzima na kuweza ku--identify maeneo yenu kwa usalama zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapozungumzia wanawake katika jeshi, leo hii Mheshimiwa Waziri ametuletea Majenerali tumewaona tunashukuru, lakini bado tuna haja ya kuongezewa vyeo kwa wanawake zaidi jeshini, hasa kada za chini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunajua wanawake wanaweza, sasa katika wote hatujajua ni wangapi, hatuna statistics kama Bunge tulioletewa kwamba wanawake wangapi ambao wana vyeo hivyo. Sawa leo wamekuja majenerali tunawapongeza na tumeyasema haya mwaka jana na mwaka juzi na miaka iliyopita, lakini bado kada ya masajenti na kuendelea mpaka makapteni waongezeke zaidi wanawake ili waweze kuongezewa vyeo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapozungumzia nyumba za askari; nimesema mimi nimezaliwa kambini; kiukweli kwa mfano flats za pale Keko njia panda ya kwenda uwanja wa Taifa tumehamia pale mwaka 1973, lakini mpaka leo hii maghorofa yale hayajawahi kupakwa rangi. Tunaomba tafadhali Mheshimiwa Kwandikwa pamoja na kwamba, maghorofa mengi yamejengwa kwa ajili ya askari, tunaomba ukarabati wa nyumba za askari uendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini si tu hivyo, bado askari wa rank za chini wanaishi uraiani. Unapokuwa na wanajeshi wanaokaa uraiani kunakuwa hakuna udhibiti wa wale askari kwa sababu hawa watu wanaweza wakaitwa wakati wowote kwa ajili ya kwenda kufanya kazi yoyote kwa muda wowote. Anapokuwa na mama mwenye nyumba mwenye funguo za geti anakaa nazo chumbani, hii si sawa tunaomba jeshi lijenge nyumba zaidi hasa kwa askari wadogo waweze kupata makazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunazungumzia habari za upandishwaji wa v eo nimeshalisema, lakini mwisho wa siku ajira kwa wanajeshi. Tumeona Kamati ya Nje, Ulizni na Usalama (NUU) imezungumza hapa kwamba kuna upungufu wa wafanyakazi jeshini, tunaomba sana ikama inayosimamia wafanyakazi jeshini waweze kuajiriwa. Na tunao vijana wa JKT wengi ambao wamemaliza JKT, kama ni kigezo cha kwenda jeshini basi wachukuliwe vijana wetu hawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikiondoka kwenye jeshi nikaingia kwenye JKT. Leo hii JKT ina vijana wengi sana walinzi, ametoka kuongea Mbunge mchana wa leo kwamba JKT haifanyi tender, mimi sikubalini. Ninaamini katika JKT kupewa malindo mbalimbali katika Taifa hili, tunaogopa sana kuwa na walinzi kwenye benki, kuwa na walinzi kwenye kampuni za kiserikali na mashirika ya umma kutoka nje ya kampuni binafsi. Tunatamani JKT iajiri vijana wengi zaidi kwenye kampuni hizi, lakini shida kubwa iliyopo kwa JKT wanawalipa mshahara mdogo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata wewe mwenyekwe ukiwa unaelekea Mbeya ukipita pale kwenye Bwawa letu la hapo Mtera utakuta vijana kwenye mazingira magumu, mishahara wanayoipata ni midogo. Tunaomba sana kwa sababu unapokwenda kumnunua mlinzi kwenye kampuni unaweza ukawa unapewa laki tano kwa askari mmoja, lakini wale vijana mshahara wanaoupata ni chini ya shilingi 200,000 tunaomba muwaongezee mishahara kusudi wafanye kazi kwa ufanisi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapozungumzia JKT hao hao wenzetu sasa wanafanya mambo mengi ikiwemo mambo ya maji kuna mmoja amasema wafanya mambo makubwa zaidi, lakini sio vibaya kuanza na madogo ili uende kwenye makubwa. Mimi ninashauri mradi wa maji kutoka JKT mashirika yote ya umma, Wabunge na maeneo mengine yote yanayohusiana na Serikali tusitumie maji ya mashirika ya watu binafsi, tulazimishe tutumie maji ya JKT kama kuwasaidia wala msishituke kwa sababu tunataka kuisaidia JKT ili iweze kutoa ajira kwa vijana wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kuelezea suala la Kiwanda cha Nyumbu; wenzangu wengi wameelezea na mimi ninaamini kuna fedha nyingi wamekwisha kupata tunaposema Tanzania ya viwanda tunataka Jeshi letu kwa sababu wao wana dhamana kabwa kwetu tuwekeze fedha nyingi kwao waweze kuzalisha. Nyumbu kama walivyosema waliotangulia ni sehemu ambayo ingekuwa mfano, waliwahi kutengeneza gari, wanatengeneza magari ya zimamoto, tuwekeze fedha ili waweze kutuzalishia zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo siungi hoja, nasisitiza fedha ziongezewe na zile zilizopangwa ziweze kuwafikia wahusika, ahsante sana. (Makofi)