Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

Hon. Khadija Hassan Aboud

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuamsha salama mpaka jioni hii ya leo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa napenda kutoa pongezi za dhati kwa Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Tanzania, Mheshimiwa Rais wetu mpendwa Mama Samia Suluhu Hassan, lakini napenda kuwapongeza Wakuu wa Majeshi yetu yote. Napenda sana kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa kazi kubwa inayofanywa ambayo inahakikisha usalama wa nchi yetu, ulinzi wa nchi yetu na pia kushughulikia mambo mbalimbali ya ustawi wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli napenda kuwapongeza kwa dhati majeshi yetu haya ya ulinzi, nchi iko salama, mipaka ya nchi yetu iko salama na hii inatokana na umahiri wao, lakini uzalendo wao, kujitoa kwao, kujituma kwao na kuwa waadilifu, wakweli na wasikivu kwa nchi yao na Taifa lao. Nawapongeza pia na majeshi yetu yote nchini Tanzania kwa kazi kubwa wanayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikiendelea na mchango wangu kwenye Jeshi la Kujenga Taifa; kazi kubwa inafanyika ya kuandaa vijana wetu, lakini na mimi napenda kuishauri Serikali, katika maandalizi yetu haya ya vijana wetu wa Jeshi la Kujenga Taifa tuendelee kuwapa skills ambazo zitawasaidia kujiajiri, lakini pia zitasaidia kuongeza kipato chao, lakini kipato cha nchi na uchumi wa nchi. Na Jeshi letu hili la Kujenga Taifa tuhakikishe wanaporudi kwenye mitaa yetu au kwenye maeneo yetu wanatumika vizuri na sio badala yake kutumika vibaya. Tuwape scheme au skills ambazo zitawafanya watumike vizuri kwa jamii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikiendelea jeshi letu la ulinzi limeanza tangu mwaka 1964 na katika miaka hiyo ya 1964 kwa mfano kwa upande wa Zanzibar mwaka 1964 kumekuwa na kambi nyingi za kijeshi ambazo kwa maeneo hayo kwa wakati huo ilikuwa ni porini na wananchi hawajawahi kufika huko, lakini kwa mazingira ya sasa hivi baadhi ya kambi zimezungukwa na raia. Tayari zimezungukwa na maeneo ya wananchi, hata magari, madaladala baadhi ya maeneo yanapita chini ya kambi. Wasiwasi wangu ni kwamba kunaweza kukatokea hatari ya kambi yenyewe au hatari kwa kambi yenyewe au kwa wananchi ambao wako jirani na kambi, apa ndio ushauri wangu unapokuja.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni vyema sasa jeshi letu au Wizara yetu hii ya Ulinzi ikawasiliana na Serikali zetu kubadilisha matumizi ya maeneo yale na kuomba maeneo mapya kwa ajili ya kuzihamisha zile baadhi ya kambi ambazo ni hatarishi kwa maisha ya wananchi, lakini pia ni hatarishi kwa jeshi lenyewe. Na kwa kipindi cha mpito nashauri kuna baadhi ya kambi ukipitia nje unawaona walioko ndani na kinachofanyika ndani. Ni vyema basi tukazungusha uzio angalao ile staha ya ile kambi ipatikane, wakati tunajiandaa na kutafuta mbadala wa kambi nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na hayo yako kwa maeneo mengi ya nchi yetu, kambi zimezungukwa na maeneo ya rai ana raia wamekuwa jirani na hizo kambi na nyingine ndio wanachunguliwa mpaka ndani wanaona kinachofanyika ndani. Lile ni jambo hatarishi kwa kambi zetu na usalama wa wanajeshi wenyewe waliomo mle ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine kwenye mipaka ya nchi, naomba Serikali ilione hili la kuhakikisha tunaongeza fedha ili mipaka sahihi ya nchi yetu iwekwe ili kuepusha mkanganyiko wa kugombaniana mipaka na kuleta taharuki kwa nchi. Sasa tuko salama, lakini miaka inakwenda na mambo yanabadilika na mahitaji yanaongezeka kwa kila nchi kwa hivyo ni vyema tukawekeza pia kuchanganua mipaka yetu kwa usahihi baina ya nchi na nchi, baina ya maeneo na maeneo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naendelea na mimi kuchangia kwamba jeshi letu lipewe nyenzo za kisasa zinazolingana na teknolojia ya kisasa na vijana wetu wanajeshi wapewe mafunzo yanayolingana na hali ya kisasa na mabadiliko mbalimbali ya kidunia yanavyojitokeza katika ulinzi wa nchi, mipaka ya nchi na usalama wenyewe wa nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kulipongeza jeshi let una vikosi vyote vya ulinzi kwa kazi kubwa wanayoifanya kuhakikisha nchi yetu iko salama, lakini pia nawapongeza yanapotokea majanga, maafa. Kwenye furaha na kwenye shida wanakuwa pamoja na wananchi bega kwa bega kuhakikisha nchi yetu inafanikiwa katika matukio yote likiwemo tukio la juzi tu la tangu kumuaga na kumsindikiza mpendwa wetu, Rais wetu mpendwa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye sasa ni Hayati Dkt. John Pombe Magufuli. Jeshi hili halikulala usiku wala mchana, lilifanya kazi kubwa kuhakikisha kwanza nchi iko salama, wananchi wako salama na mambo yote yanatekelezeka kwa wakati muafaka na hakuna tatizo lolote lililojitokeza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hilo tuwape hongera kwa umahiri wao pamoja na majemadari wao, makamanda wao kwa kazi kubwa wanayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jeshi letu ni tiifu na bila ya utiifu jeshi hili kusingekuwa na amani hii tunayoizungumza hivi sasa, lakini nalipongeza jeshi letu ni tiifu sana, ni wasikivu na naomba wapokee pongezi zangu hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na katika kuwapongeza hivyo na wao tuwaone kwa sababu mcheza kwao hutunzwa. Wanatusaidia, wanatufurahisha, wanatutengenezea mambo yetu na sisi tuwatunze, tuwaone kwa mahitaji yao zikiwemo nyumba bora, mishahara minono, marupurupu mengine ambayo yatawasaidia kustawisha maisha yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kumalizia naomba niunge mkono hoja, nakushukuru sana kwa nafasi. (Makofi)