Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

Hon. Ali Juma Mohamed

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Shaurimoyo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

MHE. ALI JUMA MOHAMED: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia leo kupata nafasi ya kuchangia katika Wizara hii muhimu Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda sana nimshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi yote ya Ulinzi na Usalama Tanzania, Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa jinsi alivyoanza vizuri kazi yake hii ya Urais wa Jamhuri ya Muungano, kwa kuliwezesha Jeshi letu la wananchi wa Tanzania pamoja na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kuweza kufanya kazi zao kwa ueledi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile napenda nichukue fursa hii adhimu nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri, kwa namna bora alivyowasilisha hotuba yake ya bajeti ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa. Pia napenda sana nimpongeze na kumshukuru sana Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Tanzania CDF, General Mabeyo pamoja na Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Ulinzi Lieutenant General Yacoub Mohamed kwa namna bora wanavyoshirikiana na Mkuu wa Majeshi kwa kuweza kufanya kazi zao kwa ueledi mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa vilevile napenda nilipongeze Jeshi letu kwa kuendelea kulinda mipaka yetu ya Tanzania na mpaka hivi sasa nchi yetu bado iko salama. Napenda nilipongeze Jeshi letu kwa kuendelea kuulinda Muungano wetu wa Tanganyika na Zanzibar na mpaka hivi sasa tumefikia umri wa miaka 57. Vilevile napenda nilishukuru Jeshi letu kwa kuendelea kuyaenzi na kuyalinda Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar nayo pia yametimia umri wa miaka 57. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nilipongeze jeshi letu kwa kuendelea kushiriki katika mission mbalimbali za Kimataifa hususani kule DRC Congo, Darfur Sudan pamoja na Lebanon. Vilevile napenda nilipongeze jeshi letu kwa namna bora wanavyoshirikiana na wananchi wa Tanzania, hasa pale panapotokea majanga na shida mbalimbali za wananchi, wanajitokeza na kuweza kusaidia jamii ya Watanzania na hii inaonesha wazi kuwa jeshi letu ni jeshi la wananchi kweli, ni jeshi la wananchi wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu nilikuwa napenda sana nijielekeze katika mashirikiano kati ya Jeshi la Kujenga Taifa na Jeshi la Kujenga Uchumi Zanzibar. Katika Ilani yetu ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ukurasa wa 157, chama chetu kimetuelekeza kushirikiana kati ya majeshi haya mawili ambayo yana dhamana ya ulinzi, lakini vilevile yana dhamana ya kukuza uchumi wetu wa pande zote mbili. Nilikuwa naomba sana ushirikiano huu uendelee vizuri japokuwa tayari umeshaanza katika kipindi kirefu, lakini nilikuwa naomba sana ushirikiano kati ya JKT na JKU kama yalivyozungumzwa katika Ilani yetu ya Uchaguzi yaendelee ili kuwapa nguvu vijana wetu wa pande zote mbili za Muungano ili kuweza kupata sifa zile za kuweza kujiajiri na kupata sifa za kuweza kuajiriwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi sasa hivi Taifa letu lina vijana wengi ambao hawana kazi, lakini wengi wanategemea wapate ujuzi kupitia majeshi yetu haya mawili. Kwa hiyo, nilikuwa naomba sana kwa upande wa JKU tangu kuasisiwa kwake jeshi hili limekuwa likijihusisha sana na masuala ya kilimo, ufugaji, viwanda vya samani pamoja na michezo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa naomba sana kupitia viongozi wa Jeshi la Kujenga Taifa – JKT waweze kushirikiana vizuri na JKU ili kuweza kuwapa nguvu nao kuweza kupata nguvu zaidi za kuweza kushiriki katika mambo mbalimbali ya Taifa letu na kuweza kukuza uchumi wetu wa Tanzania na katika hili tayari viongozi wetu wameshaonesha nia njema, hivi karibuni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, amewateua baadhi ya viongozi au Maafisa Wakuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kwenda Zanzibar kwenda Wakuu wa Vikosi vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mategemeo yetu uteuzi huu utaweza kaleta tija katika vikosi vyetu hivi vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na ushirikiano ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania pamoja na vikosi vyote vingine ambavyo kwa mujibu wa katiba yetu ni majeshi ya akiba. (Makofi)

Vilevile nilikuwa napenda nilikumbushe Jeshi letu pamoja na Waziri wa Ulinzi kuweza kuongeza nguvu katika ujenzi wa nyumba za askari wetu. Wenzangu wengi wamechangia suala hili, lakini la umuhimu jitihada zimefanyika, lakini naomba pia ziendelee kufanyika ili wanajeshi wetu waweze kuishi katika nyumba bora na kuweza kufanya kazi zao kwa ufanisi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda sana nimuombe Mheshimwia Waziri aendelee na wazo hili la kuweka bima ya afya kwa ajili ya askari wetu pamoja na familia zao. Zoezi limeanza lakini nilikuwa naomba liende kwa haraka ili wanajeshi wetu waweze kufaidika na kupata hamu kubwa ya kuweza kufanya kazi za ulinzi na usalama katika nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Shaurimoyo naunga mkono hoja. (Makofi)