Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

Hon. Esther Nicholus Matiko

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kuweza kunipatia fursa hii na mimi niweze kuchangia kwenye Wizara hii muhimu sana ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitaanza kwanza kwa kupitia utekelezaji wa bajeti ambayo tunatenga kwenye Wizara hii muhimu. Pamoja na unyeti na umuhimu wa Wizara hii kwa miaka yote tumekuwa tukitenga bajeti lakini haziendi kwa ukamilifu. Kwa mfano mwaka 2015/2016, Fungu 57 – Wizara ilitengewa shilingi bilioni 220 fedha ya maendeleo, lakini ilipokea shilingi bilioni 40 tu, sawa na asilimia 18; Fungu 38 – Ngome, tulitenga na kuidhinisha shilingi bilioni nane, hawakupokea chochote; Fungu 39 – JKT, tulitenga shilingi bilioni nne, hawakupokea chochote.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2016/2017 zilitengwa shilingi bilioni 230 Fungu – 57 wakapokea shilingi bilioni 34 tu, sawasawa na asilimia 15; Fungu 38 tulitenga shilingi bilioni 10 wakapokea bilioni moja tu, sawa na asilimia kumi, za maendeleo hizi. Fungu 39 tulitenga bilioni nane wakapokea bilioni moja, sawa na asilimia 12.5.

Mheshimiwa Naibu Spika, 2019/2020 tulitenga shilingi bilioni 220 Fungu 57, shilingi bilioni nane Fungu 38 na shilingi bilioni sita Fungu 39. Lakini mpaka ile Machi hawakutoa taarifa yoyote kwenye hili. Lakini tumeona 2021/2022 utekelezaji wake nao unasuasua.

Mheshimiwa Naibu Spika, hizi ni fedha za maendeleo, na kwa nini nimeamua kufanya hii rejea; kwanza hata fedha ambazo tunapeleka ni ndogo sana. Ametoka kuchangia hapa Mheshimiwa Mwijage, Jeshi la Wananchi wa Tanzania na JKT kwa unyeti wake Jeshi la Wananchi wa Tanzania kulinda mipaka ya nchi dhidi ya adui kutoka nje, lakini pia Jeshi hili ni mbadala kwa nchi yetu pale ambapo inapata mkwamo kwenye sekta zote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, inatakiwa Jeshi hili tuliwezeshe liweze kufanya tafiti za kina, liweze hata kufanya ugunduzi wa mambo mbalimbali, mengine ambayo hatuhitaji kuyajua ambayo yanaweza yakaisaidia nchi yetu kukwamuka kiuchumi. Lakini kwa fedha ambazo tunatenga ndogo na hatupeleki hatuwezi kufika popote.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii hili Jeshi haliwezi hata kujenga maabara ya kisasa yenye teknolojia za kisasa za kuweza kufanya huu utafiti na kuweza kujihakikishia kwamba kama nchi wanaweza ku-counter any crisis ambayo inakuwa imetokea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mathalani, dunia na sisi nchi tuko kwenye hili gonjwa la Covid-19. Kama kweli hili Jeshi tungekuwa tunaliwekeza, ndiyo maana hawa ndugu zetu wako pale kulinda mipaka ya nchi na vitu kama hivyo, yaani hawatumiki 24/7 kama ambavyo majeshi mengine yanafanya, lakini wangeweza kujiwekeza kwa kina kuweza hata kufanya tafiti za kina, wana madaktari wakaweza kugundua dawa ya Covid, wakaweza hata kugundua chanjo tukaachana na ma-debate ya kusema nchi za nje zinaleta chanjo ambazo zinaweza zikatuathiri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ikitokea Jeshi wakabobea kwenye sekta zote, mathalani siombei, unatokea mgomo wa madaktari nchi nzima, hawa wanajeshi wetu wanaweza waka-counter kuweza kuhakikisha kwamba Watanzania hawawezi kufariki pale ambapo wanaendelea kupata matibabu pale ambapo unatokea mgomo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kingine tunaona nchi kama Marekani, wanajeshi wale na nchi nyingine; mimi kuna kipindi nilikuwa nanunua blackberry wameandika research in motion. Zile ni tafiti ambazo zinafanyika na wanajeshi wa Kimarekani. Lakini pia kuna wanajeshi wa nchi mbalimbali, Mheshimiwa Mwijage hapa amelalamika kuhusu Nyumbu, sasa Nyumbu itawezaje kujikwamua wakati hata haipelekewi fedha za kutosha? Tunahitaji ku-invest kwenye Jeshi la Wananchi wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hapo hapo kwenye utekelezaji hafifu wa fedha za maendeleo, kunasababisha kuendelea kuwepo kwa migogoro ya ardhi baina ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania na wananchi ambao wamechukuliwa ardhi ile. Imechukua miaka mingi sana, ni kwa sababu tunapitisha fedha hapa, kwenye vitabu ina- reflect kwamba wanakwenda kupeleka kulipa fidia, lakini miaka inakwenda wananchi hawalipwi fidia na tunajua ndugu zetu hawa wanajeshi, hawatakiwi mtu kukatiza kwenye kambi yao, ukikatiza unapewa adhabu kali sana, utalimishwa, utarukishwa kichura na vingine, ndiyo hivyo caliber ilivyo. Sasa unakuta wakati mwingine wamechukua maeneo ambayo yako kwenye maeneo ya raia ambako watakuwa wanapita.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano mgogoro ulioko Tarime wa Jeshi la Wananchi pamoja na wananchi wa Kenyambi na Bugosi wa Kata za Nkende na Nyamisangura, tumekuwa tukiongea hapa, wanajeshi walikuwa kwenye kambi yao Nyandoto lakini kuna kipindi yalitokea mafuriko wakakaribishwa huku ni kweli, kwa sababu walikuwa hawawezi kupita kipindi hicho hakukuwa na miundombinu, walivyokuja huku wakaamua kuchukua ile ardhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tangu Bunge la Kumi, mwaka 2010, nazungumzia hili suala; pale walipo ile kambi iko katikati ya mji kabisa. Kwa hiyo raia wakipita, kuna wengine wanapita wanakwenda Kata za Bumera au Susuni, kuna wakati wakikatiza pale raia wanachukuliwa wanapewa adhabu za kulima kwa sababu wamekatiza kwenye kambi. Tukasema basi kama wameamua kutwaa ile kambi wawalipe fidia stahiki hawa wananchi kwa wakati; ni zaidi ya miaka 17 sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti ya mwaka jana na mwaka juzi Serikali ilipitisha hapa ikasema inapeleka fidia, tayari wameshatenga fedha, nikshika mpaka na shilingi, ambaye sasa hivi ni Makamu wa Rais ikawa imeshapita wakasema wame-underestimate, wakaenda wakafanya re- evaluation ili watu wale walipwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini leo nimejaribu kupitia, Tarime haipo tena. Ina maana hawa wananchi wataendelea kuteseka, kukaa wamezuiliwa wasikate mti, choo kikibomoka wasijenge, hawafanyi maendeleo yoyote yale wapo tu kwenye kakiota, nyumba ikibomoka wasifanye chochote. This is not right! This isn’t right!

Mheshimiwa Naibu Spika, kama mmeamua kutwaa hata kwa mujibu wa sheria na kanuni za ardhi kama Jeshi limeamua kuchukua, which we respect, basi lipeni fidia. Short of that, Wanajeshi wale warudi kwenye kambi yao kule Nyandoto, after all iko mbali na mji.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja yangu nyingine ni kuhusu wastaafu wetu wanaotokana na Jeshi hili la Wananchi. Tumekuwa tukishuhudia wakishastaafu wanaishi maisha ya shida sana. Kwa sababu hata hiyo lump sum wanayopewa ya asilimia 25 kuna kipindi wanacheleweshewa wengine hawapewi kabisa, lakini hata wakiipata haikidhi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunakubali wote kwamba Jeshi hili ni letu, kama vile ambavyo tunawatambua kada zingine kama Majaji na wengine, wakistaafu wanakuwa wanapata some percent, basi tuangalie hawa wanajeshi wetu wanapostaafu tuwape hata walau asilimia 20 ya mshahara wao wa mwanzo ili waendelee kujikimu na maisha wakiwa uraiani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukizingatia wanajeshi wakiwa kule kambini huwa wanapata vifaa vingi kwa ruzuku. Wameshazoea maisha hayo, wakija huku uraiani wanateseka sana. Lakini on top of that tuwakatie na bima ambayo anaweza akatibiwa muda wowote ule. Mwanajeshi akistaafu any time kuna crisis wanaweza wakawa-recall wakaingia pia kuendelea katika kunusuru nchi. Kwa hiyo, lazima tuwa- consider hata walau kwa asilimia 20, siyo asilimia 80 au 70 wanazopewa hao wengine, walau asilimia 20 ya mshahara ambao alikuwa akiupata wakati anastaafu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Ripoti ya CAG ya mwezi Machi, 2021, ameainisha kwamba SUMA JKT kuna watumishi wanadai fedha, tena Idara ya Ulinzi. Mwaka 2018/2019 walikuwa wanadai milioni 208, mwaka 2019/2020 wakawa wanadai milioni 317, hela inazidi kuongezeka. Sasa kama Idara ya Ulinzi ambayo SUMA JKT wanapeleka kwenye private sector na hata kwenye mashirika ya umma, ina maana kule wanawalipa vizuri, kwa nini hawa watumishi ambao wanakwenda kufanya kazi ya ulinzi wasilipwe fedha zao?

Mheshimiwa Naibu Spika, yaani mimi nafanya kazi ya ulinzi unapokea fedha, lakini hunilipi. Unaweza hata ukashawishika ukajiingiza kwenye uhalifu, badala ya kulinda ukala njama ili uweze kuja kufanya uhalifu kwenye sehemu husika. Kwa hiyo, tunaomba mhakikishe msiwakope watumishi, hasa Idara ya Ulinzi jamani, kuwa kwenye lindo and then unamkopa, isn’t right. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kingine wamezungumza kwa kina hapa, ni kweli tunapeleka vijana wetu JKT, wanapewa mafunzo, lakini hawawezi kuwa absorbed wote kubaki kuajiriwa Jeshini, wa JKT na JKU. Sasa wasipochukuliwa wote Jeshini wengine wanarudi uraiani na unakuta wengine hawajapata mafunzo mbadala, hawezi akastahimili kukaa uraiani hana kazi, atashawishika. Ataingia kwenye magenge ambayo ni ya uhalifu na anajua, amejifunza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa wametoa ushauri mkubwa sana hapa, na mimi na-cement; Jeshi la Kujenga Taifa likiwezesha Tanzania ya viwanda ikawezekanika, tukipeleka fedha za kutosha tutaweza kuwa na kilimo chenye tija. Maana yake vijana wetu wakienda kule watajifunza, watawezeshwa, wakiwezeshwa ina maana tutakuwa na kilimo chenye tija, tutatoa raw material yataenda kwenye viwanda, viwanda vitakuwa vingi kwenye majimbo na mikoa; niliona siku ile Mheshimiwa Jafo anasema viwanda mia kila mkoa.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuwezeshe JKT isiishie tu kufanya mashamba machache, mimi naita mashamba darasa. Kukiwa na maonesho ya Nanenane wanakuja wametengeneza kweli furniture nzuri lakini wana viwanda all over the country, tumewawezesha hawa watu waweze kujenga nchi yetu kweli?

MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, nirudie tena, ukishasema taarifa mara moja unasimama. Ndiyo maana huwa naangalia mtu kasimama wapi. Mheshimiwa Mpembenwe.

T A A R I F A

MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nimpe taarifa mzungumzaji kwamba point anazoziongea ni za msingi na zina maana sana za kusema kwamba tuweze kuwawezesha JKT na Jeshi kwa ujumla wake, lakini nataka tu nimpe taarifa mzungumzaji kwamba mfumo wetu wa bajeti ni cash budget system, tunakusanya halafu ndiyo tunatumia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ninamuomba tu mzungumzaji mimi na yeye na Wabunge wenzangu wengine wote humu ndani tuweze kushirikiana tuwe mabalozi wa kuweza kuhamasisha watu waweze kulipa kodi tukusanye ili Jeshi liweze kuwezeshwa. Ahsante sana. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Esther Matiko, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, cash budget with priorities, kama tunaweza tuka-inject trillions of money kwenye Wizara ya Ujenzi tunashindwa nini kupeleka trillions of money kwenye hii Wizara ambayo tunaiita nyeti? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ni cash budgeting, yes, lakini tunatenga shilingi bilioni 220 na haziendi zinakwenda shilingi bilioni 30 wakati kwingine unakuta bajeti imeenda zaidi ya asilimia 100. Kwa hiyo we need to be serious na tusaidiande kama Wabunge, tukitenga shilingi bilioni 300 na ziende zote katika cash budgeting hiyo hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho ninapenda kusahuri; tunasema ni Jeshi la Wananchi, sasa kama Jeshi la Wananchi liko pale kulinda mipaka ya nchi yetu ndhidi ya adui, lakini kama nilivyosema mwanzo, hii ya kuteua wanajeshi wetu wanakuja kwenye kupewa fursa au kuteuliwa kuwa watendaji Serikalini au Wakuu wa Mikoa, isn’t right. Civilian Government yaani utawala wa kiraia unamuingiza tena mwanajeshi.

Mheshimiwa Naibu Spika, na huku sisi wengine tumeshazoea, ukimuona mwanajeshi kwanza you freeze, yaani nikiona DC mwanajeshi na wanavaa yale mavazi wakiwa kwenye hizi nafasi. Mimi ninashauri sana tuangalie wananjeshi tunawatumia, sijui nieleze vipi! Sasa ukishamuingiza mwanajeshi kwenye system Serikalini, tena wengine, kwa sababu DC na RC ni siasa, it’s a political thing. Yaani ukimuingiza kwenye siasa, it isn’t right.

MHE. CHARLES J. P. MWIJAGE: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Esther Matiko, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Charles Mwijage.

T A A R I F A

MHE. CHARLES J. P. MWIJAGE: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu hili la kutumia wanajeshi kwenye kazi mbalimbali, nataka nimpe taarifa Mheshimiwa Matiko kwamba Jeshi la Tanzania ni Jeshi la namna yake duniani. Ndipo unaweza kumkuta askari anakuja kuchumbia nyumbani kwako, mnacheza na mnakula wote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi nyingine watu wakiona wanajeshi wanatupa kila kitu, hapa sivyo. Wewe ngoja kidogo tutoke nje uje uone nitakavyogongeana na majenerali wananipigia saluti. Sisi wanajeshi ni ndugu zetu, na ukimuona mwanajeshi maekwenda sehemu, jua kuna mambo. Ukimuona Kagera amewekwa nani, Mtwara amewekwa nani, fuatilia kuna mambo. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Esther matiko, malizia mchango wako.

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, napokea taarifa yake, lakini msisitizo wangu ni kwamba ukiwa Mkuu wa Wilaya au Mkuu wa Mkoa, unaingia kwenye Kamati ya Siasa ya CCM ya Wilaya au ya Mkoa; this isn’t right, that’s where my point is, kwa sababu wengine tunawaweka mipakani huko.

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

MHE. ESTHER N. MATIKO: Tulieni jamani.

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, anamalizia muda wake kwa hiyo taarifa moja tu ndiyo inayoruhusiwa hapo. Mheshimiwa Amar.

T A A R I F A

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nimpe taarifa mzungumzaji kwamba hao wanaoteuliwa kuwa Wakuu wa Mikoa, ma-DC, wanakuwa wameshastaafu tayari kutoka Jeshini. (Kicheko)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Esther Matiko, malizia mchango wako.

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, wananimalizia muda wangu tu; Jenerali Mbuge amekwenda hapa, amestaafu lini? Do a bit of research kabla hujatoa taarifa. (Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba sana, wamezungumzia kuhusu nyumba za wanajeshi wetu; ni mbovu sana, dhoofuli hali.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Naibu
Spika, kuhusu utaratibu.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Esther Matiko, kuna Kanuni inavunjwa, Mheshimiwa Jenista, Kanuni.

KUHUSU UTARATIBU

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba tu nimkumbushe Mheshimiwa Esther, Kanuni ya 71(h) ambayo inamzungumzia Mbunge kutokuzungumzia mwenendo wa Rais, Spika ama watu wengine wanaotoa haki.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nataka nimpeleke Mheshimiwa Esther kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ninaomba aende kwenye Ibara ya 36(2) ambayo inasema; Mheshimiwa Rais atakuwa na madaraka ya kuteua watu wa kushika nafasi za madaraka na watawajibika kuweka Sera na Idara na Taasisi za Serikali na mambo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini akienda kwenye Ibara 34(4) inazungumzia pia madaraka ya Mheshimiwa Rais katika kufanya uteuzi. Kwa hiyo, sasa kama madaraka haya ya Rais katika kufanya uteuzi yamewekwa kwa mujibu wa Katiba nadhani si sahihi sana kwetu sisi Wabunge kuanza kuyazungumza madaraka ya Rais ya kufanya uteuzi katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kazi hizi amepewa kwa mujibu wa Katiba na yeye katika Katiba hajafungwa amchague nani, amteue nani, amuache nani. Kwa hiyo, nilikuwa nafikiria kwa kuwa ni suala la kikanuni lakini ni suala la kikatiba haitakuwa sahihi sana sana kuanza kuzungumzia madaraka hayo ya Rais ndani ya Bunge lako Tukufu. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, wakati akichangia Mheshimiwa Esther Nicholas Matiko amesimama Mheshimiwa Jenista, akitoa maelezo kuhusu kanuni zetu namna ambavyo kwa namna moja au nyingine zinavunjwa na mchango wa Mheshimiwa Esther Matiko na ameweka maelezo yake kwenye eneo mojawapo ambalo Mheshimiwa Esther Matiko alikuwa anachangia, nalo eneo hilo linahusu wanajeshi kwenda kuwa sehemu ya Serikali huku uraiani na ametoa mifano ya namna wanavyoteuliwa kuwa Wakuu wa Mikoa na pengine Wilaya ama kuongoza vitengo mbalimbali ambavyo si vya kijeshi, lakini ni vya kiraia.

Waheshimiwa Wabunge, wakati akitusomea Mheshimiwa Jenista Kanuni ya 71(1)(a) ambayo inaelezea namna ambavyo tunakatazwa kufanya mambo kadha wa kadha hapo, lakini pia akatupeleka kwenye Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano Ibara ya 36 na 34 kwamba Rais anapewa hayo mamlaka ya kuteua mtu yeyote ambaye yeye anaona anafaa kwenye nafasi fulani.

Sasa katika, wakati akichangia Mheshimiwa Esther hakuwa amejielekeza kwenye mamlaka ya Rais kuteua, lakini twende taratibu, hakuwa amejielekeza kwenye mamlaka ya Rais kuteua, lakini kwa sababu aliyokuwa anawazungumzia ni wateuliwa wa Rais basi Mheshimiwa Jenista ameona kwamba tukiwajadili wale wanaoteuliwa na Mheshimiwa Rais ni kama vile tunazungumzia mamlaka ya yule aliyeteua kama anayo mamlaka au hana. (Makofi)

Sasa wacha niliweke vizuri, mamlaka ya Mheshimiwa Rais kuteua hayawezi kuulizwa kwa namna hiyo kwa zile nafasi ambazo zinateuliwa kikatiba ama kisheria, Rais mamlaka yake hayaulizwi kwa sababu hata wale wanaompa ushauri hafungwi na huo ushauri yeye anaweza kufanya jambo ambalo ameruhusiwa kikatiba muda wowote. (Makofi)

Sasa hoja mahsusi ya hawa ndugu ambao wanateuliwa, hii si mara ya kwanza ikizungumzwa humu ndani. Sasa wacha niweke vizuri ili wanaochangia wengine waelewe mukhtadha wake.

Amesimama Mheshimiwa Mwijage hapa ameeleza kwa upande mmoja sababu maalum zinazoweza kumpelekea yule anayeteua na kwa mukhtadha huu Rais wetu kumteua mtu fulani kumpeleka sehemu fulani, anakuwa ana sababu na ameona mtu huyu ndiye anayefaa. Sasa kwa mukhtadha huo huwezi kusema kwa nini umempeleka huyu pale.

Lakini sasa, hoja ya Mheshimiwa Esther kwamba ukiwapeleka hawa wanajeshi wakaenda kuwa sehemu ya Kamati na ametaja mahsusi Kamati ya Siasa, lakini lazima unapozungumza Ukuu wa Mkoa usiuzungumze tu kwenye nafasi ndogo ya Kamati ya Siasa ya Mkoa ama Kamati ya Siasa ya Wilaya kwa Mkuu wa Wilaya, kwa sababu pia huyu ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama kwenye huo Mkoa. (Makofi)

Kwa hiyo, wanapopelekwa huko maeneo ni kwamba huyu mwenye mamlaka ya uteuzi ameona kuna sababu. Kwa hiyo, ukichukulia tu hilo eneo ambalo wanaenda kuwa Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya na ukasema pengine haipo sawasawa hoja ya Mheshimiwa Jenista inasimama kwamba huwezi kuuliza yule anayeteua kama anaweza kumteua nani kwenye nafasi ipi.(Makofi)

Lakini sasa wanaenda pia kwenye nafasi nyingine ambazo siyo za kijeshi, lakini wanaenda wanajeshi na umetolewa mfano hapa anaweza kuwa Katibu Mkuu wa eneo fulani, Maliasili, sijui Mambo ya Nje, kwa hiyo hutegemea lile ambalo huyu mwenye mamlaka ya uteuzi ameona huyo ambaye ameteuliwa akasaidie kwenye hilo eneo. (Makofi)

Sasa kwa sababu limezungumzwa humu ndani na watu wengine huwa hawaelewi sana zile Kamati za Siasa zinafanya nini na kazi ya Mkuu wa Wilaya akiingia kwenye Kamati ya Siasa ya Wilaya kazi yake ni nini na akiingia kwenye Kamati ya Mkoa kwa maana ya Mkuu wa Mkoa kazi yake ni nini? Hiki ni Chama ambacho ndicho chenye Ilani ambayo inatekelezwa nchini. (Makofi)

Kwa hiyo, anavyoitwa kule ni kwenda kuelezea utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwenye Mkoa wake au kwenye Wilaya yake. Sasa kwa sababu Wabunge wa CCM huwa hawalizungumzi hili kwa nini, kwa sababu wao ni sehemu ya hivyo vikao kwa hivyo wanaelewa majukumu ya huyu mtu ni yapi. (Makofi)

Kwa hiyo Waheshimiwa Wabunge na wananchi, wala wasiwe na wasiwasi kwa Mkuu wa Mkoa ama Mkuu wa Wilaya ambaye ni mwanajeshi kwenda kuhudhuria hivyo vikao kwa sababu wanachoenda kukifanya kule ni kile ambacho ana kazi hiyo kikatiba kwa sababu nchi yetu imeweka utawala wa kidemokrasia lakini tunaongozwa na vyama vya siasa. (Makofi)

Kwa hiyo, chama cha siasa kilichopo madarakani kile kinachotekelezwa cha kwake lazima akawaambie wenye chama chao utekelezaji unaendaje. Kwa hiyo kule kwenye Kamati ya Siasa na Kamati ya Siasa ya Mkoa na Wilaya mukhtadha ni huo na nadhani kwa maelezo hayo nimeeleza kwa kirefu nadhani tumeelewana vizuri kuhusu hizi teuzi, lakini pia namna unavyoweza kuizungumzia humu ndani uteuzi ambao Mheshimiwa Rais ameufanya kikatiba au kuna teuzi ambazo hata pengine zinaweza kufanywa na mamlaka nyingine ambazo zimeruhusiwa kufanya hivyo. Nadhani hili limeeleweka tayari. (Makofi)

Mheshimiwa Esther Matiko malizia mchango wako.

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, nilikuwa namalizia kwenye makazi ya ndugu zetu. Ni dhahiri yapo duni sana sana, kwa hiyo, tunaomba Serikali iboreshe makazi ya hawa ndugu zetu, kwa sababu tusiishie tu kuwaambia jeshi letu lipo imara, lakini wawezeshwe basi hata wakiishi wajue kabisa kweli nchi yangu inanijali kama vile ambavyo naitumikia nchi yangu. Ahsante sana. (Makofi)