Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

Hon. Agnesta Lambert Kaiza

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi hii ili nami kwa uchache niweze kuchangia katika Wizara hii muhimu. Mchango wangu wa leo utajikita katika ripoti ya CAG ukurasa Na. 223 na ukurasa Na. 226.

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu imekumbwa na ugonjwa wa hatari ambao umeua watu wengi duniani kote wakiwemo ndugu zetu, jamaa zetu na marafiki zetu. Kila nchi imeweka mkakati madhubuti wa kupambana na ugonjwa huu wa corona; na nchi yetu Tanzania pamoja na mikakati mingine ambayo iliweka, ilijikita zaidi kuhakikisha Watanzania tunajikinga kwa kutumia barakoa na siyo tu kwa kunawa mikono.

Mheshimiwa Naibu Spika, mnamo mwezi Mei, 2020 Serikali kupitia MSD iliagiza mtambo wa kutengeneza barakoa hapa nchini. Mtambo huu umegharimu dola za Kimarekani 270,314 sawa na shilingi milioni 600 plus. Mtambo huu according to CAG ulitarajiwa kuzalisha barakoa milioni nne kwa mwezi. Hata hivyo, management ilikaa na kukubaliana kwamba badala ya kuzalisha barakoa milioni nne kwa mwezi, basi izalishe barakoa 504,000 tu kwa mwezi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeyasema haya kwa mujibu wa CAG. Pamoja na kwamba management ilijipanga kuzalisha barakoa 504,000 malengo haya hayajatimia kabisa. Ukumbuke, nimesema kwamba uwezo wa mtambo huu ulipaswa kuzalisha barakoa milioni nne kwa mwezi. Mpaka sasa nimesimama mbele zako, mnamo mwezi Agosti mtambo huu umezalisha barakoa 76,500 tu. Mwezi Septemba mtambo huu umezalisha barakoa 244,000 tu which means hata yale malengo waliyojiwekea ya kuzalisha barakoa 504,000 yameshindikana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa CAG, anasema katika ukurasa 223, kwamba changamoto hii ya mashine hii kushindwa kuzalisha milioni nne kwa mwezi ilitokana na compressor iliyokuwepo kutokufanya kazi vizuri na hivyo basi, ikabidi iletwe compressor nyingine ili kuongeza nguvu na hatimaye angalau uzalishaji ufikie malengo yale ya management iliyokuwa imejiwekea ya 504,000. Mpaka hivi sasa, kwa mujibu wa CAG mtambo huu wa kuzalisha barakoa umefanya uzalishaji kwa asilimia nne tu ya uwezo wa mtambo huu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesema kwamba ilifungwa compressor nyingine ili iongeze nguvu kwamba sasa angalau uzalishaji uweze kuwa mkubwa. Cha kushangaza…

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

T A A R I F A

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Agnesta Lambert, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Musukuma.

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Nimemsikiliza mzungumzaji, anazungumza kuhusu suala la uzalishaji wa barakoa. Nilitaka kumpa tu taarifa kwamba kitu chochote kinachotengeneza vitu kibiashara, kinategemea na mahitaji yanayotakiwa. Sasa ukiangalia hata humu Bungeni, namwona dada yangu Mheshimiwa Halima peke yake ndio amevaa barakoa. Sasa hata tungezalisha hizo milioni nne, yeye mwenyewe mwongeaji, yuko empty ingekuwaje? (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Agnesta Lambert, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, siipokea taarifa hiyo, lakini nadhani alikuwa hanisikilizi vizuri. Nilisema mchango wangu utajikita katika ripoti ya CAG. Haya siyo maneno yangu mimi Agnesta Lambert, ni maneno na ripoti ya CAG. Kwa hiyo, taarifa hiyo ingekuwa ni vyema kama ungemtafuta CAG ukampatia ili aweze kukupatia majibu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa niendelee. Nimesema mtambo huu siyo tu kwamba umeshindwa kukidhi matakwa ya kuzalisha milioni nne kwa mwezi, imeshindwa hata kukidhi matakwa ya kuzalisha barakoa 504,000 which means hapa kuna shida. Kuna utata! Ni wazi Watanzania tumeuziwa mbuzi kwenye gunia.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Agnesta Lambert, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Getere.

T A A R I F A

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, nampa taarifa mzungumzaji kwamba suala la uzalishaji wa barakoa ni biashara inayoweza kufanywa, kwa sababu kuna demand na supply. Sasa demand ya biashara ya Tanzania ni kidogo sana, lakini pia tulisharuhusu badala ya Serikali kutengeneza barakoa, tutengeneze wenyewe. Kwa hiyo, yeye asihangaike na mambo ya CAG, atengeneze tu kwa njia yake. (Kicheko)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Agnesta Lambert, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza siipokei hiyo taarifa, lakini pili naomba niwe wazi, niko hapa kuwatetea Watanzania zaidi ya milioni 60. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo hili nimalize kwa kusema hivi, lazima ufanyike uchunguzi kabisa wa moja kwa moja ili kuangalia mambo makuu mawili. Kwanza, tuhakiki kama kweli mtambo huu ulinunuliwa kwa thamani hiyo ya dola za Kimarekani 270…

(Hapa kengele ya kwanza ililia)

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niendelee nimalize kwa kusema hivi, kwa mwaka mmoja mashine hii au mtambo huu ulipaswa kuzalisha barakoa milioni 48, lakini mpaka sasa hivi nimesimama mbele zako MSD wamezalisha barakoa 320,000 tu. It is a shame.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende moja kwa moja ukurasa 226 wa ripoti ya CAG. Katika mchango wangu nilipokuwa nachangia katika Wizara ya Ofisi ya Waziri Mkuu niliongelea moja kwa moja juu ya usugu wa Serikali kutokulipa madeni ya MSD, jambo ambalo limesababisha MSD siyo tu kwamba imeshindwa kuagiza madawa, lakini Watanzania wengi wanakufa na wanakosa huduma kwa sababu tu ya madeni ya Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo nimeweka tu kumbukumbu lakini hoja yangu ya msingi imejikita…

T A A R I F A

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. PASCHAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, hiyo itakuwa taarifa ya mwisho. Mheshimiwa Agnesta Lambert, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Patrobas Katambi.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. PASCHAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nakushukuru. Napenda kumpa taarifa msemaji, suala la malipo ya MSD lilitolewa ufafanuzi na Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, kwamba liko kwenye hatua ya uhakiki wa madeni na taarifa na kama tunakumbuka katika Bunge la wiki iliyopita taarifa hiyo ilielezwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, zaidi katika eneo la uzalishaji wa barakoa; uzalishaji wa barakoa unaendana na kusudio kwa maana ya mahitaji. Zingezalishwa barakoa unazozihitaji kwa kipindi hicho, kungekuwa na query tena ya CAG kwa utaratibu ule ule. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, napenda tu kumpa taarifa kwamba awe anachunguza zaidi katika kuangalia haya mambo kabla hajaleta hoja mezani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana. Mheshimiwa Agnesta Lambert, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kiti chako kilinde muda wangu, nafikiri umeona jinsi ambavyo Waheshimiwa Wabunge wame-interfere sana.

Mheshimwia Naibu Spika, naomba niende kwa point yangu ya pili. Hoja yangu ya pili ni kuhusiana na usugu wa Serikali uliokolea sasa kwa kutokupeleka bajeti iliyoidhinishwa na Bunge lako Tukufu kwenda MSD.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka wa fedha wa 2019/ 2020, Bunge lako hili Tukufu lilipitisha bajeti ya bilioni 200 kwenda MSD, lakini pesa hii haijaenda hata shilingi moja. Matokeo yake MSD wameshindwa kuagiza madawa pamoja na vifaa tiba venye thamani ya milioni 119, yote haya Serikali ni kwa sababu inashindwa kupeleka fedha bilioni 200 kwenye MSD kupambana kuhakikisha Watanzania wanakua na afya njema, lakini wanapata huduma bora…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Kengele ya pili imeshagonga Mheshimiwa, ahsante sana.

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nipe sekunde moja ili ni-finalize wamechukua muda wangu.

NAIBU SPIKA: Sekunde 30.

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Nimalizie kwa kusema kwamba kwa kipindi cha miaka mitano Bunge lako Tukufu limeidhinisha kiasi cha fedha za Kitanzania trilioni 1.04 kwenda MSD, lakini mpaka hivi sasa nimesimama mbele yako Serikali imepeleka bilioni 315 tu. This is the shame, hii ni asilimia 30 ya bajeti nzima ya MSD.