Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

Hon. Riziki Saidi Lulida

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

MHE. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nikushukuru. Nimshukuru pia Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, kwa kunijalia kupata afya njema nami kuwepo hapa na kuchangia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa vile leo ni mara yangu ya kwanza, nitoe pole kwa familia ya Hayati Dkt. John Joseph Magufuli na Watanzania wote, kwa kweli nimeguswa na msiba wake na mimi ni mmojawapo wa wateule kwa nafasi ambayo nimekuwepo hapa Bungeni. Nitaendelea na kuwaomba Watanzania tuendelee kumwombea dua kwa vile alifanya mengi mazuri ambayo sasa hivi tunayaona, ili Mwenyezi Mungu amlaze na ailaze roho yake pema peponi. Amina.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi karibuni Ujerumani na America wametoa pongezi kubwa kwa aliyepeleka research yake kule kuhusu suala la Corona, kwa kweli ile research yake dunia wameipongeza sana. Wanakuja kumpongeza sasa hivi Hayati ameshaondoka. Wakati ule anapambana walikuwa kama wanambeza kwa vile suala la Corona na mambo mengine ni biashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo nitaongelea suala la malaria. Mimi ni Mwenyekiti wa Kupambana na Malaria ndani ya Bunge. Kwa sasa hivi katika taarifa tulizokuwa nazo, kwa siku Watanzania 104 wanakufa kutokana na malaria. Ni gonjwa zito na kubwa na tishio kuliko hata Corona Virus. Kwa maana nyingine kwa mwezi Watanzania zaidi ya 3,000 wanakufa kwa ajili ya malaria. Sasa jiulize kwa nini sana wao wanatulazimisha tutumie hizi chanjo ya Corona wakati tunahangaika na kupambana na kutokomeza ugonjwa wa malaria. Zero malaria naanza na mimi, lakini kila Mtanzania nataka tuhakikishe tunapambana na tunatokomeza malaria. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, malaria kuna mikoa sita ambayo ina maambukizo makubwa ya malaria; kwanza, Kigoma, Lindi, Mtwara, Ruvuma, Geita na Kagera. Na tumeambiwa tena Mkoa wa Geita utakuwa wa kwanza katika Tanzania kwakuwa na maambukizo makubwa ya malaria kwa ajili ya machimbo yaliyokuwepo kule Geita. Inamaana wachimbaji wanachimba, lakini hawaangalii athari zake kwa vile mikataba ya EIA (Environemt Impact Assessment) haikufanyika, hivyo watabakia jamaa zangu wasukuma kuwa ni wagonjwa ambukizi wakubwa wa malaria na watapata vifo vingi kwa kupitia katika machimbo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jiulize kama sisi tunakufa Tanzania ni nchi ya kumi katika nchi kumi na moja duniani ambayo inamalaria, maambukizi ya malaria makubwa sana mojawapo ni Tanzania, katika zile nchi kumi. Lakini sisi leo tunalazimishwa kufanya vaccination ya Corona, lakini hawajataka kutupa ufumbuzi, je, tutatokomezaje janga kubwa ambalo ni tishio kuliko hata Corona. Hapa lazima utajua kabisa hapa kuna biashara, zinaenda na hizi biashara tuziangalie kwa makini sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeambiwa wanatangaza Tanzania tunapeleka dola milioni 45 kwa ajili ya kutokomeza malaria. Pesa zote zinazokuja za UKIMWI tunaziona katika Halmashauri na nyie Wabunge ni mashahidi hasa katika Local Government. Je, hizi hela za malaria zinakwenda wapi? Hizi hela zinakwenda kwa hao kutuletea dawa na vyandarua lakini hawana nia kabisa ya kutokomeza malaria kwa vile biashara zao ziendelee kufanyika ili na sisi tuwe wahanga wa vifo vya malaria. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumefungua kiwanda kikubwa Kibaha cha viuadudu wa malaria, lakini kwa vile wao wanafanyabiashara kile kiwanda kimeambiwa kuwa hakijakubaliwa na World Health Organization hivyo tumekaa na kiwanda ambacho ni kizuri nchi za wenzetu wanachukua dawa sisi tumeshindwa kutokomeza malaria wakati kiwanda kipo Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu, Mheshimiwa Waziri wewe ni pacha wangu, hakikisha halmashauri zote zinanunua dawa kwa kupitia, za kuua wadudu maambukizi kwa kupitia kiwanda cha Kibaha. Itakuwa ni dharau kubwa wanahela za ndani za kununua dawa hawanunui na hata wakinunua hawafanyi kazi hii ya kupulizia na kuhamasisha ili angalau tutokomeze hili janga la malaria. (Makofi)

MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Lulida kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Josephat Gwajima.

T A A R I F A

MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kumtaarifu tu Mheshimiwa Mbunge anaongea mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira. Tumetembelea hicho kiwanda cha hapo Kibaha ambacho kina utaalam wa ajabu, mzuri ambao haupo mahala popote Afrika Mashariki. Wacuba wametengeneza hicho kiwanda kwamba, wanatengeneza bacteria wanapowala hawa mbu, mbu wanakufa wote.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini cha kusikitisha tulifika kwenye kiwanda hicho wafanyakazi wa hapo hawajalipwa miezi ya kutosha, wafanyakazi wanazunguka zunguka, kiwanda ambacho kingeondoa malaria kuna watu wanapambana nacho kwasababu malaria ikiondoka maana yake dawa za kupulizia zimeharibika, prescription za malaria hazipo. Kwa hiyo, namjulisha mjumbe kwamba anapambana na wafanyabiashara wanaopata fedha kupitia mradi wa malaria. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Riziki Lulida unaipokea taarifa hiyo.

MHE. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli naipokea taarifa yake kwa vile yeye naye ni mzalendo kama mimi. Wazalendo kama Mr. Gwajima ni lazima tuwapongeze na nikubali maana yake kuna Wabunge wangetaka kutumika wakataka kukidharau lakini nimeona Mheshimiwa Gwajima ni champion na Mama Gwajima naye vilevile ni Champion kuhakikisha kuwa Tanzania bila malaria inawezekana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Bima ya Afya, kama walivyozungumza Wabunge wenzangu ninamasikitiko makubwa sana na Bima ya Afya. Bima ya Afya haimlengi mtu na ni hii wazee zaidi ya miaka sitini, wazee wa miaka sitini ili atibiwe mahali popote inabidi atoe 936, tukiwemo humu Wabunge, Mbunge haruhusiwi kumtibu mzazi wake inabidi atumie mwenyewe kumtibu mzazi wake, sheria hii inatoka wapi? Na kama ipo naomba iletwe Bungeni tuibadilishe hii kanuni wazazi wetu nao wafaidike na matibabu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, unakuta mzee anaumwa mimi nitoe laki tisa nimtibu mzee wangu wakati bima yangu mimi ni bima ambayo ni ya VIP. Lakini vilevile la pili, nataka Mama Gwajima unisikilize mara mbili mbili na hoja hii naileta. Hospitali ya Aghakan…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Lulida ngoja kwanza.

MHE. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Naibu Spika, haya.

NAIBU SPIKA: kwa sababu kina Gwajima wapo wengi sasa ukimwita Mama Gwajima hapa hatuelewi unamwita mama wa Askofu ama Mheshimiwa Waziri hapa. Kwa hiyo yeye mwite Mheshimiwa ili tutofautishe na kina Mama Gwajima.

MHE. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Naibu Spika, haya, Mheshimiwa Waziri, Waziri wa Afya, nataka nimwambie, Bima ya Afya katika hospitali kubwa ya Aghakan na Regency Hospital haiwataki wajawazito. Lakini ukichukulia malaria waathirika wa kwanza ni wajawazito na wanapeleka bima kule wanasema sisi hatupokei bima za afya za wajawazito. Je, ni maana moja wanawadharau wanawake na kama wanadharau wanawake, wanawake hatukubaliani nalo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi wanawake ndiyo tunazaa Watoto, lakini leo unaambiwa pale hutakiwi kupewa nafasi ya kwenda kutibiwa kwa vile nini, utakuwa na gharama ya kwenda kupimwa pimwa mpaka kujifungua. Je, hii huoni kama inawakandamiza wanawake? na kulikuwa na haja gani ya kuwapa ruzuku mataasisi haya, wanaleta madawa na kila kitu wanapewa faida ya ruzuku lakini wanawakataa wanawake, tumeungana na wanawake Wenzangu wabunge wanataka uje utupe jibu kuhusu suala la Aghakan na Regency na vilevile waje watufanyie semina ya kututaarifu je, hizo hoja ni kweli na kama si kweli waje watuambie katika semina maalum hapa Bungeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, Bima ya Afya ambayo tunakuwa nayo sasa hivi, ukienda Aghakan kama Mbunge tunalipa bima kubwa sana lakini tunakwenda kulazwa na watu wa kawaida wanaotoa shilingi 70 na kila kitu. Wanasema sisi hatuwezi kuwapa bima ya VIP lakini hii yote ni kutunyanyapaa na kutuweka katika mazingira magumu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ningeomba ukae na hizi taasisi ambazo zinachukua hela za walipa kodi watanzania na iwatendee haki watanzania kwa kuwapa haki sawa kwa wote. Wasijione wao wamekaa kule wanatoa gharama kubwa na kuwaacha wagonjwa wengine ambao wanahitaji bima za afya zao wanazitenga kutokana na wanavyotaka wao. Kama si hivyo, pelekeni Bima ya Afya Muhimbili, boresheni Muhimbili, tutakimbilia katika mahospitali yetu ambayo ni ya walala hoi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitazungumzia changamoto za walemavu, walemavu ndiyo kundi maalum ambalo linahitaji msaada mkubwa sana katika tiba. Na katika tiba hizi hawa walemavu mpaka sasa hivi wanahangaika hawana Bima za Afya. Na kama hawana Bima za Afya hawa walemavu wengi wananyanyasika tu hawana mahali pa kukaa, hawana mahali pa kuishi. Lakini je, Bima ya Afya inasema nini kuwasaidia hawa kundi maalum ambao ni walemavu. Hatuna ma-desk ambayo yanasaidia walemavu hata katika mahospitali, leo anakwenda mlemavu ambaye ni kiziwi anataka kujifungua au ana matatizo lakini akienda pale hapati nafasi ya kusikilizwa, wanamchukulia kama mtu ambaye hana thamani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ningeomba hakikisha kuwa katika kila eneo la kituo cha afya, polisi ni lazima tuwe na desk maalum kwa ajili ya kusaidia kundi maalum la walemavu. Walemavu wanahitaji msaada wa kupata tiba kama watu wengine, walemavu wanahitaji kusaidiwa kama wengine, leo zinagawiwa chandarua Tanzania nzima lakini haimgusi mlemavu, kwa mara moja…

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa kengele ya pili imeshagonga.

MHE. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)