Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

Hon. Hawa Mchafu Chakoma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Tutakubaliana wote hapa kwamba afya ndiyo msingi wa maisha ya binadamu licha ya kwamba kumekuwa na ongezeko la magonjwa yanayoambukiza na yasiyoambukiza ambayo yanasababisha vifo vya wapendwa wetu. Sekta ya afya ndiyo mahususi kutoa huduma kwa jamii, lakini imekuwa na changamoto kadha wa kadha zikiwemo upungufu wa watumishi na vifaa tiba pamoja na uhaba wa dawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mkoa wa Pwani tuna uhaba wa watumishi takribani asilimia 52, watumishi wa sekta hii ya afya tulionao kwa sasa ni asilimia 48 tu ambayo kimsingi ni ndogo, hawatoshi kutoa huduma iliyokuwa bora.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mkoa wetu wa Pwani halmashauri inayoongoza kwa uhaba wa watumishi wa sekta ya afya ni Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji yenye upungufu wa watumishi wa sekta ya afya takribani asilimia 75, ikifuatwa na Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti yenye upungufu wa watumishi wa afya kwa asilimia 71 pamoja na Halmashauri ya Mafia ambayo ina watumishi wa afya asilimia 78 tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana Mheshimiwa Waziri aziangalie kwa macho matatu halmashauri hizi tatu, tuone namna bora ya kuwaongezea watumishi hawa wa sekta ya afya, hususan Halmashauri ya Wilaya ya Mafia ambayo kimsingi ni kisiwa, watumishi wakipelekwa kule huwa hawakai.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo naomba kuishauri Serikali tuangalie tuje na mpango kabambe wa kuhakikisha tunaandaa motisha. Tutoe motisha ya makusudi kwa hawa watumishi ambao wanafanya kazi katika mazingira magumu; maeneo ya visiwa, maeneo ya Delta na maeneo ya kule ndani ndani (remote/interior). Serikali ikitoa motisha kwa watumishi wetu hawa tutawafanya wavutiwe kubaki katika hayo maeneo, lakini sambamba na hilo, kutoa huduma iliyokuwa bora.

Mheshimiwa Naibu Spika, haikubaliki watumishi wa sekta ya afya Kinondoni na Ilala na wale watumishi wa sekta ya Afya kule Jibondo, Mafia ama wale wanaotoka kule Delta, Kibiti, wote kulipa sawasawa. Hiyo siyo sawasawa. Tena tunaambiwa kwa hawa watumishi waliokuwa Kinondoni na Ilala wenyewe wana motisha ya overtime kwa kuwa wanaona wagonjwa wengi, lakini tumewafikiria hao wanaotoka humo pembezoni. Usafiri mpaka kufika huku mjini kupata zile huduma za kijamii wanapanda kivuko, wanashuka, wanapanda bodaboda wanashuka, wanapanda magari wanashuka na bado wanatembea umbali mrefu. Mishahara yao yote inaishia kwenye nauli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo Serikali kama ambavyo busara na taratibu waliotumia kuwaongeza watumishi wa mijini kwa kuwa wanaona wagonjwa wengi, busara hiyo hiyo itumike kwa watumishi ambao wanatoka kwenye visiwa, delta na remote areas. Kwa hiyo naomba ushauri huo Serikali iuchukue na iufanyie kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Bagamoyo, Halmashauri ya Chalinze; tunaishukuru sana Serikali mmetupatia gari la wagonjwa (ambulance), lakini TANROADS ikisimamiwa na Wizara ya Afya wanao mradi wa kujenga huduma za majengo ya dharura katika barabara kuu. Kituo cha Afya Chalinze ni miongoni mwa vituo vilivyokuwa barabara kuu lakini pia ni miongoni mwa vituo ambavyo vimepatiwa mradi huu. Sasa naomba Mheshimiwa Waziri wakati anakuja ku-wind up atuambie mradi huu umeishia wapi? Unaonekana kusuasua, hatujui status yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, huu mradi ni muhimu sana kwa sababu hii leo ukipata ajali katika maeneo ya Chalinze pale Kibaha ina maana kupata huduma za dharura wewe mpaka ukimbizwe Mloganzila ama Muhimbili. Kama tungekuwa na huduma za dharura ama hapa Chalinze ama pale kwenye Hospitali ya Mkoa Tumbi, ina maana tungeweza kuokoa maisha ya Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, bado tuna changamoto ya foleni sisi, maana foleni ile tuliyoi-clear pale Ubungo ile barabara nane yote inatapikia Kibaha. Kwa maana hiyo tunaomba sana Serikali waje na majibu, watujibu, maana Wanapwani na Watanzania kwa ujumla ambao wanaitumia ile barabara kuu tunataka kujua mradi wa ujenzi wa majengo ya huduma ya dharura umekwamia wapi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri, alifanya ziara yake katika Hospitali ya Mkoa pale Tumbi; majengo yalishaanza kujengwa, yamechakaa na kuchakaa. Kwa hiyo nitaomba atuambie kwamba ule mradi gharama zake ni kiasi gani na wana mpango gani na mradi huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu huu mradi utatusaidia Wabunge tunaoishi Mkoa wa Pwani, Wabunge wa Dar es Salaam, Wabunge wa Lindi, Wabunge wa Mtwara, Wabunge wa Ruvuma pamoja na Wabunge kutoka Zanzibar. Sisi ndio wasafiri wakuu kuja Dodoma kwenye vikao na kurudi majimboni. Mungu aepushie mbali, lakini once tukipata ajali kusema tukimbizwe mpaka Mloganzila ama Muhimbili, ama hakika mradi huu utakwenda kuokoa maisha ya Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, imezungumzwa na Dkt. Thea hapa kuhusiana na masuala ya ukeketaji, lakini pia naomba niseme jambo moja; wanaume wa nchi hii wanapenda sana kujadili mpira na wanapenda sana kujadili siasa kuliko ambavyo wangeweza kujadili masuala ya kuhamasishwa kwenda kupima Virusi Vya UKIMWI. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, yaani ukiwakuta kwenye mijadala ya mpira, mijadala ya ukewenza pamoja na mijadala ya masuala mazima haya ya siasa; wangetumia effort hiyo kuhamasishana kwenda kupima Virusi Vya UKIMWI leo hii tungesaidia akinamama. Maana wanaume hawa kwenda kupima UKIMWI wanasubiri mwanamke ashike ujauzito akapime ndiyo wao wapate majibu yao na wakati kila mtu ana immunity yake, kila mtu ana kinga zake. Kwa hiyo nataka niwaombe sana kaka zangu, baba zangu na marafiki zangu, ile nguvu wanayotumia kujadili Simba na Yanga, ile nguvu wanayotumia kujadili siasa na ile nguvu wanayotumia kujadili ukewenza ihamisheni ipelekeni kwenye masuala ya kupima UKIMWI na Virusi Vya UKIMWI. (Makofi/ Kicheko)

MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Dkt. Thea kule amezungumza kuhusiana…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Hawa Mchafu, kuna taarifa, sijajua ni Mbunge gani aliomba kutoa taarifa.

MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Sawa, Mheshimiwa Twaha Mpembenwe.

T A A R I F A

MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpe taarifa tu mzungumzaji kwamba asilimia 99 ya wanaume ambao ni Wabunge katika Bunge hili la Kumi na Mbili, taarifa zilizopo ni kwamba wamepima UKIMWI. Ahsante. (Kicheko)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Twaha, naona hata wenyewe wanakushangaa maana hawajapima na kama wamepima hawajachukua majibu. (Kicheko)

Mheshimiwa Hawa Mchafu.

MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru; siipokei taarifa ya Mheshimiwa Twaha kwa sababu kama anasema kweli, hicho anachokisema wakihamishe sasa kwenye majimbo yao wakawatangazie na wananchi wao ili waweze kufanya hivyo hivyo, kwamba tukipata asilimia 90 ya wananchi wanaume kwenye jimbo lake wamepima, sina shaka Tanzania tutakuwa tuko vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, bado niko hapohapo kwa wanaume wa nchi hii, kwamba tumeambiwa madhara ya ukeketaji, lakini wanaume hawa ndio watu wa kutusaidia sisi. Wakitoka huko nje wakasema aliyekeketwa na ambaye hakukeketwa nani yuko vizuri, lakini wanaume hawa wakisema kwamba hawa waliokeketwa hawatawaoa, sina shaka itakuwa ni njia, itakuwa ni mwarobaini wa kusaidia kupunguza ukeketaji. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, natoka sasa hapo kwa wanaume, mchango wangu mwingine ni kuhusu suala zima alilozungumza Mheshimiwa Askofu Gwajima kuhusiana na chanjo ya Corona na madhara yake. Nikiwa kama Mjumbe wa Kamati ya Masuala ya UKIMWI tulipata fursa ya kutembelewa na watu wenye hii dawa inaitwa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na naunga mkono hoja. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Dakika moja, hebu elezea dawa gani. (Makofi)

MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Nilikuwa nataka kuizungumzia hii dawa Phyt Exponent. Imeonekana kusaidia watu wengi sana kwenye masuala ya Corona. Kwa bahati nzuri Mkemia Mkuu ameicheki na amethibitisha kwamba inafaa kuwa ni medicine, lakini inatambulika kama supplementary na inauzwa ghali, shilingi 150,000. Ili kuwasaidia Watanzania waweze kuipata hii dawa, ikianza kufahamika kama ni medicine, madaktari wakiweza kui-prescribe ina maana itauzwa madukani kwa bei rahisi, tutaweza kusaidia watu wetu na janga zima la Corona. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo nikushukuru sana kwa kunipa nafasi. Naunga mkono hoja. (Makofi)