Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Hon. Dr. Faustine Engelbert Ndugulile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigamboni

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, napenda kuwashukuru Wabunge wote pamoja na Kamati kwa maoni mazuri. Nami niwahakikishieni ma-crown yote tumeyachukua na tutayazingatia katika utekelezaji wa majukumu yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwashukuru sana wachangiaji wote; tumepokea michango 28 ya Wabunge ambao waliichangia hapa ndani Bungeni, 40 michango kupitia kwenye kamati lakini tumepata michango nane kwa njia ya maandishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kusema kwamba Wizara yetu sisi ni Wizara mtambuka. Ni Wizara wezeshi na Wizara ambayo inasaidia sekta nyingine zote na kuwezesha sekta nyingine zote. Kwa nini kumeanzishwa Wizara hii, nataka nitumie fursa hii kutoa elimu kidogo kwa Wabunge, kwamba Wizara hii imeanzishwa mahsusi kuangalia jinsi gani sisi kama nchi wakati dunia inaongelea mapinduzi ya nne ya viwanda forth industry revolution ambayo msingi wake mkubwa ni TEHAMA, basi na sisi kama nchi tuweze kujiandaa katika msingi huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, dunia inaongelea masuala ya digital economy na ukiangalia sasa hivi, ukiangazia miaka 10 iliyopita, makampuni makubwa duniani yalikuwa katika manufacturing, lakini sasa hivi ukiangalia makampuni makubwa yapo katika sekta ya TEHAMA. Kwa hiyo, sisi kama nchi ni lazima tuangalie na tuangazie huko.


Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kujibu swali ambalo ameniuliza Mheshimiwa Neema Lugangila ni kwamba ndiyo tupo katika maandalizi ya sasa hivi ya kuandika digital economy blue prints ya Tanzania. Kazi hiyo tumeshaanza hatua za awali na tunatarajia andiko hilo litaweza kuanza hivi karibuni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo tunataka kuangazia e-commerce na Wabunge wamesema, element za e-commerce tumeanza nazo nchini. Sasa hivi ukiangalia wafanyabiashara wanjanja ama vijana hawatumii sasa na wala hawaendi pale Kariakoo kukodisha fremu, mtu anaagiza mzigo wake anaweka nyumbani, anapiga picha anaweka kwenye mitandao ya jamii. Wewe ukitamani, unaingia katika mtandao ya jamii, unachagua pale, mnalipana kwa miamala ya simu, anamtuma boda boda anakuletea nyumbani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pale hamna kodi ya jengo, hakuna leseni za TRA, wala leseni za biashara ni lazima na sisi tuwezeshe ili kuweka mifumo mizuri kuhakikisha kwamba e- commerce hata wewe sasa hivi unaweza ukaagiza mzigo nchi yoyote ya nje na mzigo wako ukaweza kukufikia. Huo utaratibu ambao tunakwenda nao wa anuani za makazi na postikodi, tunataka mzigo ukufikie wewe nyumbani pale pale ulipo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo tunaangazia sasa hivi kuhakikisha kwamba Serikali inamfuata mwananchi mkononi badala ya mwananchi kwenda kupanga foleni katika Ofisi za Serikali, tunataka ku-digitize service za Serikali ili mwananchi aweze kupata kiganjani, kodi
za ardhi, masuala haya ya umeme na huduma nyingine za Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaangazia vilevile kuhakikisha kwamba huduma za jamii, hawa Walimu wachache tuliokuwa nao nchini hao hao tuweze kuwatumia waweze kutoa huduma za elimu katika maeneo mengine ambayo wana-shortage ya Walimu. Tuangazie kwamba badala ya Waziri wa Elimu kuhangaika kuchapisha vitabu, tunaweza tukatengeneza DG e-books na kuweza kuzisambaza na mwanafunzi akawa na kitabu chake kwa njia ya mtandao. Tukaachana na hizi library ambazo zimejazana vitabu vikuu vikuu, hizo space zikageuzwa kuwa madarasa badala yake mtoto akawa anasoma na akapata kitabu pale pale alipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaangazia kwamba Madaktari wetu wachache tuliokuwa nao waweze kutoa huduma kwa maeneo mengine ya pembezoni ambapo hakuna Madaktari Bingwa. Hilo tumelianza katika upande wa teleradiology ambapo sasa hivi tunafanya installation ya digital x-ray, Madaktari wetu Bingwa ambao wanaweza wakasoma x-ray, MRI na vitu vingine, picha inaweza ikapigwa Tandahimba ikatumwa Dar es Salaam pale MOI ikasomwa na majibu ndani ya dakika 15 yakarudishiwa kule kule alipo mwananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka kuangazia katika Sekta ya Kilimo, mkulima kule kule alipo akiwa na simu janja aweze kupata ushauri kuhusiana na masuala ya mbegu, masuala ya wadudu waharibifu, kuhusiana na mbolea na kuhusiana na masoko kule kule katika eneo ambalo yeye yupo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka kuangazia mchango wa sekta hii katika uchumi na pato la Taifa letu. Watalaam wanasema tukiwekeza katika Sekta ya TEHAMA by 10 percent inaweza kusaidia kukuza Pato la Taifa kwa zaidi ya asilimia 1.5. Sasa nini tunachotaka kukiangazia, katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi imetuelekeza sisi, kuhakikisha kwamba tunakuza Mkongo wa Taifa kutoka asilimia 45 tuliokuwepo sasa hivi hadi kufikia asilimia 80 na kuongeza mahitaji ya matumizi ya internet kutoka asilimia 43 mpaka asilimia 80 ambayo imeelezwa pale katika Ilani ya Uchaguzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua gani ambazo tunazichukua sasa hivi? Mheshimiwa Naibu Waziri ametoka kusema, sasa hivi tunavyoongea Mkongo wa Taifa tunakwenda kufikia kilometa 8,319. Katika mwaka huu wa fedha bajeti kama Wabunge watatupitishia tena hapa tutakwenda kujenga kilometa 1,880, tumeshafika katika Makao Makuu yote ya Mikoa, bajeti wakitupitishia Wabunge tunakwenda kufikisha katika Makao Makuu ya Wilaya zote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo letu tukifika 2025 tunataka tufikie Mkongo kilometa 15,000. Sasa hivi tumeweza kufikia nchi zote za Jirani, sasa hivi tunafanya upembuzi yakinifu tuweze kuunganisha na DRC. Changamoto ambayo tumeipata sasa hivi kwa sababu ya kina cha Ziwa la Tanganyika ndiyo tunajaribu kuangalia teknolojia gani ambayo tunaweza kutumia ili kuhakikisha kwamba mkongo na sisi tunaweza tukaufikisha kule DRC. Lengo letu na sisi tuwe ni hub ya TEHAMA katika Afrika Mashariki na tuweze kuwafikia wenzetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi ninavyoongea na nikimaliza Bunge naenda Mtambaswala sasa hivi tunafanya kwenye connectivity na Msumbiji, ili kuhakikisha kwamba mawasiliano yetu na sisi tunawafikishia kule Msumbiji. Sasa na hatua gani nyingine ambazo tunaendelea kuzichukua ili sasa tuweze kuwa na usimamizi mkongo ambao ndiyo highway, ndiyo njia kuu ya mawasiliano na ndiyo moja ya njia kuu ya uchumi kama ilivyo reli, barabara pamoja na bandari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkongo wa Taifa nao ni moja ya njia kuu, tutakapokuwa tunaongelea huko masuala ya barabara na tukumbuke vile vile suala la Mkongo wa Taifa ambao ndiyo njia kuu ya mawasiliano ndani ya nchi yetu. Mawasiliano sasa hivi si anasa ni haki ya msingi ya kila Mtanzania. Tunakwenda kuboresha usimamizi wa mkongo na tunakwenda kuanzisha chombo ambacho kazi yake kikiamka asubuhi ni kusimamia, kuendesha na kuendeleza suala hili la mkongo, tumeshaanza mchakato huo na tunaamini ifikikapo Julai Mosi, jambo hili tutakwenda kufanikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo suala la kuwekeza katika miundombinu halitoshi peke yake, tunataka sasa tuwekeze katika digital literacy. Tukiangalia Watanzania wengi bado hawana uelewa mzuri wa matumizi ya internet, hata sisi Wabunge tunatumia chini ya asilimia 50 ya uwezo wa simu zetu. Tunakata tu-invest kuhakikisha kwamba tunajenga digital literacy, elimu ya kutosha katika masuala ya haya ya TEHAMA, lakini sambamba na hilo kuhakikisha kwamba tunakuwa na matumizi sahihi na mazuri ya internet.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yote haya hayatakuwa na tija kama uwezo wa Watanzania kuweza kumudu kununua simu janja na vifaa mpakato. Sasa hivi tunataka kujielekeza kuhakikisha kwamba vifaa mpakato vinapatikana kwa gharama nafuu. Moja ya mkakati ambao tunao ni kuhakikisha kwamba tunakuwa na viwanda vya ku-assemble ama kujenga viwanda ambavyo vitatengeneza simu janja hapa ndani ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo tunataka kuongeza wigo wa internet na tumewasikia Waheshimiwa Wabunge, ni kweli mwanzoni tulipokuwa tunaanza mikakati yetu ilikuwa lengo ni kuwafikishia mawasiliano na ndiyo maana mitandao yetu mingi ilikuwa 2G, lakini tumekubaliana sasa minara yote tunayoenda kujenga sasa hivi itakuwa ni 3G kwenda juu, ili kuwezesha sasa Watanzania walio wengi waweze kupata huduma za internet. Hakuna mtu ambaye anayesema kwamba vijijini eti nao hawahitaji internets, tunataka hata wale wa vijijini waweze kutumia internet kwa shughuli mbalimbali za kiuchumi na kujiletea maendeleo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakwenda ku-harmonize system, sasa hivi kama unavyofahamu miaka mitano iliyopita mifumo yote nchini ilikuwa ya kutoka nje ya nchi, lakini sasa hivi tumepiga hatua mifumo mingi ya TEHAMA ndani ya nchi sasa hivi asilimia 80 tunaitengeneza hapa hapa nchini. Changamoto ni kama hizi ambazo zimejitokeza kwa hii katika mifumo ya LUKU, bado kuna changamoto ya mifumo kuingiliana, bado kuweka mifumo ya backup na bado kuna mianya kidogo ambayo inaweza ikawa ni hatarishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya yote Wizara yetu itaendelea kuyasimamia na kuhakikisha kwamba tunaweka mifumo mizuri na sahihi. Pia tutahakikisha kwamba hii mifumo ambayo imetengenezwa na vijana wetu wazalendo inakuwa ni robust na inaweza ikasimama na tunakuwa na mifumo mingine ya backup ambayo inaweza ikasaidia, pakitokea tatizo basi kunakuwa na njia mbadala ya kuweza kupata huduma zile husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo tunakwenda kufanya maboresho ya sheria. Wizara yangu na sekta yangu ni sekta ambayo inakwenda kwa kasi sana. Tumekuwa na sheria ambazo zimekuwa ni za muda mrefu sana. Niombe kusema na nasimama mbele ya Bunge hili kusema, sitaki kukumbukwa kama Waziri ambaye alikuwa ni Polisi wa sekta, nataka nikumbukwe kwamba ni Waziri ambaye alikwenda kuleta mapinduzi makubwa katika Sekta ya TEHAMA. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nirudie, sitaki kukumbukwa kwamba Waziri ambaye alienda kuminya na kuwa Polisi wa sekta, nataka nikumbukwe kwamba ni Waziri aliyeweza kuweka mazingira wezeshi ya Sekta ya TEHAMA kukua ndani ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo Wizara tunakwenda kufanya mabadiliko makubwa sana ya kimuundo ya taasisi zangu, lakini muundo wa kisheria, ikiwa ni pamoja na hawa vijana wetu ambao wanajiajiri kupitia TEHAMA. Kijana ni MC anafanya shughuli zake za harusi, anarusha picha zake kwenye You Tube ili watu wengine mumwone umahiri wake wa kazi halafu sisi tunataka kumtoza kodi, hili tunataka tuondokane nalo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vijana wetu hawa wasanii, wanatengeneza nyimbo zao, sasa hivi hawauzi cassette wala hawauzi flash, wanaziweka huko kwenye mitandao na huko ndipo wanapata mapato yao sisi tunaenda kuwaminya tena kule. Tunataka kwenda kufanya maboresho makubwa ambayo yatatengeneza mazingira wezeshi kuhakikisha hizi platform sisi tusiwe ni kizuizi bali tuwe ni watu ambao wanakwenda kuhakikisha kwamba hawa vijana wanaweza kujiajiri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo tutakwenda kuliangalia suala la visimbuzi nalo nimeshatoa maelekezo tarehe 21 watoa huduma, watoa huduma sijui wa visimbuzi wote, watu wa television wote tarehe 21 nimewaambia wakae, wakae kama wadau wakubaliane yale makubaliano sisi Serikali tutayachukua na tutayabariki, tunataka tufanye mapinduzi makubwa hata katika hii tasnia ya wenzetu ya television.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo tunahitaji tuwe na mabadiliko ya fikra na sisi kama Wabunge tunahitaji tufikiri upya sasa hivi katika sekta hii TEHAMA, Tanzania tupo nyuma sana, wenzetu Kenya, Rwanda, Ghana, Nigeria wapo mbali, kuna vitu vinaitwa startup sasa hivi. Vijana wa sasa hivi hawatengenezi makampuni ya wajukuu wao kuja kurithi, wanatengeneza makampuni ambayo lile wazo lake likikubalika likaingia katika soko anauza, anaenda kuanzisha kampuni mpya. Wale vijana hawana hela wana mawazo na wazo lake lile ndiyo hela. Ni lazima tuwatengenezee mazingira wezeshi hawa vijana yao ili kazi ziweze kukua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna vijana wa software development, nawafahamu wanafanya kazi kubwa Israel, wanafanyia kazi Uingereza, ni Watanzania, lakini sisi hatuwatambui na wala hatuwatumii. Nimeongea na vijana baada ya Bunge hili, naenda kukutana na Tanzania Startup
Association, kukaa na kuangalia mahitaji yao na pale tutakapohitaji tutawaleta Waheshimiwa Wabunge mabadiliko ya sheria ili kutengeneza mazingira wezeshi kwa hawa Startups. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nimenong’ona na Waziri mwenzangu wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, wasanii Mheshimiwa Mwinjuma tumewasikia tutakuja tukae tuongee na nyinyi tuangalie challenge zenu, tuangalie hayo masuala ya aggregation na tuangalie jinsi gani tunaweza kufanya ili sasa tupige hatua kwenda mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la TTCL, ni kampuni yetu na katika Ilani ya uchaguzi imeelezwa kwamba, tunahitaji tuiboreshe kimenejimenti na kiuwezeshaji ili iwe ni kampuni yetu ya kimikakati, ni lazima na sisi kama Serikali tuwe na kampuni yetu ya kimkakati ya mawasiliano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na hili sisi kama Wizara na tukumbuke kwamba Waheshimiwa Wabunge sasa hivi sisi Wizara yetu ina miezi mitano tu, lakini hili na sisi tumelichukulia kwa uzito ambao unastahili. Tumeshakaa na wenzetu wa TTCL wameandika andiko lao la mahitaji yao na tumeshalipokea na tumeshalipitia na tutashirikiana na wenzetu wa Wizara ya Fedha, ili kuangalia huo mkakati wa kibiashara ambao wanataka kuja nao jinsi gani sisi kama Serikali tutakwenda kuwa-support. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tumeanza kufanya mapitio ya sheria ili kuhakikisha sasa na hili shirika letu ambalo linajiendesha kibiashara kuna sheria nyingi ambazo zinatukwaza. Kwa hiyo, mambo hayo mengine kwa mfano shirika letu sasa hivi haliruhusiwi kununua minara ambayo imetumika. Kwa hiyo, nayo tunataka kwenda kufanya mabadiliko ya sheria za manunuzi, ili tuwaruhusu kuweza kufanya manunuzi ya minara ambayo imetumika ama vitu vingine na kurahisisha utoaji huduma zao kama wanavyoweza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niseme kwamba tu kuna maboresho makubwa sana tunakwenda kuyafanya katika nyanja hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nigusie suala la digital taxes na hili nilishawahi kulisema lakini nadhani ilitafsiriwa vibaya, lengo letu sio sisi kuja kuweka kodi kwenye Whatsaps, Instagram na twitter huko siko. Lengo letu wale wakubwa sisi tunatumia mitandao hii bure, wanaotengeneza ni wale wakubwa ambao wanapata fedha nyingi za matangazo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo letu ni sisi tuwafikie wale sio mlaji huyu wa mwisho ambaye anakuja anatumia Instagram, Twitter na Facebook. Kwa hiyo, sisi tunajiangalia jinsi gani ya ku-analyze potential ya digital taxes kule badala ya kumbana mtumiaji huyu mmoja mmoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo hili nilitaka nalo niliseme, lakini sambamba na hilo tunakwenda kufanya maboresho ya sheria ya kulinda faragha za watu. Tuna data nyingi tunazi-generates unapotumia mitandao hii hii unapokwenda sehemu mbalimbali, kuna taarifa nyingi sana za kwako ziko pale zinaeleaelea. Kwa hiyo, tunakwenda kutengeneza sheria mpya ya data privacy na data protection lengo sio kuminya uhuru wa watu, lengo ni kukulinda wewe taarifa zako ambazo zinauzwa huko duniani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sambamba na hilo tutakwenda kuwekeza katika innovation hub natamani kuona miaka mitano ijayo Tanzania na sisi tunakuwa seal convert vijana wabunifu, sectoral developers, masuala ya cyber security, internet of things, block chain technology, artificial intelligence, tunajenga capacity ndani ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kusema tunatambua jambo hili la uhalifu wa mitandao na usajili wa online tunakwenda kuboresha mifumo na hiyo tarehe 26, tutakaa na Mawaziri wenzangu tuangalie njia bora zaidi ya kuangalia jinsi gani tunaweza kubana katika usajili huu wa line za simu. Ikiwa ni pamoja tunaweza tukaja na zoezi tena jipya la uhakiki wa watu wote ambao wamejisajili kwa njia ya biometric, ili kuhakikisha kwamba ni watu ambao wana kadi za simu wote wamesajiliwa na tunaweza kuweka mifumo ya kuweza kuwabaini. Na teknolojia tunayo ya kuangalia jinsi gani na kuweza kuzi-block hizo simu ambazo zinaweza kuwa zinatumika kwa njia ya kiuhalifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nimejielekeza zaidi katika kutoa elimu zaidi kuliko kuwaadhibu kwasababu, nimeona kwamba watu wengi hatujui sheria, watu wengi hatujui haki zetu, watu wengi hatujui matumizi sahihi ya mitandao. Kwa hiyo, na mimi nataka kama Waziri kujielekeza katika maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa michango yenu mizuri niwahakikishieni yote haya ambayo mnayasema tunaenda kuyafanyia kazi na kuweka mipango mikakati ya kuhakikisha kwamba tunakuwa na Tanzania ya TEHAMA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naomba kutoa hoja. (Makofi)

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naafiki.