Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Hon. Hawa Subira Mwaifunga

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia hoja ya Wizara hii ya Mawasiliano. Kwanza nikupongeze kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Bunge na leo umekalia kiti hicho. Naomba Mwenyezi Mungu akuongoze uendelee kuwa na hekima kama ilivyokuwa hapo awali tuendelee kwenda vizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na malalamiko makubwa sana ya masuala ya ma-bundle. Wananchi wengi sana wamekuwa wakilalamikia wizi mkubwa unaofanywa katika ma-bundle. Unapoweka bundle unapewa expire date, unaambiwa kwamba hii utatumia kwa mwezi mmoja, utatumia kwa wiki moja, utatumia kwa siku moja, lakini unaweza usitumie kwa mwezi mmoja, lakini inapofika ule wakati wanakufyeka inabidi uweke fedha nyingine sasa fedha hizi zinakwenda wapi? Tungeomba sana Wizara ya Mawasiliano waangalie jambo hili, limekuwa likipigiwa kelele sana na wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, walichofanya wamerudisha vifurushi vile ambavyo gharama ambazo zilikuwa hapo zamani. lakini, bado kuna hitaji kubwa sana la wananchi kutumia vifurushi hivi, lakini gharama hizi zinaonekana ni kubwa hasa kwa wananchi wa maeneo ya vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Waziri anawasilisha hapa amezungumzia kuhusiana na masuala mazima ya kesi za wahalifu wa mitandaoni. Mheshimiwa Waziri hajatuambia mpaka sasa, ni kesi ngapi mpaka sasa zimeshatolewa maamuzi. Kwanza zipo ngapi, lakini ni ngapi mpaka sasa zimeshatolewa maamuzi. Pia ni adhabu gani zinazochukuliwa kwa watu hawa wanaohusishwa na uhalifu wa mitandaoni. Labda wakisema wazi pengine haya mambo yanaweza yakapungua kulingana na adhabu ambazo zinatolewa na Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na changamoto kubwa sana ya TCRA kufungia Vyombo vya Habari bila kuwaita na kuwasikiliza. Tunataka kujua, haki iko wapi kama unamfungia mtu bila kumsikiliza. Malalamiko yamekuwa makuwa hasa kwa hawa wanaotumia mitandao ambao vyombo vyao vya habari viko mitandaoni. Wanafungiwa sana bila hata kuitwa na kusikilizwa na wao waweze kujieleza. Kwa hiyo, ningeomba sana Serikali iwe inafanya utaratibu wa kuwaita wale wanaowafungia, wawasikilize, wakishawasikiliza ndiyo waweze kufanya maamuzi kuliko kuwaumiza kama ambavyo wanafanya sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na ufungiaji pia wa vyombo vya habari kama magazeti na magazeti haya yamekuwa yakichaguliwa, yapi yafungiwe na mengine yasifungiwe. Sasa tungetaka kujua, Serikali ituambie ni utaratibu upi au ni maudhui gani yanayotakiwa kwenye gazeti yaandikwe ndiyo gazeti lifungiwe na gazeti hili lisifungiwe. Kwa sababu unaona kuna magazeti mengine yanaandika vitu vya ajabu lakini utashangaa magazeti haya hayafungiwi, yanafungiwa magazeti mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaomba tufahamu na tujue haya magazeti yanayofungiwa, yanafungiwa kwa makosa yapi na haya ambayo yanaendelea kuwepo na tunayaona mitaani yakiandika vhabari za ajabu, yenyewe yanakuwa na uhalali gani wa kuendelea kuwepo kwenye tasnia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeomba nishauri kidogo Serikali kuhusiana na suala zima la ruzuku. Ningeishauri Serikali iondoe mpango wa kutoa ruzuku kwa watoa huduma za internet ili kupunguza gharama za upakuaji wa mada ama machapisho ama vitabu. Tunafahamu kabisa sasa hivi hata wanafunzi wanapewa masomo yao katika mitandao. Sasa wanapokuja kwenye suala la kupakua unakuta kwamba gharama inakuwa kubwa zaidi. Kwa hiyo, nashauri Serikali ingejitahidi kutoa ruzuku ili basi wanafunzi hawa na hata maeneo mengine ya watu wa Serikalini ambao wanafanya machapisho mbalimbali ziweze kuwa hazina gharama zozote, yaani iondolewe kabisa na iweze kuwa bure.

Mheshimiwa Mwenyekiti, natoka Mkoa wa Tabora. Moja kati ya Mikoa ambayo ina changamoto kubwa sana ya mawasiliano, unaweza ukajikuta umetembea hatua chache tu huwezi kupata mawasiliano. Amezungumza hapa Mbunge wa Tabora Mjini lakini naomba niongezee. Jimbo la Tabora Mjini lina Kata 29, katika kata hizi 29, Kata 12 ni Kata za Vijijini. Unapokwenda kwenye Kata hizi, ukitoka tu kwenye kata ya mjini ukaingia kwenye kata ya vijijini mawasiliano yanakata kabisa. Kwa hiyo, hata kama unakuwa na changamoto yoyote ambayo umeiacha huku mjini, mtu anapokutafuta huwezi kupata mawasiliano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sana Wizara iangalie maeneo haya iweze kutupelekea minara ili wananchi wale na wao waweze kupata huduma ya mawasiliano. Kwa sababu, inafika mahali mtu anapotaka kupata mawasiliano lazima apande kwenye eneo la muinuko…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ya pili hiyo, ahsante na mwinuko.

MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ya kwanza!