Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Hon. Rashid Abdallah Shangazi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mlalo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ya kuwa mzungumzaji wa kwanza katika Wizara hii ya Teknolojia ya Habari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nitumie nafasi hii kukupongeza wewe binafsi kwa imani ambayo Wabunge wamekuwa nayo juu yako na kukurudisha katika kiti cha enzi, na ninaamini kwamba utatuombea dua na siku ya Jumamosi mambo yatakuwa mazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Waziri mwenye dhamana ya Wizara hii, lakini pia nimpongeze Naibu Waziri, Mheshimiwa Eng. Andrea Mathew Kundo pamoja na Katibu Mkuu, Dkt. Chaula, lakini pia na Naibu Katibu Mkuu Jim Yonazi, kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii bado ni mpya kwa maana ya kuundwa hivi karibuni lakini mambo ambayo inafanya ni mambo ya siku nyingi. Na Wizara hii imeundwa mahususi kabisa kuja kuwasaidia Watanzania na hususan vijana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Ilani ya Chama chetu Cha Mapinduzi katika ukurasa wa 96, imezungumzia suala la uwekezaji na kuwezesha mashirika kimitaji na kimenejimenti. Kwa bahati nzuri sana menejimenti iliyopo sasa chini ya Mtendaji Mkuu wa TTCL Waziri Kindamba, anafanya kazi nzuri sana, na kama Serikali ikimpa ushirikiano tunaoutaraji ambao umeelekezwa katika ilani wa uwezeshaji wa kiuchumi na kimenejimenti, maana yake shirika hili litakwenda mbali sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa masikitiko makubwa kama ambavyo mmesikia ripoti ya Kamati hapa inaonesha kwamba madeni makubwa ambayo TTCL anadai yamesababishwa na Serikali. Kwa hiyo, Serikali yenyewe imekuwa sasa ndio muuaji wa mashirika yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, kwa hiyo katika eneo hili hatutakubali kwa sababu tumekukabidhi tools za kusimamia Wizara hii kupitia ilani ya chama, kwa hiyo chama tutakuuliza; tumekupa ukaue shirika au ufanye shirika lifanye kazi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa ripoti ya CAG, takribani bilioni 40 zinadaiwa kupitia Mkongo wa Taifa. Kamati hapa imeeleza kwamba na yenyewe inaona takribani dola milioni 68 za Mkongo wa Taifa ni deni kutoka TTCL. Kwa hiyo, tunaomba sana kwamba eneo hili tulisimamie vizuri ili shirika hili liweze kushindana na mashirika binafsi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ikumbukwe hatujaweka mtaji wowote mkubwa kwa kipindi cha takribani miaka kumi mpaka kumi na mbili wakati kampuni hizi binafsi karibia kila mwaka zinaweka mtaji wa dola 100,000 mpaka 150,000. Katika hali ya kawaida hatuwezi kufanya Shirika hili lishindane. Kwa kweli tunaomba sana Shirika hili lijengewe uwezo, uwezo wa management upo na tunaridhika nao lakini uwezo wa mtaji ndiyo jukumu la Serikali hasa kupitia madeni …

MWENYEKITI: Mheshimiwa Shangazi makampuni binafsi hayaweki dola laki moja wanaweka dola milioni mia moja kila mwaka. (Makofi)

MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa sahihisho hilo, sasa nadhani Mheshimiwa Ndugulile amekaa kwa kutulia pale unaweza ukaona kwamba makampuni binafsi wanaweka dola milioni mia moja sisi miaka 12 mpaka 15 hatujaweka chochote. Hata hicho wanachozalisha tunaendelea kukivuna, madeni yale ambayo Serikali inazalisha hatuyalipi. Kwa hiyo, tunaomba suala hili lishughulikiwe na jioni hapa kwenye shilingi tunakuandaa kabisa uwe tayari vinginevyo leo utaondoka bila mshahara hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo nilitaka nilizungumzie ni kwamba Shirika hili tunataka liwezeshwe kimenejimenti kwa maana kwamba liwe huru kibiashara. Yapo mashirika kama haya kwenye nchi za wenzetu, kwa mfano, kuna Deutsche Telecom Ujerumani, China Telecom, Telecom Egypt, Telecom Namibia, ni Mashirika ya Umma lakini yanajiendesha kibiashara moja kwa moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa huku tunakoendesha sana kwa kisiasa hivi ndiyo maana wakati mwingine sasa tunayanyang’anya hata mitaji ya kujiendesha na kuyafafanisha na makampuni binafsi, hii siyo sawa. Kwa kuwa vijana tuliowakabidhi wana uwezo wa kuliendesha kimenejimenti ni lazima tulipe sasa kazi ya ziada na tupate shirika ambalo linakuwa la matokeo, result oriented. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo napenda kuchangia ni TCRA. Hapa napo kuna shida, sisi kama Taifa ni lazima tutangaze utamaduni wetu kimataifa na hili eneo zile TV za kulipia (Pay TV) zinafanya kazi nzuri sana, lakini zinazuiliwa kuweka matangazo katika zile channel zao ambazo zipo katika Pay TV. Kwa mfano, Azam Media kupitia Cinema Zetu ambapo wote tunafahamu kwamba tasnia ya Bongo Movie na Bongo Fleva wanaitumia sana ku-promote muziki wao, hawaruhusiwi kuweka matangazo wala kuwa na wadhamini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Pay TV ndiyo TV pekee ambazo zinaonekana ndani na nje ya nchi kwa maana kwamba zinakuwa katika ving’amuzi vya ndani na vya nje, kule ndiyo utamaduni wetu unaweza ukaonekana. Utamaduni huu ukionekana kupitia wadhamini na matangazo maana yake uzalishaji wa hizi sinema utakuwa bora zaidi na vijana wengi watapata ajira ya kutosha hapa na matokeo yake na Serikali nayo itapata kodi kupitia matangazo na udhamini. Sasa Serikali inakwama wapi kuziruhusu hizi Pay TV kuweka matangazo na wadhamini? Hii siyo sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, TV kama ya Wasafi, kijana mdogo yule anajaribu kukua, lakini tunamuwekea vizingiti vya namna hii, tunatarajia tuwe na Wasafi nyingi, ni watu wangapi wameajiriwa ndani ya Wasafi Media. Unapowanyima fursa ya kuweka matangazo na kuwa na wadhamini atatokaje huyu kwenda kuzalisha vijana wengine watengeneze maudhui mazuri ili yauzike kimataifa na sisi utamaduni wetu uzidi kukua huko lakini mwisho wa siku Serikali mtapata kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi Azam Media ndiyo inaonyesha mpira katika Ukanda huu wa Kusini mwa Afrika inashindana na TV nyingi za Kimataifa DSTV, GTV na nyinginezo, lakini ile ni sifa ya Watanzania. Mwaka huu wameweka uwekezaji mkubwa, nadhani tutatangaziwa hivi karibuni kupitia ligi ya VODACOM mkataba wa miaka kumi shilingi bilioni 190, haijawaji kutokea. Hiki ni chombo cha Watanzania, hizi ni bidhaa za Watanzania lazima tufaharike nazo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapowawezesha hawa ndiyo wanaongezeka akina Baraka Mpenja kule ambapo wanapata ajira, akina Ally Kamula watapata ajira tutakuwa nao, lakini wakina Gift Macha watapa ajira tutakuwa nao. Sasa TCRA hili eneo la kwenye Pay TV matangazo na udhamini tatizo lenu ni nini? Mbona Serikali wakati mwingine mnakuwa na wivu ambao hauna sababu? Kwa sababu kwa kupitia matangazo na huo udhamini tutapata kodi na tukipata kodi ndiyo tutazidi kutanua hii tasnia na itakuwa kubwa zaidi, itaajiri vijana wengi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua kabisa kwamba katika ukuaji wa pato la Taifa ina sehemu kubwa sana ya mchango wa sanaa, sasa sanaa yetu itakuwa tu endapo itakuwa inaonekana katika ving’amuzi vya kimataifa na vya ndani kwa sababu sasa ndani tumejitosheleza twende nje, tuwaruhusu hawa waweke matangazo. Utalii wetu pia tutautangaza kupitia hizo Pay TV tukiweka matangazo pale Nigeria, Ivory Coast na kila mahali wataona. Tunalalamika hapa kwamba hatutangazi utalii wetu tunaweza tukautangaza kupitia Pay TV.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi hii, huo ndiyo ulikuwa mchango wangu kwa siku ya leo. (Makofi)