Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Eng. Dr. Leonard Madaraka Chamuriho

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia afya njema na kutuwezesha kufika hatua hii ya mwisho katika kuhitimisha hoja yangu ambayo niliiwasilisha jana tarehe 17 Mei na kujadiliwa na Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee kabisa napenda kuchukua fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuniamini kuongoza Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Wizara ambayo ni kichocheo cha ufanisi wa utendaji wa sekta zingine za kiuchumi na kijamii. (Makofi)


Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru pia Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa maelekezo na miongozo yake ambayo imenisaidia wakati nikitimiza majukumu ya Serikali katika kipindi hiki kifupi kutoka ateuliwe kuwa Makamu wa Rais.


Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie fursa hii kumpongeza Kiongozi wa Shughuli za Serikali Bungeni Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa Mbunge, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutumia uzoefu wake wa uongozi katika kutuongoza kwa umahiri na kimkakati kutekeleza majukumu yetu kila siku hapa Bungeni.


Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie fursa hii pia kumshukuru Mheshimiwa Spika na pia kukushukuru wewe binafsi Naibu Spika na Wenyeviti wa Wabunge kwa ushirikiano mnaoipatia Wizara hii ninayoiongoza katika kutekeleza majukumu mbalimbali ya Serikali ndani na nje ya Bunge.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, nichukue fursa hii kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ushirikiano wao wa dhati wanaonipatia kutoka nilipoteuliwa kuwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, nimejifunza masuala mengi kutoka kwao, ujuzi ambao utaniwezesha kutekeleza majukumu yangu kwa sasa kwa kiwango cha hali ya juu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia kipekee nimshukuru Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Mheshimiwa Moshi Selemani Kakoso pamoja na Wajumbe wa Kamati yake ambao wamepitia bajeti ya Wizara kwa niaba ya Bunge lako Tukufu na kuanisha namna bora ya kiutendaji kazi kufikia malengo ya Taifa letu. Naahidi kwamba Wizara itazingatia maoni, ushauri na mapendekezo ya Kamati hii kwa weledi wa hali ya juu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee niwashukuru Mheshimiwa Engineer Godfrey Msongwe Kasekenya na Mheshimiwa Mwita Mwikwabe Waitara pamoja na Makatibu Wakuu Mhandisi Joseph Christopher Mwalongo na Gabriel Joseph Migile wa Ujenzi na Uchukuzi kwa ushirikiano wao katika kutekeleza majukumu yangu. Aidha, nawashukuru Wakuu wa Idara, Vitengo, Wenyeviti wa Bodi zilizo chini ya Wizara, Viongozi wa Taasisi na Watendaji wote wa wizara kwa ushirikiano mzuri na juhudi walizozifanya kuhakikisha kwamba tunatimiza majukumu tuliyokabidhiwa na Taifa ipasavyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nilihakikishie Bunge lako Tukufu na Watanzania kwa ujumla kwamba, Wizara ninayoisimamia itatimiza matarajio ya Serikali na kuhakikisha kazi inaendelea. Mimi kama waziri mwenye dhamana nitatekeleza wajibu wangu kwa ufanisi na weledi wa hali ya


juu kwa kushirikiana na wenzangu katika Wizara yangu. Ni imani yangu tutafikia matarajio ya Taifa ikiwa ni pamoja na yale ya Waheshimiwa Wabunge.

Mheshimiwa Naibu Spika, niwashukuru tena Waheshimiwa Wabunge waliochangia hoja ya Mpango wa Bajeti ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, michango ambayo itanisaidia sana katika kuboresha hoja niliyoiwasilisha. Naomba sasa nijielekeze katika kutoa maelezo kwenye hoja mbalimbali zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kutumia fursa hii kuwatambua Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia katika bajeti yangu. Waheshimiwa Wabunge 59 waliochangia wakati wa majadiliano ya hoja ya Waziri Mkuu na Waheshimiwa 158 wamechangia wakati wa hoja ya Wizara yangu ambapo 84 wamechangia kwa kuzungumza na 14 wamechangia kwa maandishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi punde Waheshimiwa Manaibu Mawaziri wa Wizara yangu wameanza kujibu baadhi ya hoja za Waheshimiwa Wabunge. Nawashukuru sana kwa jinsi ambavyo wamejibu baadhi ya hoja zilizojitokeza wakati wa kujadili hoja hiyo niliyoitoa hapa Bungeni wakati nawasilisha hapo jana, hoja kuhusu mpango wa bajeti wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwa mwaka 2021/ 2022.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, naomba kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba Wizara itajibu hoja zote za Waheshimiwa Wabunge kwa maandishi na kuziwasilisha kwao kabla ya kuhitimisha kwa Mkutano wa Bunge hili la Bajeti unaoendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa nianze kuhitimisha hoja yangu kwa kutoa ufafanuzi wa kiujumla wa baadhi ya hoja zilizojitokeza. Bajeti ya Wizara imejikita katika kutengeneza Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025, Mpango wa Taifa wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano kuanzia 2021/2022 hadi 2025/2026, Ilani ya Uchaguzi wa


Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020, maagizo mbalimbali ya Viongozi Wakuu wa Serikali na Sera, Mikakati na Miongozo Mbalimbali ya Kitaifa na Kimataifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mpango wa Taifa wa Maendeleo pamoja na Ilani ya Uchaguzi zina lengo kuu la kujenga uchumi shindani na viwanda kwa maendeleo ya watu. Wizara ninayoiongoza ina jukumu kuu la kuwezesha kufikiwa kwa lengo hili kwa kuwa inawezesha sekta nyingine kufikia malengo yao ikiwa ni pamoja na kuunganisha maeneo ya uzalishaji na masoko. Hii ina maana kwamba ufanisi wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi utawezesha Sekta nyingine za uchumi na kijamii kuwa na ufanisi.


Mheshimiwa Naibu Spika, katika uchaguzi wa mwaka 2020 Chama cha Mapinduzi kilipata ushindi wa kishindo ngazi ya Urais, Wabunge na Madiwani. Hii ilitokana na ubora wa Ilani yake ya Uchaguzi ambayo kiujumla inalenga kujenga uchumi imara na kuwawezesha wananchi kunufaika nayo ikiwa ni pamoja na kuondoa kila aina ya kero za wananchi kuliko ilivyokuwa kwa Ilani nyingine. Kwa kuzingatia hili nina wajibu wa kueleza vitu ambavyo Wizara ninayoiongoza itatekeleza katika kipindi cha miaka mitano ijayo kuanzia 2021/2022 hadi 2025/2026 tukianza na mwaka wa fedha 2021/ 2022.

Mheshimiwa Naibu Spika, baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wameitaka Serikali ya Awamu ya Sita kuendelea na utekelezaji wa miradi ya kimkakati iliyoanza kutekelezwa kipindi cha kwanza cha Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, kwa kuwa miradi ndiyo msingi wa ukuaji wa uchumi wa Taifa letu. Miradi hiyo ni pamoja na kuendelea na ujenzi wa ukarabati wa barabara kuu za mikoa ili kuiunganisha nchi, ujenzi wa madaraja ya muhimu ya barabara na vivuko, kuendelea na ujenzi wa reli ya Standard Gauge, uboreshaji na upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam na kuendelea na ujenzi wa ukarabati wa meli katika maziwa.


Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi thabiti wa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imedhamiria kuendelea kutekeleza miradi yote ya kimkakati ili Taifa liweze kunufaika nayo kwa kujenga uchumi endelevu. Miradi hiyo inatekelezwa na Wizara yangu kama ilivyoanishwa kwenye Mpango wa Taifa wa Maendeleo na Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020 kwa umakini na umahiri mkubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka sasa mazuri tunayoyaona, lakini tumedhamiria kazi iendelee ili mazuri zaidi yaje kuonekana ifikapo mwaka 2025. Serikali zilizopita za Chama cha Mapinduzi zilijiwekea dhamira ya kuunganisha Makao Makuu ya Mikoa yote nchini kwa barabara kuu za lami. Dhamira hii inakaribiwa kufikiwa ambapo kwa uchache kwa nchi ambapo kazi inaendelea. Kazi hizo zinahusisha ujenzi wa barabara za kuunganisha Mikoa ya Tabora na Kigoma, Mikoa ya Kigoma na Kagera, Mikoa ya Tabora na Mbeya. Aidha, maeneo mengine ni pamoja na kuunganisha na Mkoa wa Manyara, Mkoa wa Morogoro ambao utapewa kipaumbele ndani ya kipindi hiki cha utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020-2025.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi na wasaidizi wangu tutakuwa karibu sana, karibu sana na mahali pa kazi za ujenzi wa barabara zinazofanyika ili kuhakikisha zinafanyika kwa ubora kama walivyoshauri Waheshimiwa Wabunge. Ningependa kulitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba tayari tunatangaza miradi 16 ya barabara ambayo tumeanza kuitangaza wiki hii, ambayo ni kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa kwanza, ni Barabara ya Ntendo hadi Muze kilometa 25; Barabara ya Isonje hadi Makete kilometa 25; Barabara ya Mianzini hadi Ngaramtoni kilometa 18; Barabara ya Bigwa – Kisaki kilometa 15; Barabara ya Uvinza – Malagarasi kilometa 51.1; Barabara ya Mbulu – Hydom kilometa 25; Barabara ya Matai – Kasesya kilometa 25; Barabara ya Ntyuka Junction – Mvumi Hospital


hadi Kikombo Junction kilometa 25; Barabara ya Tarime - Mgumu kilometa 25; Barabara ya Vikonje hadi Uvinza kilometa 25; Barabara ya Kibondo hadi Mabamba kilometa 10; Barabara ya Noranga – Itigi hadi Mkiwa kilometa 25; Barabara ya Itoni hadi Lusitu kilometa 50; Barabara ya Handeni hadi Kibereshi kilometa 20; Barabara ya Kitai hadi Litai kilometa 35; na Barabara ya Kibaoni hadi Stalike kilometa
50. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo Bunge lako Tukufu wataona kwamba kazi inaendelea na tunaendelea kuZitendea haki barabara kama ambavyo zimepangwa katika bajeti yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Viwanja vya Ndege vina uhusiano wa karibu sana na huduma za usafiri kwa njia ya anga. Baadhi ya Waheshimiwa Wabunge kwa nyakati tofauti ikiwa ni pamoja na kwenye Bunge hili la bajeti wameainisha umuhimu wa usafiri wa njia ya anga. Kiutalam ndege inatakiwa kuwa angani kwa wastani wa masaa 12 hadi 15 katika saa 24 za siku, hiki ni kigezo kimoja muhimu cha matumizi sahihi ya ndege.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, nchi yetu ina urefu wa zaidi ya kilometa 1,200 Mashariki hadi Magharibi na zaidi ya kilometa zaidi 1,700 kutoka Kaskazini Magharibi hadi Kusini Mashariki. Umbali huu ni stahiki sana kwa matumizi ya usafiri wa njia ya anga, hata hivyo ni viwanja vile tu, vya Julius Nyerere International Airport, Kilimanjaro International Airport, Mwanza na Dodoma ambavyo kwa sasa vinaweza kutumika kwa saa 24 kwa siku.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili Shirika letu la Ndege linufaike na uwepo wa viwanja hivi vya ndege, napenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba Wizara kwa kushirikiana na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege itawekeza vifaa muhimu vyenye kukidhi mahitaji ya utoaji huduma wa ATCL ikijumuisha taa za kuongoza ndege kwenye viwanja vya kimkakati kuanzia mwaka wa fedha 2021/2022. Viwanja ambavyo vipo kwenye mpango huo ni Uwanja wa Ndege


wa Kigoma, Uwanja wa Ndege wa Mbeya, Uwanja wa Ndege wa Mtwara, Uwanja wa Ndege wa Bukoba na Uwanja wa Ndege wa Geita.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Viwanja vya Ndege vya Tabora, Shinyanga, Sumbawanga, Songea na Iringa navyo wakati wa ukarabati wake vitafanyiwa utaratibu wa kuwekewa taa za kuongozea ndege. Ukamilishaji wa mradi huo wa kuweka taa za kuongozea ndege kwenye viwanja vya ndege utaongeza ufanisi kiutendaji kwa Kampuni ya Ndege ya Tanzania (ATCL). Maelekezo yangu ni kwamba kabla ya mwisho wa mwaka wa 2021 Mamlaka ya Viwanja vya Ndege, TANROADS na ATCL zikutane ili kujipanga kufikiwa kwa lengo hili mahsusi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi nyingi duniani zilizopiga hatua kubwa za kimaendeleo zimefanya hivyo kutokana na sababu kadhaa mojawapo ikiwepo ni kuwepo na huduma za reli zenye uhakika, gharama nafuu na salama. Kwa kulitambua hilo moja ya vipaumbele kwenye bajeti ya mwaka 2021/2022 ni kuendelea na ujenzi wa reli ya SGR.


Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kulihakikishia Bunge hili Tukufu kwamba tutaendelea na ukamilishaji wa ujenzi wa vipande viwili vya reli vya SGR ambavyo ni Dar es Salaam hadi Morogoro kilometa 300, ambapo kwa sasa imefikia asilimia 91 na kipande cha Morogoro hadi Makutupora kilometa 422 kilichofikia asilimia 60.2 ya ujenzi na kipande cha Mwanza hadi Isaka kilometa 341 ambacho kwa sasa Mkandarasi yupo katika hatua za awali ya kuanza kazi.


Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Wizara kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango itaendelea na kipaumbele cha kutafuta fedha za ujenzi wa reli ya SGR kwa vipande vitatu vya Makutupora hadi Tabora kilometa 294, Tabora hadi Isaka kilometa 133 na kile cha Tabora hadi Kigoma kilometa 411.


Mheshimiwa Naibu Spika, ukamilishwaji wa reli hizi utaziingizia Taifa kipato kikubwa cha fedha za kigeni kutokana na kusafirisha mizigo ya nchi jirani za Burundi, Rwanda, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Kwa sasa wataalam wanakamilisha taratibu za kuanza kumtafuta mkandarasi wa kujenga kipande cha Uvinza hadi Msongati kwa ajili ya kubeba tani milioni tatu kwa mwaka za mizigo ya kwenda na kutoka Burundi hadi Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara yangu kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango itafanyia kazi ushauri wa Waheshimiwa Wabunge katika kutumia mbinu mbalimbali za kupata fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa vipande vilivyobaki kwenye mtandao wa Standard Gauge.

Mheshimiwa Naibu Spika, usafiri wowote unatakiwa kuwa na vigezo vikuu vitatu; uhakika, gharama nafuu na usalama. Kwa upande wangu nitalisimamia kwa umakini suala la usalama wa usafirishaji na usafiri, nitaendelea kuhakikisha kwamba matumizi bora ya TEHAMA katika kuboresha huduma za uchukuzi unafanyika. Aidha, changamoto katika matumizi ya mifumo ya ufuatiliaji wa mabasi na tiketi za kielektroniki zitafanyiwa kazi kwa karibu na kushirikisha wadau wote hususani wasafirishaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu taasisi za mafunzo Sekta ya Uchukuzi nchini itazidi kuboreshwa kwa kiwango kikubwa kutokana na ukuaji huo, ukuaji wa mahitaji ya wataalam wenye weledi wa kusimamia na kuendesha miundombinu na huduma za uchukuzi yanazidi kukua.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutambua hili Wizara itazidi kuboresha vyuo vya mafunzo ili viweze kuzalisha watalaam wenye weledi unaotakiwa kukidhi haja hii. Aidha, tutafanya jitihada za makusudi kukamilisha uanzishwaji wa Bodi ya Watalaamu wa Logistic na Usafirishaji ili watalaam wa sekta ya uchukuzi waweze kusimamiwa vizuri na sheria hiyo.


Mheshimiwa Naibu Spika, kabla ya kuhitimisha, ningependa kuongelea hoja mahsusi ambazo zimetolewa na Wabunge, kwanza nikianza na hoja ya daraja la JPM ambalo tuliambiwa lina changamoto kwamba kuna mkandarasi ambaye hawajibiki vizuri, lakini ukweli ni kwamba mkandarasi yule ameahidi kuchangia huduma kwa jamii, kwa Kijiji cha Bukumbi kwa kuchangia milioni 50 na analipa mrabaha wa kila tripu ya kokoto kwa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi na hadi hivi sasa amekwishalipa jumla ya milioni
20. Vilevile mkandarasi huyo ameajiri wakandarasi wazawa wanne ambao wanamsaidia katika kazi hizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile wazawa ambao wameajiriwa katika shirika lile wanafikia asilimia 90, kwani kuna wafanyakazi 274 ambao ni wa Kitanzania kati ya wafanyakazi 350 ambao wanafanya kazi pale. Mnamo tarehe 12 Januari mwaka huu nilitembelea daraja lile na taarifa hizi nilizipata pale mimi mwenyewe.


Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu ATCL tayari tunafanya kila tunaloliweza kuhakikisha kwamba mifumo ambayo inafanya kazi pale hairuhusu watu kufanya hujuma za kujaza ndege bila sisi wenyewe kutarajia. Mifumo ile hairuhusu kukata tiketi kama ndege imejaa lakini kuna station ambazo zina adhabu ya kuwa haziwezi kujaza ndege, vituo hivyo ni kama Bukoba, Songea, Mbeya na Iringa ambapo kiutalaam huwezi kujaza ile ndege na ukaondoka nayo kwa usalama, hivyo huwa haijai na pengine wananchi hudhani kwamba ndege ile imeachwa bila kujaa kwa makusudi, lakini siyo hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri umetolewa kuhusu viwanja vya ndege, ujenzi wake, tutakwenda kulifanyia kazi hilo, kwamba kuangalia ni wapi waendelee kuvijenga ni TAA au TANROADS kulingana na ushauri ambao Wabunge wametupatia. Vilevile zile bypasses katika Miji ya Mbeya, Songea, Dodoma, Mwanza na Arusha na Iringa tutakwenda kuzifanyia kazi ili tuweze kuendana na ushauri wa Bunge lako Tukufu. (Makofi)


Mheshimiwa Naibu Spika, ugawaji wa rasilimali vilevile utazingatiwa kulingana na ushauri walioutoa Wabunge hapa Bungeni na hakutakuwa na tashiwishi katika suala hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kumeongelewa vilevile ucheleweshaji wa kutolewa GN kwa ajili ya barabara mbalimbali. Hili suala nalo tunaenda kulifanyia kazi tayari, tumekwishaongea na wenzetu wa Wizara ya Fedha na umeandaliwa mpango maalum ambao utahakikisha kwamba hizi GN za misamaha ya kodi zinatolewa mapema ili tuweze kuharakisha katika mijengo hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, hitimisho, mwisho ninawaomba Waheshimiwa Wabunge waipitishe hoja yangu kwa kuwa tunataka kusimamia kwa niaba ya wananchi wote utekelezaji wa maendeleo na ya Ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2020 pamoja na mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Tatu wa mwaka 2021/2022 hadi 2025/ 2026.

Mheshimiwa Naibu Spika, nyenzo ya kutuwezesha sisi pamoja na watumishi wenzetu katika Wizara hii ni bajeti hii na kupitia kwake Serikali itafanya kila iwezekanalo kuhakikisha kwamba, miundombinu ya sekta ya ujenzi na uchukuzi na huduma zake zinaboreshwa na kulingana na matakwa ya sasa na miaka ijayo. Hivyo, kwa niaba ya wenzangu katika Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi na kwa niaba yangu mwenyewe ninaomba sana bajeti hii ipitishwe ili kazi iendelee.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hoja zingine ambazo zimetolewa na Wabunge zote tutazizingatia kwa mfano hii ya viwanja vinne ambavyo ni viwanja vya Sumbawanga, Kigoma, Tabora na Shinyanga ambavyo vina ufadhili wa benki ya EIB tunakwenda kumalizia maongezi nao ili tuweze kuhakikisha kwamba vile vikwazo ambavyo vilikuwepo tunaviondoa vyote na viwanja hivi vinaanza kujengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, kwa reli yetu ya TAZARA ambayo imeonekana ni kiungo muhimu kwa nyanda


za juu, tayari tuna mpango wa open access ambao tunaruhusu watu binafsi kuendelea na kupitisha mizigo yao pale. Tayari kuna kampuni moja ambayo inaitwa Calabash inafanya kazi hiyo na tayari tumetoa zabuni ambapo wauzaji wawili wa kizawa wako tayari kujiunga pale na kuweka treni zao binafsi ili ziweze kusaidia katika kuendesha pale TAZARA.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vile vile tunaendelea na ukarabati wa reli ya TAZARA ili kuhakikisha kwamba reli hiyo inatoa huduma nzuri katika mikoa ya nyanda za juu na kote inakopita.


Vilevile, tunalipa madeni ya TAZARA hasa ukizingatia kwamba tunatoa ruzuku ya mishahara kwa wafanyakazi wa TAZARA ili tuweze kuhakikisha kwamba TAZARA yetu inaendelea. La mwisho kwa TAZARA tunamalizia marekebisho ya sheria mpya ili tuweze kuboresha uwekezaji ndani ya TAZARA lakini vile vile tuwezeshe kuruhusu mambo ambayo yataongeza tija. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa hoja.
(Makofi)