Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Mwita Mwikwabe Waitara

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tarime Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Namshukuru Mungu kwa uzima na nafasi. Pia namshukuru Mheshimiwa Waziri, Eng. Dkt. Leonard Chamuriho, kwa ushirikiano; Naibu Waziri mwenzangu; Makatibu Wakuu wote wawili; familia yangu; na wapiga kura wa Jimbo la Tarime Vijijini; pia namshukuru sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuniamini katika nafasi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge, shikamoo. Tumewasikia. Nimekaa hapa, tumesikiliza maoni. Nimewaamkia Waheshimiwa Wabunge, shikamoo tena Waheshimiwa Wabunge. Nawasalimia kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Kicheko/Makofi)

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, hii Serikali ni Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, hii ni bajeti yake ya kwanza katika Awamu ya Sita. Wizara hii ya Ujenzi na Uchukuzi ndiyo Wizara ambayo alikuwa anaongoza Hayati Dkt. John Pombe Magufili. Kwa hiyo, nilishtuka sana nilipoona Waheshimiwa Wabunge wanataka kupiga sarakasi kwa bajeti ya kwanza ya Mheshimiwa Mama Samia na Wizara ya Hayati Dkt. Magufuli na wengine wakataka kugaragara.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niwaombe, hakuna sababu ya kugaragara, kazi inaendelea. Sisi wasaidizi wa Mheshimiwa Rais kwa niaba ya Serikali hii ya Awamu ya Sita tunafanya kazi hiyo. Ndiyo maana nikasema shikamooni Waheshimiwa Wabunge na tumewasikia vizuri kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Baba wa Taifa aliwahi kusema, ili Taifa liendelee mambo matatu yanahitajika; la kwanza ni watu. Sisi tupo Waheshimiwa Wabunge na ninyi na Watanzania wengine. La pili, akataka tuwe na uongozi bora. Uongozi bora wa Awamu ya Sita upo, mama Samia ameshika usukani. Pia tunatakiwa tuwe na siasa safi, ndiyo maana hata juzi wakati Mheshimiwa Rais Samia anateua Wakuu wa Mikoa, ameteua na mtu aliyekuwa Upinzani, tena alipambana naye kutaka kuwa Rais wa nchi hii; kwa hiyo, hiyo ni siasa safi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile maoni yote ya Waheshimiwa Wabunge wamezungumza hapa, mimi ni Naibu Waziri mzoefu kidogo, hii ni Wizara ya tatu; nilikuwa TAMISEMI, nikaenda Muungano, sasa nimekuja Ujenzi. Ukweli ni kwamba wakati Waheshimiwa Wabunge wanachangia hoja, mimi nilikuwa Mbunge wa Ukonga, Mbunge wa mijini. Sasa ni Mbunge wa Tarime Vijijini. Nilikuwa nawasikiliza vizuri kuanzia kwenye utosi mpaka kwenye unyayo wa mguu. Mnachokizungumza, mnataka barabara za majimbo yenu zipitike na kura zetu ziendelee kuwa salama na hasa kwenye uchaguzi ujao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niwakumbushe Waheshimiwa Wabunge wa Chama cha Mapinduzi, tunayo maelekezo ya chama katika maeneo hayo mahususi kabisa, tunayafanyie kazi na yote yanaungana mkono na maoni mliyoyatoa hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niseme kwamba katika michango ya Waheshimiwa Wabunge, kuna Wabunge walijaribu kuhoji hata miradi mingine ya kimkakati. Amiri Jeshi Mkuu, Kiongozi Mkuu wa Serikali, Rais wa Nchi, ameshasema kazi iendelee na amesema ndani ya Ukumbi huu wa Bunge kwamba miradi ya kimkakati, miradi vielelezo ni lazima iendelee. Kwa hiyo, hakuna namna ya kuanza kujadili tena habari ya Daraja la Busisi, habari ya SGR, Bwawa la Umeme la Mwalimu Nyerere na miradi mingine ya kimkakati; itaendelea. Rais ameshasema, nani tena apinge katika mazingira hayo? Kwa hiyo, hakuna mjadala mwingine wa hivyo. Sisi kazi yetu ni kutekeleza na kuhakikisha kwamba fedha ya Serikali inasimamiwa vizuri, kazi iende vizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hoja mahususi ambazo zimezungumzwa, nataka nijibu baadhi ya maeneo. Kwa mfano, maboresho ya bandari, imezungumzwa hapa. Hata hivyo, tukumbuke Mheshimiwa Rais juzi tu ameteua Mtendaji Mkuu wa Bandari hii; haya ni maboresho. Tunajua kwamba kuna fedha zimewekezwa kule Tanga, zimewekezwa Bandari ya Mtwara, tumeweka fedha Kigoma; na mabadiliko lazima yafanyike. Mtarajie mabadiliko makubwa katika maeneo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, kuna watu wamezungumza habari ya fidia; Mheshimiwa Kunti Majala amezungumza hapa. Juzi Kamati ya Miundombinu ilikuwa hapa, fedha zimetoka na watu wanalipwa fidia Uwanja wa Ndege wa Msalato, wanalipwa fidia Uwanja wa ring road ya hapa Dodoma, fedha zinatoka na mambo yote yanafanyiwa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Musoma, tunapozungumza Mheshimiwa Mathayo anajua kabisa, fedha zimetengwa; jana na leo na kesho, watu wote watakuwa wamelipwa fidia. Mkandarasi yupo site. Tarehe 30, Desemba, 2022 Uwanja wa Ndege wa Musoma utaanza kufanya kazi. Sasa kazi hii inafanyika vizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, zimezungumzwa hapa barabara. Nataka niwaombe Waheshimiwa Wabunge, kwa kweli Wizara hii inataka kufanya kazi nzuri sana. Wote hapa ni Wanasayansi; Dkt. Chamuriho ni Engineer, mimi ni Mwanasayansi hapa, tunajua barabara ni sayansi pia.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Kunti Majala ametaja barabara ambayo ina kilometa 20, wametengewa shilingi bilioni tano za kuanzia, anasema yeye hahusiki na fedha hiyo; lakini tunataka tujue kwamba kwa kuwa kuna Wabunge hapa kweli hawakupata mgao, haya ndiyo mambo ambayo Mheshimiwa Waziri ameshatuelekeza, tukimaliza tu bajeti hii kesho, sisi hatulali, ni kupitia maoni na mawazo ya Waheshimiwa Wabunge ili wale waliokosa kipindi hiki, bajeti ijayo uwe mjadala tofauti. Hata sisi tungefurahi sana mambo yakienda sawa sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumekubaliana na watendaji pia, baada ya bajeti hii kupitishwa leo, mkitupitishia fedha mkatutuma kazi, hata watendaji wenyewe huko waliko wakae mguu sawa. Haya mambo yote mliyojadili tumechukua, tumeyafanyia kazi. Sisi ni wasikivu Waheshimiwa Wabunge, ninaomba mtuelewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimalize kwa kusema hivi, yako mambo ambayo sisi tunategemeana sana humu; na hii ni Serikali ya Watanzania; na barabara hizi mnazozungumza; viwanja vya ndege na maeneo mbalimbali ni vitu ambavyo na sisi pia ni wahusika. Tunataka tusaidiane katika jambo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, wewe mwenyewe umezungumza, nami nimesema nitakwenda kwenye barabara yako kule Mbeya na shida ambayo unazungumza na migomo mbalimbali, Mheshimiwa Waziri ataeleza, tumewasikia vizuri sana. Nataka niwaambie tu kwamba mkipitisha fedha zinazotengwa hapa, sisi bajeti ijayo lazima tuje kuonesha zinafanya kazi zipi na utekelezaji wa miradi. Uzuri ni kwamba miradi yenyewe mtaiona huku.

Mheshimiwa Naibu Spika, mmetupa ushauri, sisi hatutalala. Mimi, Mheshimiwa Waziri, Naibu mwenzangu, watendaji wakuu na kila mtu pale alipo tutafanya kazi ya ziada sana. Tumepewa mfano hapa wakati wa mchango kwamba tuangalie mchango wa Wizara ya Maji, wamefanya kazi nzuri sana. Tumesema na Mheshimiwa Waziri kwamba kipindi kijacho, Wizara ya Ujenzi itakuwa ni Wizara ya kupigiwa mfano kwa sababu ni Wizara ambayo inashikilia uchumi wa nchi hii, inamgusa kila Mbunge, inagusa kila Mtanzania, inagusa kila mkoa, inagusa kila wilaya. Kazi yetu, Mungu ametupa uhai, Mheshimiwa Rais ametuamini; tutachapa kazi kweli kweli. Hapa kazi lazima iendelee.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme kwamba Waheshimiwa Wabunge, Waheshimiwa Mawaziri na watendaji wengine wa Serikali, Watanzania wanataka tufanye kazi; na wanataka wafanye kazi ili hotuba ya Mheshimiwa Rais nzuri hapa Bungeni lazima itimie kwa vitendo huko kila mwananchi alipo.

Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge, baada ya kusema hayo, nawashukuru sana kwa kunisikiliza, naomba niseme naunga mkono hoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi.