Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Anne Kilango Malecela

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Same Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kushukuru sana kwa nafasi uliyonipa. Vilevile nachukua nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Mawaziri wawili na watendaji wote wakuu wa taasisi ambazo ni za Wizara hii tunayoizungumzia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nawashukuru Wabunge sana. Wabunge wamefanya kazi kubwa sana kuanzia jana. Kazi waliyoifanya ni kazi yao ya Kikatiba. Naomba nikiri, kweli mimi tangu nilipochangia hotuba ya Waziri Mkuu nilizungumzia barabara.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niwaambie Serikali kitu kimoja; mnajenga barabara, lakini mnajenga barabara ambazo sizo. Hamjafanya research ya kutosha mkajua barabara zinazostahili kujengwa. Mnarudia barabara zile. Serikali imesoma hotuba hapa, lakini hotuba ambayo Serikali mmeisoma ni ya Serikali; hotuba ambayo inapaswa kutekelezwa na Serikali, ni hotuba inayotoka kwa wananchi hawa; hawa Wabunge ambao ndio wawakilishi wa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni vyema Serikali ikajua kwamba wanaozijua barabara hizi ni Wabunge. Wabunge ndio wanaotoka wananchi walipo; Wabunge wanawakilisha wananchi kwenye majimbo yao, ndio wanaozijua hizi barabara.

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme ukweli, sitaki kusema kwa kirefu, lakini Serikali niwaombe sasa, tena nawaomba kwa mara ya pili; fanyeni kazi kubwa kuanzia kesho, mpite nchi nzima ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mkazijue hizi barabara. Barabara nyingi vijijini hamjazijenga ndiyo maana kumekuwa na kelele mno hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hawa Wabunge wote waliosema, hakuna kichaa hata mmoja humu. Wote wana akili timamu. Haiwezekani mtu na akili zake timamu atake kucheza karate humu ndani, hapana. Anaogopa 2025 watammeza Wajumbe. Hali ni mbaya sana kwenye majimbo yetu, hasa ya vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali nawaomba – tena nisiseme kwamba nawaomba, hapana; nawasimamia sasa. Haya ni madaraka yangu niliyopewa na Katiba kwamba niwashauri, lakini wakati mwingine niwasimamie. Hamzijui barabara ambazo mnapaswa kuzijenga. Barabara nyingi sana, zote zilizotajwa na hawa Wabunge hapa, ndizo barabara ambazo zinahitaji kujengwa. Hotuba mliyoisoma hiyo, sasa pateni picha kamili, hotuba ni hii huku. Hii huku ndiyo hotuba. Sisemi lugha tofauti, lugha yangu ni kwamba hotuba mnayopaswa kuiangalia ni hii inayotoka huku sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nafikiri nimeeleweka.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Naibu Spika, dakika zangu mbili nizungumze kitu kimoja; barabara nimeeleweka…

NAIBU SPIKA: Kengele imeshagonga Mheshimiwa.

MHE. ANNE K. MALECELA: Hapana, dakika mbili bado.

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumze kidogo kuhusu bandari. Tumezungumza sana kuhusu barabara…

NAIBU SPIKA: Sekunde 30 malizia sentensi.

MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie tu kidogo, ahsante. Amenipa dakika mbili.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumezungumza sana kuhusu barabara, tunaisahau bandari. Bandari ni kitu kikubwa chenye mambo mengi ambalo ndilo lango la uchumi wa nchi hii, lakini bandari tumekwenda tukaiweka ndani ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi. Tuwe makini.

Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna mfanyabiashara mzuri kama India, lakini mwaka 2020 India ameichukua bandari akaiundia Wizara yake ili aweze kuishika vizuri.