Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Dr. Christine Gabriel Ishengoma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nianze kwa kuunga mkono hoja.


Mheshimiwa Naibu Spika, nitachangia kuhusu barabara, mipango mizuri ya Serikali ipo lakini nachoomba ni utekelezaji. Naongelea barabara ya Ngiloli – Iyogwe - Kilindi (Tanga). Tatizo hapa tunaomba ijengwe kwa kiwango cha lami. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, halafu jambo kubwa lingine ni kuhusu madaraja. Kuna madaraja ya Chakwale na Nguyami. Madaraja haya yanajengwa kila mwaka lakini mwaka mvua ikinyesha yanakatika. Je, ni lini haya madaraja ya Chakwale na Nguyami yaliyopo Gairo yatajengwa kwa ukamilifu ili kuondoa tatizo la kukatika kila mwaka kwani tunaharibu fedha za Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara nyingine nayoongelea ni ambayo imeshaongelewa ni ya Kidatu – Ifakara – Malinyi – Londo - Kitanda -Namtumbo. Barabara hii tumeiongelea mara nyingi humu Bungeni inasuasua na ni ya muhimu sana. Kwa hiyo, mipango yote iliyopangwa tunaomba itekelezwe kwa sababu tumeiongelea muda mrefu na lakini hakuna utekelezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara nyingine ni ya Bigwa – Mvuha - Kisaki ambayo inakwenda mpaka Bwawa la Mwalimu Julius Nyerere. Tunashukuru imewekwa kwenye mpango na imetengewa kiasi kidogo cha fedha, lakini kwa umuhimu wake tunaomba mipango yote iliyopangwa iweze kutelezwa kwa sababu nayo hii barabara tumeiongelea miaka nenda miaka rudi.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara nyingine ni Ubena - Zamozi - Ngerengere - Mvuha – Kisaki. Barabara hii nayo imetengewa fedha kiasi lakini kutenga sio kutenda, tunaomba itekelezwe kama ilivyopangiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara nyingine ni Dumila - Magole - Turiani - Mziha – Handeni. Hii barabara nayo tumeiongelea lakini nashukuru kipande cha Magole - Turiani kimetengenezwa kwa lami, kipande cha Turiani - Mziha - Handeni bado hakijatengenezwa. Naomba kufahamu hiki kipande kitatengenezwa lini? Kipande hiki pia kimetengewa fedha lakini naomba utekelezaji uende kama ilivyopangwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Dumila – Ludewa – Kilosa - Mikumi tumeiongelea mara nyingi. Barabara ya Dumila - Ludewa tayari imejengwa kwa kiwango cha lami na barabara ya kutoka Ludewa - Kilosa ujenzi unaendelea. Tatizo ni kipande cha barabara ya kutoka Kilosa - Mikumi, usanifu ulishafanyika muda mrefu, sasa mnasema mipango ya kutafuta hela inaendelea, sasa itaendelea mpaka lini? Naomba kujua kipande cha barabara ya kutoka Mikumi - Kilosa kitatengenezwa lini? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Ifakara – Lupilo
– Mahenge - Mwaya, sijaiona kwenye mpango wowote. Watu wa Mahenge tunaomba hii barabara kwa sababu Mahenge ni Wilaya inayozalisha sana mpunga na kuna madini. Naomba na barabara hii iweze kuonekana kwenye mpango. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Ifakara – Mlimba – Lupembe; wakati wa mvua huwezi kupita. Tunaomba na yenyewe itengenezwe vizuri sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna barabara ya kutoka Kihansi - Madeke – Njombe. Hii ni barabara inayounganisha mikoa miwili ambapo tunaweza kufanya biashara kama itatengenezwa mpaka Njombe.

Mheshimiwa Naibu Spika, reli ya mwendo kasi. Tuinashukuru sana Serikali kwa kujenga hii reli ya mwendo kasi ambapo kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri amesema kuanzia Dar es Salaam - Morogoro imefikia asilimia 91, tunashukuru. Tunaomba ujenze uende vizuri kusudi tuweze kuifaidi kama ilivyokusudiwa ambapo wananchi wa Morogoro wataweza kunufaika kwa kufanya biashara na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, hayo ndiyo nilipenda kuchangia, nakushukuru sana. (Makofi)