Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Vincent Paul Mbogo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nkasi Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. VINCENT P. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Napenda kuwapa pongezi Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika nchi hii yapo majimbo yaliyokatwa kutoka Majimbo mengine kutokana na ukubwa wa eneo pamoja na Mikoa. Hii Mikoa ambayo ni michanga inatakiwa hii Wizara ya Uchukuzi iwaone kwa jicho la kipekee kwa sababu miundombinu bado. Ile mikoa ambayo ni mama ikagawiwa ikatoa Majimbo mapya ambayo bado machanga, inatakiwa hii Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi ifanye tathmini, iende ikaangalie barabara ambazo ni main road za Majimbo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hii TARURA au TANROADS imebaki kwenye yale Majimbo mama. Ukichukua sisi watu wa Rukwa, Songwe, Kigoma Nyanda za Juu Kusini, Mtwara, Lindi, Wizara ya Uchukuzi inatakiwa ikae chini iangalie hii Mikoa ambayo kidogo ilikuwa imesahaulika. Nirudi kwenye Jimbo langu; Jimbo langu limekatwa kutoka Jimbo la Nkasi Kaskazini. Mimi ni Mbunge wa Jimbo la Nkasi Kusini. Ukiangalia Jimbo la Nkasi Kusini halina barabara ya TANROADS ina kilometa sita tu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna Kata nne ambazo toka mwezi wa 11 mvua imeanza, sasa hivi ni miezi sita au saba, wala magari hakuna, hakupitiki barabara zina miaka karibu 10, 20, sasa unakuta barabara huku wametenga maintenance; tena barabara ile ya TANROADS kupitia hiyo maintenance wanatengeneza barabara ambayo tayari inapitika. Sisi kule ni lami, hiyo hiyo moram ni lami wakati kuna barabara huko kata nyingine hazipitiki, magari hayaendi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hawa ni wananchi, TANROADS na TARURA wote wanahudumia wananchi. Kwa hiyo, wanatupa wakati mgumu sisi majimbo ambayo yapo pembezoni. Mfano Jimbo la Nkasi Kusini, kuna bandari mbili Wilaya ya Nkasi ambazo zimejengwa kwa fedha nyingi sana za Serikali, lakini miundombinu ya barabara ambazo zinakwenda kwenye bandari hiyo hakuna. Barabara ya kutoka Paramawe kwenda kwenye bandari ya Kipili na barabara ya Kabwe ziwekwe lami ili kuweza kuinua uchumi wa mwambazo mwa Ziwa Tanganyika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ipo barabara ya Ninde – Wampembe; Wampembe ni main feeder road. Wanasema feeder roads hazikidhi vigezo, lakini kila Jimbo lina barabara zake. Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi inatakiwa iwasiliane na sisi Wabunge tunaowakilisha Majimbo tuwaambie barabara zipi ziingizwe TANROADS? Kwa sababu mwanzo ilikuwa ni mfumo, kuunganisha Mkoa na Mkoa, tayari Mikoa mingine imeshaunganishwa. Sasa tuje kwenye barabara za vijijini. TANROADS hata ikiweka barabara za lami, hizi barabara za vijijini ambako ndiko mazao yanazalishwa, hivi barabara za TANROADS itabeba nini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara za vijijini ndiyo viwanda ambako mazao yanazalishwa. Huko barabara ziboreshwe, zikishaboreshwa, hizi main roads ndiyo zitakuwa zina umuhimu zaidi. Kwa sababu tunatengeneza barabara ya lami, lakini mazao hayafiki, ni kazi bure. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, katika mji wangu mdogo wa Kijiji cha Chala TANROADS barabara imepita wamebomolewa nyumba miaka 10 sasa wale wazee hawajapata fidia. Piga mahesabu, mtu wa kijijini amebomolewa nyumba yake ambayo alikuwa anategemea kupata fidia, hajapata fidia na wale wengi ni wazee.

Naomba Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, njooni katika Wilaya ya Nkasi katika Kijiji cha Chala mje mtoe tamko la kuwapa fidia wale watu waliobomolewa nyumba zao. Wengi wanalalamika, wengine wamesha-paralyze, maisha ni magumu. Yote haya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi nawaomba njooni muwape fidia wale watu, muwalipe haki zao, wanalalamika. Sisi Wabunge tunapata shida, tunawajibia nyie majibu ya Wizara ya Ujenzi wakati haupo Wizara ya Ujenzi, inabidi ujibu tu kwa niaba ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, hizi kata tatu ambazo toka mwezi wa 11 magari hayaendi, naomba kwa namna ya pekee Wizara ije ijenge zile barabara. Sasa hivi namkabidhi hizi barabara ziingizwe TANROADS.

Mheshimiwa Naibu Spika, samahani, mhudumu aje amkabidhi barabara Waziri wa Ujenzi.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Mbogo.

MHE. VINCENT P. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)