Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Omari Mohamed Kigua

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilindi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kunipa nafasi niweze kuchangia hoja ya bajeti ya Wizara ya Ujenzi iliyopo mbele yetu. Mimi nitajikita kwenye eneo moja tu nalo ni barabara ambayo inaunganisha mikoa minne ya Tanga, Manyara, Dodoma na Singida. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wewe ni shahidi upo toka Bunge la Kumi na Moja, kila nikisimama hapa hoja yangu ilikuwa ni moja tu kuizungumzia barabara hii. Cha kushangaza Mheshimiwa Waziri kwa makusudi kabisa ameamua kutenga shilingi bilioni 3 mwaka huu ambayo haiwezi kutosha hata kujenga kilometa tatu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii mwaka wa Bunge lililopita au mwaka huu wa fedha tulio nao zilikuwa zimetengwa shilingi bilioni 6 za kitanzania, lakini leo hii nimesimama mbele ya Bunge lako Tukufu barabara hii haijatangazwa kwa maana bado mwezi mmoja, kwa hiyo, matarajio ya barabara hii kujengwa kwa kiwango cha lami yanazidi kupotea. Mimi naomba Mheshimiwa Waziri aniambie barabara hii inatangazwa lini? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini naizungumzia barabara hii? Ni kwa sababu ni barabara ambayo Wabunge takribani sita wameizungumzia; Mbunge wa Singida Kaskazini, Mashariki, Chemba (Dodoma), Kiteto, halikadhalika Mbunge wa Handeni na mimi wa Kilindi tumeizungumzia barabara hii. Kwa nini Mheshimiwa Waziri haoni umuhimu wa barabara hii? Haoni kwamba Watanzania wa kwenye maeneo haya wanahitaji na wao kuwa na afya ya maendeleo ya barabara ya kiwango cha lami? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ndipo bomba la mafuta ambalo nchi ya Tanzania na Uganda linaenda kupita ambapo Mheshimiwa Rais anakwenda kusaini mkataba keshokutwa. Wenzetu wa Uganda tayari miundombinu iko vizuri, sisi wa eneo hili la Tanzania ambapo sehemu kubwa barabara hii inapita haijajengwa kwa kiwango cha lami. Tunataka kuwaambia nini wenzetu ambao wameamua kupitisha bomba hili la mafuta kwenye nchi ya Tanzania? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namuomba sana Mheshimiwa Waziri, ni mgeni kwenye Wizara hii lakini naamini watendaji wake wanafahamu umuhimu wa barabara hii. Hata Mpango wa Maendeleo ulioishia mwaka jana umeitaja barabara hii kwamba ina umuhimu sana kwa ajili ya uchumi wa nchi hii, kwa nini Mheshimiwa Waziri ametuwekea hela ndogo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi huwa sipendi kuzungumza kwa hali ya kukasirika lakini kwenye hili Mheshimiwa Waziri amenikwaza. Ni lazima niseme Wanakilindi, Dodoma, Singida wanahitaji barabara hii ijengwe kwa kiwango cha lami. Tunazungumzia kudumaa kwa uchumi, leo unapokuwa huna barabara ya kiwango cha lami; barabara ambayo haipitiki maana yake uchumi wa wananchi wa maeneo hayo unadumaa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo hili ndilo ambalo linasafirisha kwa kiwango kikubwa mazao kwenda Kenya, Kilimanjaro, Arusha, yote yanapita kwenye njia hii. Sasa iweje Mheshimiwa Waziri usitenge fedha ili barabara hii ijengwe kwa kiwango cha lami? Sitegemei kushika shilingi lakini naomba unipe maelezo ya kutosha ni lini ataitangaza barabara hii kujengwa kwa kiwango cha lami? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara nyingine ambayo napenda kuizungumzia ni ya kanzia Songe - Gairo ambayo Mheshimiwa Mbunge mwenzangu wa Gairo ameizungumzia jana. Waheshimiwa Wabunge mtakumbuka kwamba mwaka juzi ilitokea Daraja la Kiyegeya lilikatika wiki nzima magari yanayoenda Rwanda, Burundi yalikuwa hayapiti. Njia iliyo rahisi ambayo inaweza kuwa ni suluhu wakati barabara hii ikiwa imepata tatizo ni njia hii ya kutoka hapa Dodoma - Kilindi - Tanga ni takribani kilometa mia tatu na zaidi. Barabara hii itasadia kwa sababu tunatarajia kujenga Bandari ya Tanga, ili bandari hiyo iweze kuwa na faida ni lazima tujenge barabara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)