Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Rashid Abdallah Shangazi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mlalo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii niweze kutoa mchango wangu katika Wizara hii ya Ujenzi na Uchukuzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru dada yangu Jacqueline Msongozi kwa kunitunuku cheo ambacho amekitamka muda si mrefu hapa Bungeni. Nami naahidi nitatenda mema kulingana na ukubwa wa cheo alichonipatia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ambayo ndiyo imekipatia chama hiki ushindi ukurasa wa 177 tunayo barabara yetu ambayo imewekwa pale kwa ajili ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kilometa 278 kutoka Same – Mkomazi – Umba Junction ambapo unaipata Tarafa ya Umba kwa Kata za Lunguza, Mng’aro na Mnazi kwenda Mabokweni kwa ndugu Kitandula, kufika Maramba kuunganisha na barabara inayokwenda Horohoro kwenda Mombasa na kurudi Tanga Mjini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ni muhimu sana na ni barabara ya kimkakati. Kwanza iko pembezoni mwa mpaka wa Tanzania na nchi jirani ya Kenya. Lakini pia iko pembezoni kabisa inazunguka hifadhi ya Taifa Mkomazi. Na huku ndiko kule kwenye mazalia pekee ya vifaru ambao tunawatumia katika Taifa letu hili kama kielelezo miongoni mwa vielelezo vya urithi wa Kitaifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ninamuomba sana Waziri mwenye dhamana kwamba wakati tunajadili barabara hii huko nyuma ulikuwa ni Katibu Mkuu wa Wizara unayoiongoza sasa. Sasa unakwenda kusimamia Sera na Chama Cha Mapinduzi kitakuja kukuuliza ni kwa namna gani umezitekeleza sera zinazotokana na Ilani ya Chama chake. Kwa hiyo, tuanomba uweke msisitizo sana katika hili eneo la upembuzi na usanifu wa kina ufanyike kwa haraka ili tangawizi kutoka Mambamlyamba, tangawizi kutoka Mbaramo, na Mnazi ziweze kwenda kwenye masoko ya Mombasa na Tanga Mjini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Mombo – Lushoto kilometa 36 na wewe umeipita lakini ninafaharika pia kusema kwamba na Mheshimiwa Rais wa Awamu hii ya Sita amepita katika barabara hii alivyokuja Mlalo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nikuombe sana Mheshimiwa Waziri, barabara hii ni nyembamba mno na sasa hivi Wilaya ya Lushoto imekuwa na magari mengi sana ya usafirishaji wa mboga mboga na matunda lakini pia na mabasi. Kwa hiyo, barabara hii magari lazima yapishane kwa kusimama kwenye makona ili anayeshuka na anayepanda aweze kupishana vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba sasa, tumeshazungumza mara nyingi kwenye vikao vyetu vya RCC na tunavyopitisha bajeti katika RCC, tunavyopeleka Serikali Kuu, Engineer Mfugale mara zote alikuwa anaziondoa hizi bajeti zetu. Tunaomba sasa zisimamiwe. Barabara hii ni barabara muhimu sana. Watanzania wanajua kwamba ukiondoa Ikulu ya Dar es Salaam kabla ya hii tuliyojenga Chamwino juzi, Ikulu kubwa nyingine tangu wakati wa mkoloni wa Kijerumani ni ile iliyoko Lushoto. Kwa hiyo, barabara hii ni muhimu sana kwa sababu hapa ndipo penye Ikulu kubwa ukiondoa Dar es Saalm kabla ya hii ya Chamwino. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya kutoka Lushoto – Magamba – Mlalo kilometa 33. Hii imekuwa na ahadi nyakati zote lakini pia ikiwa ni ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Awamu hii ya Sita alivyokuja Mlalo alituahidi kwamba barabara hii tutahakikisha kwamba inajengwa kwa kiwango cha lami. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wameshaanza lakini walikuwa wanafanya awamu ya kilometa tano, tano. Mwaka jana yalitokea mafuriko ambapo Naibu Waziri mwenye dhamana hiyo ambaye sasa hivi ni Waziri wa Ulinzi Mheshimiwa Kwandikwa alikuja pale na akaahidi kwamba Mwaka huu wa Fedha angalau ataijenga kwa kiwango cha kilometa 10. Ninaomba sana kwamba bajeti hii kabla haijapita lazima eneo hili mliangalie kwa kina. Tunapozungumza mazao yanayolimwa Lushoto ni mazao yanayoharibika kwa wepesi. Viazi, karoti, matunda na mboga mboga. Hivi viazi ambavyo vinafanya wale wa mjini wanaitwa ‘baby’ japo ni wazee wazima vinatoka Lushoto. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo. Engineer tunakuomba sana kwamba uende ukatenge hii fedha kama ambavyo ilikuwa ni ahadi ya Serikali ya Awamu ya Tano lakini kazi inaendelea. Tunaamini kabisa kwamba Serikali ya Awamu ya Sita itatekeleza.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)