Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Tecla Mohamedi Ungele

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja katika Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi. Awali ya yote, napenda kushukuru Wizara hii, kwa ajili ya ujenzi unaoendelea, sasa hivi mkandarasi yupo pale kwenye barabara ya Nanganga
kwenda Ruangwa. Ila ombi langu naomba ujenzi uende na viwango, lakini pia uende kwa wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, Barabara ya Nachingwea kwenda Liwale, kilometa 130; Nangurukuru – Liwale, kilometa 230; na Kiranjeranje - Namichiga – Ruangwa, kilometa 120. Hizi zote zipo kwenye hatua za upembuzi yakinifu na usanifu wa kina. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ufikie wakati zijengwe kwa lami. Kwa nini naomba hivyo? Barabara hizi kuwa katika kiwango cha lami ni muhimu sana kwa sababu usafirishaji wa watu, lakini usafirishaji pia kwa wagonjwa, lakini usafirishaji wa mazao ya korosho na ufuta ambayo ni mazao ya biashara kwenye Mikoa ya Lindi na Mtwara.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaposhindwa kusafirisha mazao haya Maisha ya watu kule Mkoa wa Lindi yanakuwa duni. Naamini kabisa siku moja ukipata bahati kwenda Liwale utaona kabisa huku ulipo ni kugumu sana, lakini kule kunapatikana korosho na ufuta kiasi kwamba unaweza kukwamua wananchi wa kule.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo ni mfanyabiashara gani atakayehangaika kwenda kununua korosho kule, badala ya kwenda kununua kwenye maeneo ambayo yanapitika. Naomba ufike wakati kuwepo na barabara ya lami kwenda Liwale na kwingineko. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuongelea pia habari ya Uwanja wa Ndege wa Nachingwea. Nimeona kwenye Randama kunataka kuwekwa lami, naomba hilo lifanyike kwa umuhimu wake sana. Uwanja wa Ndege wa Nachingwea una umuhimu sana kwa sababu pale ni center mtu wa Liwale, Ruangwa, Masasi anaweza kusafiri kupitia Nachingwea kuliko kwenda Mtwara kilometa 200 kutoka Masasi. Pia itarahisisha wawekezaji, kule kwetu sasa hivi kuna madini, kuna madini Nditi, kuna madini Ruangwa, ni rahisi kwa wafanyabiashara wawekezaji kupitia kuanzia Nachingwea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia na-share tu experience niliyoipata wakati wa mazishi ya Mzee Mkapa. Ndege nyingi, viongozi wengi walitua katika Uwanja wa Ndege wa Nachingwea, lakini uwanja ule kwa sababu ni wa vumbi adha iliyopatikana wanaifahamu mmojawapo akiwa Mheshimiwa Spika mwenyewe wa Bunge letu, Mheshimiwa Ndugai, anapafahamu Nachingwea. (Makofi)

MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Ungele kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Hamida Abdallah.

T A A R I F A

MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumpa taarifa mzungumzaji anayezungumza hivi sasa kwamba Uwanja wa Ndege wa Wilaya ya Nachingwea, atambue kwamba tumerithi kutoka kwa wakoloni kikiwemo pia Kiwanja cha Lindi Mjini. Kuna umuhimu mkubwa sasa Serikali kuona namna bora ya kuboresha uwanja ule, tena kwa haraka zaidi. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Tecla Ungele.

MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, napokea kwa mikono miwili taarifa hiyo. Uwanja ule pia ni muhimu sana kwa ulinzi na usalama. Nachingwea tuna vikosi vya jeshi, kwa hiyo kunavyokuwa hali yoyote ya kuhitajika usalama ndege pale zitatua na mambo mengine yataendelea. Ufikie wakati Wizara iiangalie Nachingwea na Mikoa ya Lindi na Mtwara kwa ujumla. Ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)