Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Ritta Enespher Kabati

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia. Nianze na kumtanguliza Mwenyezi Mungu katika mchango wangu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwanza na kuwapongeza sana Wizara ya Uchukuzi na Ujenzi. Tumetembelea miradi yao tukiwa na Kamati ya miundombinu, miradi ni mizuri sana, wameitendea haki nchi yetu na wametekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niende moja kwa moja kwenye Mkoa wangu wa Iringa na niende kwenye changamoto kubwa za barabara za kiuchumi zilizopo katika Mkoa wetu wa Iringa. Tunazo barabara ambazo kwa kweli tunaomba Serikali ingezichukua na kuanza kuzifanyia kazi kwa sababu Mkoa wetu wa Iringa unakosa uchumi kwasababu ya barabara ambazo ni mbovu, hazipitiki mwaka mzima. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunayo barabara kwanza inayokwenda katika Mbuga za Wanyama. Hii barabara imeshasemewa na Wabunge karibu wote wa Iringa. Hii barabara inakwenda kwenye Mbuga ya Wanyama ambayo ni ya pili kwa ukubwa kwa Afrika. Tulikuwa tunategemea kama hii barabara ingeisha kwa wakati, basi wananchi wa Iringa wangeweza kujiajiri kupitia hata hii barabara kwa utalii.

Mheshimiwa Naibu Spika, imekuwa inajengwa dakika mbili mbili…

MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Dkt. Ritta Kabati kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Grace Tendega.

MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Napenda kumpa taarifa mzungumzaji anayezungumza kwamba barabara hiyo ya kwenda Ruaha National Park kilometa 104 ni barabara ambayo imeahidiwa na Hayati Rais wa Awamu ya Tatu, Rais wa Awamu ya Nne na Hayati Rais wa Awamu ya Tano.

Mheshimiwa Naibu Spika, hizi kilometa zote kuanzia mwaka 2015 walikuwa katika upembuzi yakinifu na usanifu wa kina toka 2015. Kwa hiyo, ninapoona hivi, nataka kumpa taarifa kwamba hii hali ni mbaya na tumetengewa pesa ya kushika mfuko tu, shilingi milioni 1,500.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Dkt. Ritta Kabati, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naipokea taarifa hiyo kwa sababu kwa kweli lazima Wabunge wote wa Iringa tuisemee kwa sababu inatusaidia wananchi wote wa Iringa. Naomba sasa Mheshimiwa Waziri aone umuhimu, kwa sababu tumeambiwa kwamba itakuwa kwenye package ya World Bank, lakini toka Mheshimiwa Marehemu yupo akiwa Waziri nilishawahi kuuliza swali na mpaka amekuwa Rais; naomba Mheshimwa Waziri hebu tupe kipaumbele kwenye hii barabara ambayo inakwenda kwenye Mbuga za Wanyama.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tunazo barabara nyingine ambazo ni za kiuchumi zinahitaji sasa kupewa kipaumbele. Kuna barabara ile ya Nyololo - Mafinga kilomita 40.4. Hii barabara hata Mbunge wa Mafinga kila siku anaizungumza. Kuna Mgololo, kuna Igoole - Kasanga kilomita 54 lakini kuna Kinyanambo C - Usokami ambayo inakwenda mpaka Kisusa; kuna Kinyanambo A – Sadani – Madibila, hizi barabara na zenyewe zipatiwe kipaumbele kwa sababu ni za kiuchumi ambazo tuna imani kabisa Serikali ikizichukua, basi Iringa itakuwa ni moto kweli kweli.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tunayo barabara nyingine ya Iringa - Idete hii barabara inaunganisha Jimbo la Iringa Mjini - Jimbo la Kilolo na kwa kweli hii barabara inakwenda Idete mpaka Mlangali mpaka inaenda kuunganisha Mlimba. Hii barabara itasaidia kutoboa, kwamba tutakuwa tunafika mpaka Morogoro na itakuwa mbadala kama kutakuwa kuna tatizo kwenye huu mlima wa Kitonga, hatutakuwa na haja ya kupita mlima wa Kitonga, tutatokea Morogoro kuja kufika mpaka Iringa.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuna ile barabara ya Ilula, Mlafu, Mkalanga, Ipalamwa, Kising’a na Kilolo. Hizi barabara zote ni za kiuchumi. Tunaomba kwa kweli Serikali iziangalie ili uchumi uweze kufunguka. Kwa kweli hizi barabara mara nyingi hazipitiki hata Mbunge wa Kilolo juzi nilimsikia anaongelea. Kwa nini sasa kama alivyoshauri Mheshimiwa Kawawa, kuna maeneo korofi ambayo yanajulikana, ni kwa nini sasa yale maeneo korofi Serikali ingekuwa inaangalia kuliko kuanza kutengeneza kilomita labda mbili kutoka Iringa mjini, mbili kutoka Kilolo: ni kwanini sasa wasiangalie tu yale maeneo korofi halafu ndiyo waweke kipaumbele katika kutengeneza ili ziweze kupitika mwaka mzima? Kwa sababu zote zina maeneo korofi, siyo kwamba yote haipitiki, lakini tunachotaka ipitike mwaka mzima ili wananchi waweze kupitisha mazao yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tunayo barabara ile ya mchepuo ya Tumaini, kuchepusha yale magari mazito malori yasipite katikati ya barabara ambayo hata leo Mheshimiwa umesema kwamba ile barabara ya Tanzam malori yanapita mengi sana pale mjini kiasi kwamba kuna wakati itatokea ajali kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mbaya zaidi Iringa pale hatuna sehemu ya kupaki magari, kwa hiyo, magari yakipaki pale barabarani yanaleta shida kwa sababu wafanyabiashara wanashindwa kufanya biashara zao, kwa sababu wakiweka tu magari TANROAD wanafunga yale magari na hapo hapo watu wanalipa karibu shilingi 150,000/= au shilingi 200,000/=, wafanyabiashara wanashindwa kufanya biashara. Sasa Serikali ione umuhimu hizi barabara zetu ziweze kujengwa kwa kiwango cha lami ili zipitike mwaka mzima. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie kuhusu mfuko ambao wanawake huwa wanasaidiwa. Wizara ilikuwa inatoa fedha ili iwasaidie Wakandarasi wanawake kuwajengea uwezo ili tuwe na wakandarasi wengi wanawake. Nampongeza Mheshimiwa Eng. Ulenge ambaye nakumbuka wakati ule alikuwa kwenye hiki kitengo, sasa sijajua; changamoto kubwa ilikuwa ni ufinyu wa bajeti kwamba wanawake wengi hawajengewi uwezo. Sasa naomba hiki kitengo kitengwe fedha nyingi ili wanawake wengi waweze kuwa makandarasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapo hapo nampongeza binti mmoja katika barabara ile ya Tanzanite Bridge, tulikuta mtoto wa kike mdogo kabisa, yeye ndyo anasimamia ile barabara. Ni Engineer; kwa kweli alitu-impress sana sisi Wajumbe wa Kamati ya Miundombinu na tukasema kwamba ipo haja sasa kwa watoto wetu wengi wa kike wajengewe uwezo. Tunakupongeza Engineer Mfugale lakini tunaomba weka wanawake wengi pengine hata ukiondoka waachie hawa akina dada; na unajua akina mama sasa wanaweza na huu ni wakati wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia niendelee kupongeza mradi wa SGR; kwa kweli tumepita katika eneo lote kuanzia hapa mpaka Dar es Salaam na tumekuta asilimia 50 ya wataalam ni vijana wetu. Kwa hiyo, hiki ni kitu kizuri ambapo wanawajengea uwezo na uwe utaratibu mzuri kwamba hata hawa wataalam wa makampuni haya makubwa yakiondoka, vijana wetu wanakuwa wamejengewa uwezo. Kwa hiyo, hili lilitufanya na sisi tukapongeza sana kwamba vijana wengi sasa ma-engineer tutapata kutoka hapa hapa Tanzania na wanajengewa mradi mzuri. Pia kuna fursa nyingi sana kwenye huu mradi ambazo tuliziona. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nipongeze sana pia ujenzi wa uwanja wa ndege uliopo Iringa na tuliambiwa kwamba mwaka huu, huu tutaenda kuzindua ule uwanja wetu na tunaimani sasa tutafanya biashara kupitia huu uwanja, lakini kama haitajengwa ile barabara, bado tutakuwa tunahitaji kwa kweli mfanye kazi nzuri. Vile vile tunapongeza kwamba wananchi wameshalipwa kabisa, hawadai kitu chochote. Kwa hiyo, tunaomba Waziri azingatie hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nizungumzie kuhusu malipo ya Wakandarasi. Wakandarasi wengi bado wanadai. Tulipokuwa kwenye Kikao cha Road Board cha Mkoa wa Iringa, walikuwa wana changamoto nyingi sana kwamba hawalipwi malipo yao, wanadaiwa pesa nyingi kwenye benki, wanadaiwa TRA na walikuwa wanaomba kujengewa uwezo. Tumekuwa na miradi mingi na tulisema kwamba Wakandarasi wa ndani wajengewe uwezo na ikiwezekana pengine hawa Wakandarasi wa nje wakija, pengine zile kazi ndogo ndogo wapatiwe Wakandarasi wetu wa ndani ili pia iwasaidie, pengine wanaweza wakaachiwa vifaa na pia wakapewa uwezo mkubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hapo nakushukuru, naomba Mheshimiwa Waziri, zingatia Mkoa wetu wa Iringa, una changamoto nyingi sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)