Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

Hon. Dr. Godwin Oloyce Mollel

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Siha

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL):
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ni mara ya kwanza kusimama hapa, kwanza nimshukuru Rais wetu mpendwa, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuniamini tena na kuniteua kuendelea kumsaidia katika eneo hili la afya. Vilevile, nimpongeze Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango kwa kuteuliwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa mentoring nzuri anayotufanyia wakishirikiana na Chief Whip, Mheshimiwa Mama Jenista Mhagama ambapo kwa kweli imetusaidia sana kurahisisha shughuli zetu. Pia nikushukuru wewe na Mheshimiwa Spika kwa ushirikiano mzuri ambao mnatupa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nijielekeze kwenye hoja za Waheshimiwa Wabunge. Kabla ya kuanza, niseme tu kwamba sitaweza kuwataja kwa majina wote waliochangia lakini wakati Waziri atakapohitimisha ataonyesha michango yenu na wote waliochangia.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kujibu hoja za Kamati ambapo kimsingi zimefanana na zimegusa yale ambayo vilevile yamechangiwa na Waheshimiwa Wabunge. Hoja ya kwanza ilikuwa ni kuhusu kuongezeka kwa bajeti kwenye eneo la akina mama na watoto ili kupunguza vifo vyao. Katika eneo hilo Wabunge wengi vilevile wamechangia lakini utaona kwa bajeti ya mwaka 2021 ilikuwa ni shilingi bilioni 55 na sasa imeongezeka imefika shilingi bilioni 63. Maana yake kuna ongezeko la bilioni kadhaa hapo ambazo sasa zinaenda kuongeza nguvu kwenye yale maeneo ambayo yanaenda kutuongezea kasi kwenye kupunguza vifo vya akina mama na watoto. Pia utaona vituo vya kufanyia upasuaji kwa maana ya kupasua kutoa mtoto tumboni vimejengwa 304 na tayari vifaa tiba kwa ajili ya upasuaji huo vimeshawekwa kwenye vituo 238.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye eneo hilo hilo Mheshimiwa Dkt. Thea Ntara, amezungumzia upandikizaji wa mimba. Tumelichukua jambo lake ambalo kwa kweli kwenye kutengeneza Bima ya Afya kwa Wote, lakini kwenye ongezeko hili la bajeti na eneo hilo linaenda kuongezwa nalo ili kuchukuliwa uzito ambao Mheshimiwa Mbunge ameuzungumzia.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini Mheshimiwa Dkt. Thea na Mheshimiwa Hawa Chakoma Mchafu walieleza suala la tohara kwa akina mama ambalo nalo hili linaongeza vifo vya akina mama. Waziri wetu anapouliza wanaume mpo huwa anataka tuelekeze nguvu kwenye eneo hilo, tu-address magonjwa yanayotuhusu sisi wanaume na yale ambayo yanaumiza akina mama ambapo sisi tunaweza tukawa solution. Sisi Wabunge tunaotokea maeneo yenye changamoto hiyo kama Umasaini au Ukuriani ambapo hali ni mbaya zaidi tuungane na tutengeneze utaratibu wa pamoja tukaenda kuhamasisha na sisi tukawa watu wa kwanza kulizungumzia hilo kwa uzito unaostahili.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya pili ya Kamati ambayo vilevile Wabunge wengi wameizungumzia ni suala la watoto njiti. Kamati ilizungumzia hasa Muhimbili lakini utaona kuna upanuzi walikuwa na vitanda 66 tu lakini sasa vimeongezwa vimefika 130. Vilevile ukiangalia Muhimbili kwa mwaka akina mama wanajifungulia pale ni 54,000, lakini watoto njiti kati ya hao 54 ni 14,400. Kwa hiyo, hapa ili tuweze kutoka vizuri eneo hili Serikali imeongeza bajeti kutoka shilingi bilioni 37.8 hadi shilingi bilioni 52.2. Pia ongezeko la bajeti ya shilingi bilioni 55 hadi shilingi bilioni 63 nalo linaenda ku-address eneo hili na kutatua tatizo ambalo linasababisha yatokee matatizo ambayo Wabunge na Kamati yetu imeyaainisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo limeibuka ni eneo la Bima ya Afya, wengi wamezungumzia matatizo yalioko kwenye eneo hili. Vilevile Kamati imeshauri suala la ushirikishwaji kwamba kabla ya kuleta Bima ya Afya kwa Wote hapa Bungeni wananchi na wadau mbalimbali washirikishwe. Serikali imechukua ushauri huo na kabla ya Muswada huo kuja hapa Bungeni wadau wote watashirikishwa kuanzia wananchi na watu wengine wowote ambao utawagusa na tunaamini na ninyi kama sehemu muhimu sana mtaingiza input ambazo zitaondoa matatizo mengi yaliyoko kwenye Bima ya Afya iliyopo kwa sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo Kamati imelizungumzia lakini na Waheshimiwa Wabunge pia wamegusia ni kuhusu ushirikishwaji wa sekta binafsi kwenye suala la Bima ya Afya. Sisi tunasema wakati Muswada huu utaletwa Bungeni mtaona umeweka kipengele ambacho kinaruhusu sekta binafsi kushiriki kwenye eneo la bima.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo limekuja ni wateja wa NHIF kukosa huduma lakini likagusiwa suala la CHIF. Tulichokuja kugundua wakati tunasikiliza kwa makini kuna wakati watu wanachanganya wanasema bima akimaanisha CHIF na wakati mwingine anasema bima akimaanisha bima ya afya ile kubwa ambayo inatolewa kwa wafanyakazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunachoweza kusema hapa ni kweli tatizo hilo liko na linasababishwa na upungufu wa madawa kule chini. Ukienda kwenye eneo la CHIF wananchi wamehamasishwa sana kukata zile kadi zao lakini wanapokuwa na kadi zao wanapokwenda kwenye dirisha la dawa wanakuta hamna dawa, kwa hiyo, thamani ya ile kadi aliyoikata inakosa maana. Tumeenda baadhi ya maeneo kwenye wilaya hata wananchi wenye bima hii ya afya kubwa kama walimu hata wafanyakazi wa afya wanapokuwa maeneo remote huko vijijini wakikosa dawa kwenye vituo vyetu na hakuna duka lenye dawa zote kwenye eneo lao inabidi asafiri kilometa nyingi ambapo anatumia shilingi 10,000 kufuata dawa ya shilingi 3,000. Tunachosema wakati tunakuja kwenye Muswada wa Bima ya Afya kwa Wote, lakini wakati tunaelekea kwenye kuboresha upatikanaji wa dawa kwenye vituo vyetu haya matatizo yote yataenda kutatuliwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni eneo la Corona. Watu wengi wamezungumzia Corona na ni namna gani tunafanya. Kwanza, niwaondoe wasiwasi Waheshimiwa Wabunge kwa sababu kwanza kuna Kamati ya Rais ambayo inafanya kazi hiyo na inatoa ushauri mzuri sana kwa Serikali na hilo linaendelea vizuri. Hakuna kitu kipya hapa ambacho kimeanzishwa kwa sababu kama mnakumbuka Mheshimiwa Rais wetu Hayati Dkt. John Pombe Magufuli akiwa Kagera alitushauri Wizara ya Afya msipokee vitu, lakini msifanye vitu bila kufanya upembuzi yakinifu. Hicho ndicho anachoendeleza Rais wetu wa sasa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ameunda Kamati Maalum ambayo itaangalia kwa umakini ni nini kinaingia na nini kinafanyika kwa ajili ya usalama wa watu wetu. Mheshimiwa Rais ameendeleza umakini kwenye hilo hilo na Kamati hiyo inashauri vizuri sana kuhakikisha mambo ambayo tunaenda kufanya ni yale ambayo yataboresha usalama wa watu wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Gwajima amesema jana kwa uchungu mkubwa sana na hasa akitilia hofu kwenye eneo la chanjo. Amezungumzia chanjo za RNA na DNA na ameuliza chanjo zingine ni vitu gani. Ukweli ni kwamba Serikali inajua na ndio maana kuna Kamati Maalum ya wataalam yenye Maprofesa na watu wengine waliobobea na wanajua kwamba kuna hizo chanjo za RNA na DNA. Zile za RNA zinaingia kwenye seli lakini zinasemekana haziendi kwenye nuclears kwa maana ya kugusa DNA. Hata hivyo, watu wetu wanaangalia ukweli huo ni wa kiasi gani kabla sisi hatujasema lolote ndio maana ya timu hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuna zile ambazo ni za DNA ambapo wametumia adenovirus ambao ni virus kutoka kwenye chimpanzee, wanachukua DNA ya virus wa Corona halafu wanachanganya na adenovirus ambayo ni type 5 unakuta katikati kuna virus huyo wa Corona pembeni na pembeni kunakuwepo na DNA ambayo anatokana na adenovirus ndiyo anaingizwa mpaka kwenye nuclear halafu baadaye anatengeneza hizo protini. Ndiyo kazi ya Maprofesa wetu na Rais ameelekeza nguvu zote pale ili wajihakikishie hiyo adenovirus na vitu vingine haina matatizo mengine? Kwa sababu tunajua genetic makeup moja hai-present kitu kimoja, unaweza ukasema unataka kutengeneza protini hizi lakini kumbe hiyo sehemu ilikuwa na uwezo wa kutengeneza protini zingine ambazo zinaweza zikawa na madhara kwa watu wetu. Timu hiyo ndiyo inafanya kazi hiyo kuhakikisha tunajibu maswali haya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuwahakikishie kabisa Serikali ya Tanzania haibishani na dunia au WHO, wala Tanzania haijioni yenyewe ni kisiwa, inakubaliana na mambo yote yanayotokea kisayansi na afya katika dunia. Ubishani hauko kati ya Serikali au Wizara na mtu yeyote, ubishani uko kati ya wanasayansi kuhusu usalama wa kitu tunachoenda kufanya. Kwa hiyo, huo ni ubishani sio kutofautiana, hapana! (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaulizana kisayansi unaposema hiki kinaingia kwenye cell hakikuzi DNA, ukizingatia tunajua kwenye eneo la mimea (Genetic Modified Foods) wakati fulani mapapai yalikuwa modified genetically yakatoa mapapai mwaka wa kwanza baada ya miaka miwili yakatolewa mapapai lakini hayana mbegu. Kwa hiyo, sasa tunajiuliza haya maswali, je, kwa binadamu usalama uko wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, tukubaliane kwamba dunia inakoelekea mwisho wa siku chanjo nyingi baadaye zitakuwa zinatengenezwa na RNA na tunaenda kwenye genetic therapy. Kwa hiyo, hatuwezi kubishana na dunia na sayansi iliyopo, anachofanya Amiri Jeshi wetu Mkuu ni kwamba hata kama tunakubaliana na dunia tuhakikishe tuko salama kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kingine ni kwenye tiba ya asili, Wabunge wengi wamezungumzia eneo hili na tumechukua mawazo yao yote. Mpaka sasa wataalam wa tiba asili na tiba mbadala 27,793 wameshasajiliwa, vituo 1,003 vimesajiliwa, dawa 49 zimesajiliwa lakini mafunzo yamefanyika kwa wataalam wa tiba asili 335.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunataka kwenda mbali zaidi ndiyo maana utaona Serikali yetu imepeleka fedha NIMR kwenye sehemu ya utafiti, hatutaki tu kuishia kusema huu mti unatibu, unaupika huo mti halafu unapata juice yake halafu unakunywa, tunataka watu wa NIMR wakae chini wajue ndani ya huo mti ni molecule gani ziko ndani yake ambazo ndiyo zina sifa ya tiba. Pia hizo molecule ziwe extracted vitu vingine vinatupwa tunaanza kutengeneza syrup na vidonge, huko ndiko tunakotaka kuelekea. Kama mnavyojua quinine inachukuliwa kwenye magome ya miti inaenda nchi zingine mwisho wa siku inatolewa kile kinachotibu inarudi kama sindano tunakuja kutibiwa hapa malaria. Kwa hiyo, tunataka tufike kwenye sayansi kubwa na ndio muelekeo wa Wizara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho ni suala la CCBRT kusajiliwa...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Sekunde 30, kengele imeshagonga.

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL):
Mheshimiwa Naibu Spika, tayari CCBRT imesajiliwa, hivyo, agizo la Kamati limeshatekelezwa. Tunatambua mchango mkubwa unaofanywa na CCBRT na Kamati ilitembelea kwa kweli Mkurugenzi wa CCBRT anafanya kazi kubwa na sisi kama Wizara tutampa ushirikiano mkubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na naunga mkono hoja. (Makofi)