Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Yosepher Ferdinand Komba

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. YOSEPHER F. KOMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Samahani, jina langu ni Yosepher Komba sio Yosephu. Nashukuru kwa kupata nafasi ya kuchangia hotuba ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma kitabu cha Waziri ukiangalia na uhalisia, hakuna kitu. Kwa sababu gani nasema hivyo? Inaonekana Tanzania ya viwanda ipo hewani, haina mizizi. Huu msemo ni msemo wa kisiasa ambao hauna mizizi. Kwa sababu gani nasema hivyo? Wameongea Wabunge waliopita kwamba hakuna uhusiano wa viwanda na mahitaji ya viwanda; hakuna uhalisia wa viwanda na mahitaji ya viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kwa nature ya nchi yetu, tukubali tukatae, kama tunataka viwanda, ni lazima viwe ni agro-industries, viwanda vinavyotegemea kilimo, vinavyotegemea mazao yanayotokana na kilimo, lakini hakuna uhusiano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi wakulima wanahangaika, Mheshimiwa Waziri wa Kilimo aliwahi kusema kwamba jembe tutalikuta makumbusho. Hizo ni lugha za kisiasa. Tumefikia Tanzania kutokutumia jembe! Tumefikia Tanzania ambayo hatutegemei mvua kwa ajili ya kilimo! Viwanda vinahitaji malighafi muda wote, lakini kilimo chetu cha kutumia mvua; isiponyesha hakuna kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri wa Viwanda, pamoja na kukaa na kupanga, kuna utaratibu mzuri na uhusiano mkubwa na sekta nyingine. Tusiongee kama sisi, tuongee kama nchi, tuongee kama Wizara ambazo zinafanya kazi pamoja. Kila mtu asiwe na personal interest kwenye Wizara yake; kila mtu anaongea anavyojisikia. Waziri wa Viwanda wewe huwezi kukamilisha lengo lako kama huna uhusiano mzuri na Waziri wa Kilimo, huna uhusiano mzuri na Waziri wa Ardhi, huna uhusiano mzuri na Waziri wa Miundombinu na sekta nyingine. Hakuna kitu!
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua mahitaji ya viwanda kama malighafi na teknolojia. Tuangalie suala la teknolojia. Ni kwa kiasi gani hivyo viwanda vitakavyojengwa vitaweza kukidhi teknolojia ambayo wananchi wetu wanayo? Tumelenga viwanda vidogo na viwanda vya kati ambavyo kwa asilimia kubwa ni wananchi wa kawaida, wenye elimu ya kawaida. Tumeongea kuhusu VETA, tumeongea kuhusu maeneo mbalimbali ambayo yangeweza kutoa ujuzi kwa wananchi wetu; hilo halijafanyika. Mheshimiwa Waziri anatuambia Tanzania ya Viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitegemea miaka mitano hii ungetumia nguvu nyingi sana kutengeneza miundombinu ya viwanda, lakini siyo viwanda kwa maana ya majengo, tunadanganyana. Tungetengeneza miundombinu ambayo inge-facilitate viwanda. Tunasema uwekezaji, tunasema Serikali haijengi viwanda, tunawaita wawekezaji. Tujiulize, miaka yote wawekezaji walikuwa wapi kiasi kwamba Mheshimiwa Waziri amefanya lipi kubwa la kumvutia mwekezaji katika kipindi ambacho yeye amekuwa Waziri? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mazingira ni yale yale ambayo miaka 20 au 30 iliyopita wawekezaji walishindwa kuja kuwekeza. Hata yale maeneo ambayo viwanda tulivibinafsisha, vingi vimekufa. Mimi natokea Mkoa wa Tanga, kuna viwanda vingi. Tulikuwa na viwanda vya chuma, viwanda vya blanketi, viwanda vya matunda, viwanda vya mafuta, viwanda vya kila aina, vimekufa. Tanga ilikuwa ni Mkoa wa Viwanda miaka ya 1980, lakini sasa hivi Tanga imekuwa ni magofu. Viwanda vingi vilivyokuwepo wameiba mashine, wameiba kila kitu, wengine wamehamisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa tunategemea zao la mkonge, tulikuwa tuna mashamba kwa ajili ya kuzalisha mbegu za mkonge, yamekufa. Tulikuwa na estate nyingi sana, zimekufa. Wawekezaji wameshindwa, wamerudi kwenye nchi zao, yale maeneo wananchi hawayatumii kwa kilimo, yamebakia kuwa mapori.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasema tunataka viwanda, viwanda vipi ambavyo haviangalii malighafi? Tunajua bei ya katani katika Soko la Dunia; tunajua bei ya mkonge, tunajua thamani yake kwenye Soko la Dunia; lakini tunataka viwanda ambavyo tutawadanganya wananchi kwa maneno, kwenye uhalisia hakuna kitu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tujiulize, Mheshimiwa Waziri anapotuambia nchi ya viwanda, anataka ku-compete na nani? Amejiandaa ku-compete na nani? Anaposema Tanzania ya viwanda, ajue kwenye dunia hii kuna nchi kibao ambazo zipo katika hiyo level ya viwanda. Amejiandaaje ku-compete nao? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesoma kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri, ukurasa wa 91, kuna hili Shirika la Viwango (TBS), naomba ninukuu baadhi ya maneno aliyoyaandika hapa. TBS imekuwa ikishirikiana na Jeshi la Polisi na Taasisi nyingine za Serikali kama TFDA, TRA FCC, GSLA na EWURA katika kufanya ukaguzi wa kushtukiza sokoni ili kuhakikisha kuwa bidhaa dhaifu zilizo chini ya kiwango na ambazo siyo salama kwa afya au matumizi ya mlaji zinaondolewa sokoni.
Kwa hiyo, sasa TBS wanaenda kuvizia sokoni. Wanaenda na Polisi, TRA na FDA kuvizia sokoni. Wakati zinaingia, hakuna utaratibu wa kuhakikisha kwamba haziingii. Hii kauli inajidhihirisha, hata Mheshimiwa Rais juzi amesema.
Wafanyabiashara wanavizia sukari ambazo zinaelekea kuharibika, wanazinunua, wanaziingiza Tanzania. Viongozi mnalijua hilo, mnangoja ziingie, zikifika sokoni, mnaenda kuzitafuta. Wangapi watakuwa wameathirika na hizo bidhaa? Tunajua bidhaa zinazotoka nje ni za hali ya chini; zinakuwa na bei ya chini kutokana na ubora pia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Watanzania wanazalisha bidhaa ambazo ni bora, lakini inakuja kwenye bei kutokana na hali halisi ya Mtanzania hawezi kununua kitu cha sh. 10,000/= wakati kuna kitu hicho hicho kwa sh. 5,000/=. Kwa hiyo, Watanzania wengi kutokana na hali ya uchumi, hatuangalii ubora, tunaangalia uwingi. Kwa hiyo, hakuna namna kama hamjaweka mkakakati mzuri, kuhakikisha kwamba wazalishaji wa ndani wanalindwa kuanzia kwenye utaratibu wao wa uzalishaji. Wanatumia gharama nyingi sana, mwisho wa siku sokoni lazima bidhaa yake iwe na bei ghali. Mtanzania anashindwa kuinunua, anangoja inayotoka nchi za nje. Tunalalamika, tunataka viwanda, tuna nchi ya viwanda, naona hiki ni kitu ambacho hakiwezekani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipindi nasoma shule ya msingi, kulikuwa kuna kitu tunaita mazingaombwe. Anakuja mtu, tunachangia shilingi hamsini hamsini, tunaingia, tunaonyeshwa namna ya kutengeneza shilingi elfu kumi. Sasa naona mazingaombwe yale ambayo nilikuwa naamini ni utoto kudanganywa, yanaendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamwomba Mheshimiwa Waziri, tunajua ipo kwenye ilani, ipo kwenye maneno ya viongozi wako; Mheshimiwa Rais na viongozi wengine kwamba Tanzania ya Viwanda. Mkoa wa Tanga tuliahidiwa Tanga ya Viwanda mwaka 2010 na aliyekuwa Rais wa Awamu ile ya Nne, sasa leo hii ukisema Tanzania ya Viwanda, watu wa Tanga hawatakuelewa, kwa sababu walishasikia Tanga ya Viwanda, haikuwezekana. Tanzania ya Viwanda ni ndoto! Kwa miaka hii, kwa utawala huu ambao hauna uhusiano katika Taasisi zake, ambao kila mtu anataka kujinufaisha yeye kutengeneza jina lake! Ukiwa Waziri, cheo cha kisiasa kiweke pembeni. Ukiwa Waziri, jaribu kusikiliza wataalam. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo ni kwamba Waziri anakuwa mkuu kwenye Wizara yake kushinda mtaalam, kushinda mtu yeyote hata kama hana utaalam wowote, kwa sababu tu ya cheo. Hiyo imekuwa ikiathiri sana mapendekezo na nia ambayo tunayo Watanzania. Naomba Mawaziri, Mwanasiasa yeyote anayejiamini na mwenye nia njema na nchi yake, lengo lake hata kama hana ujuzi wowote ni kuhakikisha wenye ujuzi wanafikia matamanio yao. Mwanasiasa lazima ahakikishe kwamba binadamu hafi; lazima ahakikishe mkulima anapata mazao mazuri kwa sababu ndiyo lengo la mkulima; ahakikishe kwamba engineer anatengeneza barabara nzuri; siyo kuwa na amri kwenye kila kitu ambacho hatuna utaalam nacho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nizungumzie suala la masoko. Tunajua wakulima wetu wanavyolima kwa shida na hilo jembe la mkono ambalo tumeambiwa litakuwa historia, sijui ni mwaka gani. Tangu mwaka 1961 tunapata uhuru lilikuwepo, hatujui limepungua kiasi gani, lakini tunaambiwa na Waziri wa Kilimo litakuwa historia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Watanzania kwa kilimo cha jembe la mkono wamejitahidi sana hapo walipofikia. Masoko yamekuwa ni shida! Masoko yamekuwa ni tatizo! Sijui ni kwa namna gani na kwa kiasi gani mnawaandalia masoko wakulima hawa ili hayo mazingira ya viwanda yawe rahisi kwao? Kwa sababu gani nasema hivyo? Masoko yanaendana na miundombinu, masoko yanaendana na bei, yanaendana na gharama za uzalishaji,…
MWENYEKITI: Mheshimiwa Yosepher muda wako umemalizika.
MHE. YOSEPHER F. KOMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naunga mkono hoja ya hotuba ya Upinzani.