Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

Hon. Anton Albert Mwantona

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Rungwe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

MHE. ANTON A. MWANTONA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kupata nafasi kuweza kuongea neno kidogo kwenye Wizara hii ya Maji. Pia namshukuru Mungu kwa kunipa uhai hadi siku ya leo napochangia katika Wizara hii. Nampongeza sana Waziri wa Maji mdogo wangu Mheshimiwa Aweso, Naibu Waziri wa Maji Mheshimiwa Maryprisca Mahundi, Katibu Mkuu pamoja na watendaji wote wa Wizara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa, nimepitia bajeti ya Wizara ya Maji kwa kweli nimeona bajeti hii ni ndogo kwa Wizara hii. Mwaka huu wa fedha Wizara imepata shilingi bilioni 705 kwenye bajeti lakini kwa bahati mbaya sana fedha ambazo zimekuja kwenye Wizara ni bilioni 346 ambazo ni asilimia 53, ni fedha ndogo sana kwa Wizara. Tuombe Serikali ihakikishe kwamba fedha zinazopangwa kwenye bajeti zinapelekwa kama inavyotakiwa ili kumaliza kiu ya Watanzania kuhusu maji safi na salama kwa wananchi wake. Vinginevyo kila mwaka tutakuwa tunakuja kupiga kelele hapa kwamba bajeti ni ndogo, fedha haziendi na kwa sababu ya ufinyu wa bajeti ndio maana Wizara inashindwa kutekeleza malengo yake kama inavyotakiwa. Chonde chonde Serikali tunaomba tupeleke fedha kama inavyotakiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia ninamshukuru Rais wetu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan alisema ataboresha Mfuko wa Maji nchini. Nimuombe Rais ahakikishe kwamba Mfuko wa Maji unapatiwa fedha ya kutosha ili changamoto za maji ziweze kuondoka hapa kwetu nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, nije Jimboni kwangu, namshukuru Waziri wa Maji pamoja na Naibu Waziri walipanga ziara kuja katika Jimbo la Rungwe wakatembelea miradi mbalimbali ikiwepo Mji wa Tukuyu, tukawaeleza matatizo yetu pale, mpaka leo local radio za pale Rungwe zimemnukuu Naibu Waziri akiahidi kwamba tatizo la maji Tukuyu litakwisha, kila siku ndio salamu za asubuhi pale Rungwe. Nashukuru Waziri Mheshimiwa Jumaa Aweso pamoja na Naibu Waziri baada ya kusikia kilio cha wana Rungwe, Mji wa Tukuyu juzi juzi wamewapelekea shilingi milioni 500.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia alitembelea Mradi wa Rukata, Kata ya Kinyala, juzi juzi pia kawapelekea shilingi milioni 100 angalau mradi uanze wananchi wapate moyo. Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu Waziri ninawashukuru sana Mungu awatie nguvu katika utendaji kazi wenu ili miradi hii ya wananchi iweze kwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi mwingine ambao napenda kuishukuru Wizara ni wa Masoko. Kuna mradi upo pale na kuna vijiji vingi vimenufaika. Kwenye bajeti hii kuna fedha kwenda kurekebisha madhaifu yalikuwepo kwenye mradi huu. Vijiji vitakavyofaidika nii zaidi ya 16 ambayo ni Ikama, Itagata, Lufumbi, Lupando, Bujesi, Lwifwa, Isabula, Mmbaka, Busisya, Burongwe, Ngaseke, Igembe, Mtandabara, Nsyasya, Mperwangwasi pamoja na Nsaga. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli hivi vijiji vilikuwa na matatizo makubwa, chanzo cha maji kimetokea katika eneo lao lakini maji ya kutosheleza yalikuwa hayapatikani katika vijiji hivyo. Wizara imetenga zaidi ya shilingi milioni 500 kwenda kurekebisha miundombinu ili wananchi katika maeneo hayo waweze kupata maji ya uhakika, hiyo peke yake nashukuru sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia Wizara imetenga fedha kwa ajili ya kupeleka maji kwa awamu ya pili katika mradi huu, vijiji 15 vinanufaika. Kuna Kijiji cha Mpumburi ambacho ni chanzo cha maji pia pale kinakwenda kupata maji. Vijiji vingine vya Segera, Mpombo, Masukuru, Ijiga, Mpakani, Byebe, Njugiro, Kiroba, Kikore, Matwebe, Kiambambembe, Lubanda, Katunduru na Ilima vinakwenda kupata maji. Hiyo ni shukrani ya pekee sana kwa Waziri lakini pia wa Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna vijiji vilikuwa kwenye bajeti ya mwaka huu ambayo inaisha mwezi wa sita, sijaviona kwenye bajeti inayofuata. Naomba chonde chonde tuna siku kadhaa kumaliza mwaka huu, mwaka unakwisha mwezi wa sita; kuna vijiji kama Champandapanda, Kata ya Kiwila mwaka huu unakwisha na ilitengewa shilingi milioni 205, kuna Kijiji cha Ikuti, Lyenje vilitengewa shilingi milioni 126, ni fedha ndogo, naomba Wizara kama kutakuwa na uwezekano kabla ya mwaka huu wa fedha haujaisha tuwapelekee hawa watu fedha ili miradi yao iweze kutekelezwa kwa sababu changamoto ni kubwa.

NAIBU SPIKA: Kengele imeshagongwa Mheshimiwa.

MHE. ANTON A. MWANTONA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano pale Lyenje pale Ikuti kuna kituo cha afya kimejengwa lakini kwa bahati mbaya sana hawana maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, naomba kuwasilisha. (Makofi)