Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

Hon. Ester Amos Bulaya

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia ya Wizara hii muhimu ambayo inatesa sana wanawake kwa kutembea umbali mrefu kutafuta maji na Mheshimiwa Rais amesema hilo jambo la maji ni kitu chake cha moyoni kwa sababu anajua wanawake wa nchi hii wanateseka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze kuzungumzia tatizo la upotevu wa maji. Tatizo hili limekuwa sugu tangu nimeingia katika Bunge hili mwaka 2010 tunazungumzia changamoto ya upotevu wa maji kwenye mamlaka zetu. Nitoe mfano kwenye mamlaka 23, mamlaka 21bado zina changamoto ya upotevu wa maji kupita kiasi. Kwa miaka miwili tu kwa mfano mwaka wa fedha wa 2019/ 2020 kutokana na upotevu wa maji Serikali imepata hasara ya billioni 177. Mwaka 2081/2019 kutokana na tatizo hili la upotevu wa maji Serikali ilipata hasara ya bilioni 155. Sasa kwenye miaka miwili tumepoteza bilioni 332 ambazo Waheshimiwa Wabunge tutafakari, ingetengeneza miradi mingapi katika majimbo yetu, au tungechimba visima vingapi katika majimbo yetu na kumtua mwanamke ndoo kichwani.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine tunapoyasema haya, tunataka tatizo hili liishe na tunajuaje kuna upotevu wa maji? Ni baada ya kukokotoa maji yanayozalishwa na yanayomfikia mteja. Tatizo hili sugu kwa nini tunakubali kupoteza pesa za walipa kodi, kwa uzembe, kwa kutokuwa na ufanisi wa kuhakikisha miundombinu ya maji inakuwa salama na kuziba mianya ya watu kujiunganishia maji kiholela.

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati haya yanaendelea, kwa mujibu wa Kanuni ya 6 ya mwaka 2013 ya Usambazaji Maji, Serikali inapaswa kupeleka ruzuku kwenye mamlaka ambazo zimefuzu, ziko Daraja A, B na C. Kwa mwaka 2019, Serikali imeshindwa kupeleka bilioni 856 katika mamlaka 10. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hizi mamlaka zitawezaje kujiendesha? Zinatakiwa zijiendeshe, zinatakiwa ziendelee na ukarabati wa miundombinu ya maji, na hizi halmashauri, ikiwepo na kwako Mbeya. Sasa haya mambo hatuwezi kuyavumilia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi kweli huku tunashindwa kuminya, huku tunashindwa kuhakikisha tunatengeneza miundombinu mizuri ya maji, huku hatupeleki pesa kwenye mamlaka ziweze kujiendesha na kukarabati hii miundombinu ya maji halafu tunataka kumtua ndoo mwanamke kichwani. Kwa miujiza? Kwa mambo haya?

Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na tatizo la kutokukusanya madeni kwenye mamlaka ya maji; bilioni 148 ziko nje! Lakini mbaya zaidi, Serikali inadaiwa bilioni 64 katika mamlaka zake. Lipeni madeni ili hii Wizara iweze kuweka mipango yake mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, madeni mengine, bilioni 83 ni kwenye viwanda na wateja wa kawaida. Tuna changamoto nyingi za miundombinu, tuna changamoto za kuhakikisha tunamaliza miradi kwa wakati, lakini bado Wizara hii imekuwa na changamoto kubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo linguine Serikali kutolipa wakandarasi kwa wakati na kufanya riba ziongezeke; kwa mfano kuna ujenzi wa jengo la Wizara ambalo linagharimu bilioni 44. Lakini wameacha kulipa kwa wakati, riba imetoka kuanzia milioni 99 mpaka bilioni 4.9; shame! Hizi pesa mngekuwa mnalipa kwa wakati zingeenda kutengeneza miradi mingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa mtambo wa kusambaza maji Mradi wa Ruvu Chini, ambao Serikali inadaiwa bilioni 17 na Mchina, wameshindwa kulipa riba ni bilioni 3.9. Hivi kama mngelipa kwa wakati hizi pesa zingine zingeenda kukamilisha miradi mingine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano kuna miradi sita Dar es Salaam, Moshi na Arusha imeshindwa kuendelea kwa miaka mitatu mfululizo kwasababu tu Serikali imeshindwa kupeleka bilioni mbili. Na huo mradi mpaka sasa hivi wamelipa bilioni 16, mradi una gharama ya bilioni 18. Mnalipa riba huku kwa uzembe wa kutokupeleka pesa kwa wakati, mnaacha miradi mingine ambayo inatakiwa ikamilike kwa wakati inashindwa kukamilika. Haya mambo ndiyo yanafanya Wizara hii ishindwe kutimiza wajibu wake na kuhakikisha mwanamke anatuliwa ndoo kichwani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge, hebu tujiulize hizi tathmini ambazo tunapewa kwamba upatikanaji maji vijijini maybe ni asilimia sabini na. nilikuwa nimepitia ripoti; EWURA inasema Mkuranga, Kisarawe, Chalinze, upatikanaji wa maji ni asilimia 96, lakini CAG amekwenda kuchunguza, upatikanaji wa maji ni asilimia 53.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, takwimu tunazopewa na Wizara na changamoto ya kutokamilika miradi na upotevu wa maji, inawezekana kabisa upatikanaji wa maji katika nchi yetu haufiki hata asilimia 50. Kwa hiyo, haya ni mambo ya msingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa moja ya miradi iliyokaa muda mrefu ni pamoja na Mradi wa Maji wa Bunda unaotoka Ziwa Victoria. Biashara ya chujio tumeisikia sana, biashara ya usambazaji wa mabomba kwenye kata saba tumezisikia sana. Sasa tunataka kata 14 za Mji wa Bunda zipate maji; hilo ndilo nimetaka kulisisitiza. Zibeni mianya ya upotevu maji, pesa zinapotea.

NAIBU SPIKA: Ahsante sana.

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, sasa wewe unasema wakikuzingua utawazingua, na sisi Wabunge humu ukituzingua maji hayatoki katika maeneo yetu na sisi tutakuzingua kabla Rais hajakuzingua. Ahsante sana.