Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

Hon. Issa Jumanne Mtemvu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibamba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nichangie...

NAIBU SPIKA: Samahani Mheshimiwa Issa Mtemvu kabla hujaanza kuchangia, Wajumbe wa Kamati ya Uongozi, saa tano na nusu Mheshimiwa Spika anawaita kwa ajili ya kikao hapa lounge.

Mheshimiwa Issa Mtemvu, endelea.

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Naibu Spika nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nichangie katika Wizara ya Maji, Wizara ambayo ni muhimu sana kwa wananchi wa Jimbo la Kibamba. Nitumie nafasi sana kuwapongeza viongozi wenye dhamana ya Wizara hii ndugu yangu Mheshimiwa Jumaa Aweso, Waziri, lakini pia dada yangu Maryprisca kwa kufanya kazi vizuri pamoja na Katibu Mkuu Dkt. Sanga. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimekuwa nikisema mara nyingi hapa Dar es Salaam ina mafanikio makubwa sana kwenye suala la maji na taarifa zetu zote Mheshimiwa Waziri Mkuu amewahi kutuambia hapa, Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa mara nyingi sana amekuwa akisema takwimu zaidi ya asilimia 92 Dar es Salaam ina maji. Nawapongeza sana, lakini nimekuwa nikisema hizo asilimia zilizobakia Dar es Salaam ni za Jimbo Kibamba. Kibamba kuna shida kubwa ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, miradi imeenda mingi sana ipo pale Kibamba imeenda kwa kaka yangu Mheshimiwa Jafo kule, mradi mzuri kabisa zaidi ya asilimia 97 umetoka Luguruni Kibamba. Umeenda kwa kaka yangu Profesa Kitila Alexander Mkumbo, akinamama wametuliwa ndoo kichwani kule Ubungo, lakini wananchi wa Jimbo la Kibamba wanaendelea kuteseka.

Mheshimiwa Naibu Spika, miradi iliyopo pale ambayo inaendelea nishukuru sana upo mradi mkubwa sana unatoka changanyikeni unaenda Bagamoyo lakini lipo tanki kubwa la lita milioni 5.6, liko pale Tegeta A, hili likitengenezwa vizuri, linaenda vizuri, likikamilika na usambazaji wa mabomba Kata nzima ya Goba wanaenda kupata maji salama na yenye kutosheleza.

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi tunaoulilia sasa, ambao Hayati alipita mchakato ulikuwa tayari unaendelea, lakini akasema mfanye kwa dharura ni tanki kubwa pale Mshikamano, Kata ya Mbezi, mpaka sasa halijaanza, Mheshimiwa Waziri akija naomba nifahamu vizuri ni lini tanki
hili pale Mshikamano lisaidie wananchi wote wa Makabe, wananchi wa Msakuzi, wananchi wa Mpiji Magoe, wote waweze kupata maji safi, salama na yenye kutosheleza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye taarifa ya Mheshimiwa Waziri niliisikiliza, mmoja wa mradi uliotamkwa ni pale Kata ya Kwembe Kinyazi A, unazungumza milioni 33, mradi ule umekamilika mwezi Februari, ni ukweli hakuna kitu kama hicho. Bahati nimemwomba Mheshimiwa Waziri kwenda baada ya bajeti yake kupitishwa na amekubali na barua ipo mezani kwake, tutaenda tutafika pale ataona watu wanaendelea kunywa maji ya chumvi, lakini maji ya njano, maji mabaya kabisa ndani ya Kata ya Kwembe au eneo la Kinyazi A.

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme juu ya changamoto kubwa katika Kata ya Kibamba maji yapo changamoto ni usambaji wa mabomba. Ipo miradi midogo midogo zaidi ya kumi na mbili toka mwaka 2020 mwezi Machi, bajeti iliyopita tena ya juzi yake ya mwaka 2019/2020 mpaka leo katika mabomba haya maji hayatoki.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri aliwahi kufika Wilaya ya Ubungo, upande wa Jimbo la Ubungo, kwa bahati tulikuwa wote. Nafurahi sana kaka yangu Rwemeja pale anafanya kazi vema, lakini katika hili wanisaidie kutoa mabomba, yasambazwe kwa wananchi hawa niliotamka katika kata nyingi ili waweze kupata maji salama na yenye kutosheleza.

Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo kama Kibwegere, Kwembe, Msingwa, Malamba Mawili, Ukombozi na Msumi na kule Kibesa mbele ya Mpiji Magoe kwenda Mabwepande, kule kunataka tusambaze mabomba tu il mtu aweze kupata.

Mheshimiwa Naibu Spika, najua bado dakika moja au na nusu, nimwombe sasa Mheshimiwa Waziri, katutengea bilioni 25, usambaji wa maji katika maeneo ambayo hakuna maji Jijini Dar es Salaam. Naomba hizi hela alizozitenga Waziri, hajasema zinakuja Kibamba ameweka kwa ujumla wake, asilimia 92 tayari Dar es Salaam, hakuna maji Kibamba, tupeleke Kibamba ili wananchi wapate maji salama na nyenye kutosheleza.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, nikushukuru kwa kunipa nafasi, naunga mkono hoja ya Mheshimiwa Waziri na Wizara ya Maji kwa asilimia zinazotosha kwa sababu wananchi wanaenda kupata maji salama na ya kutosheleza. Ahsante sana. (Makofi)