Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

Hon. Khadija Hassan Aboud

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwanza naunga mkono hoja hii. Lakini pia naipongeza Wizara ya Maji, Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na Watendaji wote katika juhudi zao za kila siku za kuhakikisha wananchi wa Tanzania wanapata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuliona hili na dhamira yake ya dhati ya kumtua mwanamama ndoo kichwani. Ambapo ameahidi kwamba, atauongezea nguvu mfuko wa maji kwa kutafuta vyanzo vipya vya kuongeza nguvu katika mfuko huu wa maji. Napongeza sana juhudi za Wizara kwa kukamilisha utekelezaji wa miradi 422 ya maji mijini na vijijini, pamoja na kupunguza gharama za uwekezaji kwenye miundombinu ya maji. Naomba juhudi hizo ziendelee ili kuokoa pesa nyingi za Serikali kwa ajili ya uwekezaji wa miradi ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wizara ina upungufu mkubwa wa wataalam wa maji, naishauri Serikali ione umuhimu wa kuajiri hawa wataalam wa maji, ili kwenda kusimamia miradi ya maji huko mijini na vijijini. Ikiwa pamoja na kuwatumia wataalam wetu waliobobea ambao kwa sasa wamestaafu, angalau wawatumie kwa kipindi kifupi cha mwaka au miaka miwili ili kuongeza nguvu katika kuwekeza huduma hii ya maji kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, maji ni muhimu kwa wananchi kwa maana ya binadamu, maji yanahitajika kwa wanyama, maji yanahitajika pia kwa miti na mimea yetu. Kwa hivyo, suala la maji ni suala la msingi na ninaipongeza Serikali kwa juhudi hizo kwa kuona tunafikia ile asilimia tuliyojiwekea kwa upatikanaji wa maji safi na salama mijini na vijijini. Lakini pia, napongeza juhudi za Serikali kwa maana ya Wizara ya Maji wameliona hilo sasa, kwa kuhifadhi au kuvuna maji ya mvua. Hili ni jambo jema ambalo litasaidia sasa kupunguza zile changamoto za maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama tunavyojua maji ya mvua ni maji mazuri na yenye rutuba kwa kilimo. Kwa hivyo, tukihifadhi na kuvuna maji haya ya mvua yatakwenda kusaidia sana kwenye sekta hii ya uwekezaji wa kilimo lakini pia kwa matumizi mengine ya binadamu. Uvunaji wa maji ya mvua ni jambo la msingi kwa kuzingatia kwamba tunapoteza maji mengi na yanaharibu miundombinu yetu. Kwa hivyo, tukiyavuna na kuyahifadhi kwa kuyatumia kwa mahitaji yetu yote kwa viumbe sisi binadamu na wanyama, na kwa matumizi mengine ya kijamii yakiwemo mambo kama mfano, wakivuna maji ya mvua watu wa magereji wanaotumia maji mengi sana katika ukoshaji wa magari. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hivyo tungeweka msisitizo pia kwa hawa wanaotumia mambo ya ukoshaji magari wakavuna maji ya mvua ili kusaidia kupunguza yale maji safi na salama kutumia kwa mambo ya magari na mambo mengine. Kuna madeni makubwa sana kwenye Wizara hii ya Maji, ni vyema sasa Wizara ya Fedha ikawakata moja kwa moja wale wadaiwa sugu maana kuna wadaiwa na wadaiwa sugu. Sasa wale wadaiwa sugu wale Serikali ikate moja kwa moja ili fedha zile zikasaidie kuhakikisha kwamba, miundombinu ya maji inakarabatiwa, tunadhibiti upotevu mkubwa wa maji ili sisi tunaopata maji ambao hatulipi basi zile fedha zisaidie kwenda kutengeneza miundombinu na wale wenzetu ambao hawapati maji waweze kupata maji tuwalipie hizi fedha Serikali ikate moja kwa moja hizi fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na pia, hawa wadaiwa sugu naiomba Wizara prepaid meter zianze huko kwao kwasababu, wameonesha kwamba wao hawalipi kwa hivyo zile prepaid meter zikaanze kwa wadaiwa sugu wa maji, ili tuweze kupata fedha zetu za maji tuwekeze zaidi kwa wananchi wengine wapate maji. Nimalizie kwa DDCA - Wakala wa Uchimbaji Visima na Mabwawa. Naomba Serikali iwekeze pale kwasababu, sasa miundombinu waliyonayo ya vifaa ni hafifu haviwezi kuchimba kina kirefu cha maji. Visima virefu vya maji inahitaji tuagize mitambo na wataalam kutoka nje waje watusaidie. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tukiwekeza pale tukisomesha wataalam wetu tukawa nao sisi wenyewe na tukawekeza mitambo ya kutosha pale ya kuhimili kuchimba kina kirefu cha maji, tunaweza tukaokoa pesa nyingi za Serikali na kupunguza urasimu wa utendaji katika kufanya kazi hii ya DDCA. Naomba Uwakala huu uongezewe nguvu na uwezo na kuwekewa wataalam wazalendo ili tukafanye kazi ya kutafuta maji, kwenye ardhi kuna maji ya kutosha.. (Makofi)

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Spika, nakushukuru naunga mkono hoja. (Makofi)