Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

Hon. Husna Juma Sekiboko

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa fursa na mimi kuchangia kwenye Wizara yetu hii maalum kabisa ambayo tunatarajia inakwenda kumkomboa mwanamke wa Kitanzania kwenye jambo hili la shida ya maji.

Mheshimiwa Spika, kabla ya kutoa mchango wangu nimpongeze sana kaka yangu Mheshiwa Jumaa Aweso kwa kazi kubwa ambayo ameifanya kwenye Wizara hii, hakika nchi yetu sasa imekuwa na matumaini makubwa ya kutatua kero ya maji, pamoja na Naibu wake dada yangu kipenzi kabisa Engineer Mahundi. Uwezo wao na namna ambavyo wanaongoza hiyo Wizara inatusaidia sana kuwasemea akinamama kwenye jambo hili la maji.

Mheshimiwa Spika, kipekee kabisa nimpongeze sana dada yangu Engineer Upendo Omari Lugongo, Mhandisi Mkuu wa Maji, Mkoa wa Tanga. Anafanya kazi kubwa sana, lakini kazi hii anayoifanya itakuwa na tija kama mambo haya mawili ambayo natamani kuyazungumza yatafanyiwa kazi katika Mkoa wa Tanga.

Mheshimiwa Spika, jambo la kwanza, shida ya maji ni kubwa, pamoja na jitihada kubwa ambazo zinafanywa na Serikali lakini huwa tunapeleka fedha nyingi kwenye kuanzisha miradi mipya lakini tumekuwa tukiiacha miradi ya zamani bila ukarabati. Ukiangalia kwenye Idara zingine kwa mfano Idara ya barabara tukishajenga barabara tunakuwa na ruzuku ya ukarabati wa barabara. Tukijenga vituo vya afya tunakuwa na bajeti kwa ajili ya ukarabati wa vituo vya afya vivyo hivyo kwenye mashule na maeneo mengine.

Mheshimiwa Spika, lakini fedha ambazo tunatenga kwa ajili ya ukarabati wa miradi ya maji ni ndogo sana, muda mwingine tunaziachia Jumuiya za Watumia Maji ambazo hazina uwezo. Hizi Jumuiya za Watumia Maji ambazo kwa utaratibu wa sasa tunajenga miradi kwa kutumia fedha nyingi, lakini tunawakabidhi wenzetu waweze kuisimamia na kutumia charges ndogo ndogo ambazo wanachangia wakati wa kuchota maji waweze kukarabati hiyo miradi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni utaratibu ambao kwa kweli unaweza kutukwamisha katika kutatua tatizo hili la maji katika nchi yetu kwa sababu hizo jumuiya kwanza hazina elimu, hazijaelimishwa vya kutosha, lakini jumuiya hizo zina-charge hao tunaowaita Watanzania wanyonge, Watanzania wa hali ya chini, ukienda huko vijijini hao wanaoenda kuchota maji kwa shilingi 200, mia 300 mpaka 500 ndiyo wale wale ambao tumeona kwamba hawawezi kulipa ada tunawapa elimu bure. Ndiyo wale wale ambao tunawapelekea ruzuku ya TASAF kwa kushindwa kukimu miasha yao. Sasa bado tumewawekea huu mzigo wa kuwa wanachangishana fedha kupitia kwenye visima vya maji, lakini baadaye wakusanye kwa ajili ya kukarabati jambo ambalo tungelifanya sisi kama Serikali, lingekuwa na mantiki kubwa sana katika kutengeneza uendelevu, (sustainability) ya miradi ya maji vijiji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niishauri sana Serikali ione namna gani sasa inaweka kusudi la dhati katika kukarabati miradi hii hasa visima vile vya vijijini kabisa, kuwapunguzia huu mzigo akina mama wa vijijini ambao wanashindwa kuoga, wanashindwa kunywa maji, wanashindwa kulea watoto wao vizuri. Utakutana nao barabarani wamebeba madumu ya maji kama watoto mgongoni, wanahemea maji mbali kwa kushindwa kulipia gharama za maji muda mwingine lakini kukosa maji maeneo ya Jirani. (Makofi)


Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo nilitamani kulizungumza ni ukarabati wa mabwawa. Kule Tanga hususani kwenye Wilaya ya Mkinga kuna bwawa pale Duga, kule Handeni kuna mabwawa ya Mandera, Masomanga na Gendagenda. Kule Kilindi kuna bwawa la Kwamaligwa, Kwadudu na Mkuyu, mabwawa haya ni ya siku nyingi yamejengwa takribani kipindi cha uongozi wa Mwalimu Nyerere. Ni mabwawa ambayo yalikuwa na uwezo wa kutoa maji kwenye jamii nyingi, lakini hayajawahi kukarabatiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo ambalo sasa wanashindwa kupata maji lakini haya ukijumlisha na ile miradi mikubwa kama Potwe kule Muheza, Maramba kule Mkinga, Magina na Kwesine kule Lushoto ikikarabatiwa hii miradi ya siku nyingi ambayo ilikuwa inazalisha maji na kuhudumia kwa watu wengi zaidi inaweza kutatua kwa sehemu kubwa sana tatizo hili la maji. Lakini kwa sababu, muda ni mfupi sana nimeipitia hiyo hotuba ya Mheshimiwa Waziri inshallah Rais ajaye labda, lakini kuna hii miradi ya payment for result P4R. mikoa nane haijaguswa na hii miradi ikiwemo Mkoa wa Tanga. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini Mkoa wa Tanga ina vijiji 846 lakini kati ya hivyo ni 400 tu vina mtandao wa maji na angalau watu wanapata maji safi na salama. Zaidi ya vijiji 400 kwenye Mkoa wa Tanga hawapati maji kabisa vijiji hivyo havina miundombinu ya maji kabisa, hawapati maji safi na salama. Sasa kwa nini tusipeleke huu mradi niiombe Wizara ya Maji na Serikali ione umuhimu wa kupeleka hii miradi ya P4R kwenye Mkoa wa Tanga. Lakini mwisho kabisa gharama ya maji ni kubwa sana, maeneo mengine tunaona mvua zikinyesha watu wananyanyua mikono juu wanamshukuru Mungu na hapo hawachukui tena maji ya RUWASA wala ya DAWASA wanatumia maji ya mvua kwasababu ya kutafuta ahueni.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja nashukuru sana. (Makofi)