Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

Hon. Esther Lukago Midimu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia Wizara ya Maji. Kwanza kabisa nampongeza Waziri kwa hotuba yake nzuri iliyosheheni matumaini ya Watanzania. Mheshimiwa Aweso unafanya kazi nzuri pamoja na Naibu wako.

Mheshimiwa Spika, nampongeza Rais wangu, Mheshimiwa Mama Samia Suluhu kwa kuchaguliwa kwa kishindo kuwa Mwenyekiti wa Taifa wa Chama. Haijawahi kutokea mwanamke kuwa Mwenyekiti wa Taifa. Wanawake tunajivunia hilo, Mheshimiwa Rais ametuheshimisha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais ana dhamira ya dhati ya kumtua mama ndoo kichwani, ni mwanamke mwenzetu, shida zote zitaisha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba sasa niongelee mradi wa Ziwa Victoria. Toka mwaka 2010 tunaongelea mradi huu, tunaomba maji kutoka Ziwa Victoria, hatimaye Serikali yetu sikivu ikatusikia, ikakubali kutuvutia maji kutoka Ziwa Victoria kuleta Mkoa Simiyu. Nilishawahi kusimama mwaka juzi kuuliza swali hapa kuhusu mradi huo utaanza lini.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri wa kipindi kile alinipa majibu mazuri akasema mradi huo utaanza na Wilaya tatu; utaanza na Busega, Bariadi na Itilima, lakini hadi sasa hakuna kitu kinachoendelea. Baadaye wakati wa kampeni, Mheshimiwa Hayati Dkt. John Pombe Magufuli wakati anafanya kampeni zake alisema Mkoa wa Simiyu tayari wameshatenga shilingi bilioni 800 kwa ajili ya kuvuta maji kuleta wapi Mkoa wa Simiyu kutoka ziwa Victoria, lakini hadi sasa hakuna kinachoendelea. Naiomba Serikali yangu Sikivu, kwa vile inasema hizo fedha imetupa, itoe sasa mradi uendelee. Mradi huo utainua uchumi wa Simiyu na Mikoa ambayo ni ya pembezoni mwa Simiyu. Kwa sababu wanawake wa Mkoa wa Simiyu ni wakulima wazuri, wachapakazi, tutalima kilimo cha umwagiliaji, tutalima mboga mboga na matunda, tutauza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sera ya Serikali ni kuwa na uwanja wa ndege kila Mkoa. Simiyu tumetenga tayari eneo la uwanja wa ndege, nina imani utajengwa na ndege zitatua, tutasafirishva mboga mboga kwenda nje. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika maji waathirika wakubwa ni akina mama. wanaume muda mwingi nyie mmepumzika, mmelala tu, sisi tunakwenda kutafuta maji, tukirudi ndani tunapika. Ninaomba Serikali ibaini sasa maeneo ambayo yana shida na hali mbaya kabisa ya maji, ichimbe visima vidogo vidogo kwa sababu tunaoathirika ni sisi wanawake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niendelee kuishukuru Serikali yangu na kuipongeza kwa mradi mkubwa wa maji wa Lamadi ambao umejengwa kwa shilingi bilioni 12.8 na unahudumia vijiji vitatu; Kijiji cha Lamadi, Kijiji cha Lukungu na Kijiji cha Mwabayanda. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo, bado kuna vijiji vingine vina uhitaji zaidi, hawana maji kabisa; Kijiji cha Mirambi na Mwanhari. Wilaya ya Meatu ina shida kubwa sana, haina maji kabisa na wanawake wa kule wanahangaika sana. Muda mwingi wanaupoteza kutafuta maji kuliko kufanya kazi za maendeleo. Halafu jiografia ya Meatu ni mbaya sana, maeneo yale yana ukame sana, hata kama maji yakichimbwa kule chini unakutana na magadi, unakutana na maji ambayo hayafai katika matumizi ya binadamu. Naiomba Serikali ifanye utaratibu kila mwaka itenge fedha iwe inachimba hata mabwawa mawili mawili wapate maji watu wa Meatu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna bwawa la Mwanjoro huko huko Meatu. Kipindi kile Mheshimiwa Rais wa sasa wa Awamu ya Sita alikuwa Makamu wa Rais, alikwenda kulizindua. Sasa hivi limejaa tope. Naiomba Serikali yangu itoe fedha hilo bwawa likarabatiwe, kwa sababu linahudumia vijiji vitano ili wanawake waweze kupata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, upatikanaji wa maji Mkoa wa Simiyu asilimia 60.3 Wilaya ya Meatu, asilimia 62 Wilaya ya Maswa, asilimia 69.2 Wilaya ya Itilima na asilimia 50.8 Wilaya ya Busega. Upatikanaji wa maji bado upo chini, tunaomba Serikali ituletee fedha ili tuchimbe visima virefu viweze kusambaza maji. Bahati nzuri kwa Simiyu tuna Meneja mwana mama mchapakazi, anachapa kazi, ni mtu mzuri, yeye anasubiri fedha tu aweze kusambaza maji kila kona. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi, ubarikiwe sana. (Makofi)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Esther Lukago Midimu.

MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Kicheko/Makofi)