Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

Hon. Nashon William Bidyanguze

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigoma Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpongeze Waziri wa Maji. Waziri wa Maji huyu ametokea kwenye nafasi ya Naibu Waziri, inaonekana Mheshimiwa Rais alimwona pale alipokuwa akitenda kazi kwenye nafasi yake ya Unaibu Waziri ndipo akaona ampandishe daraja awe Waziri kamili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nimpongeze Meneja wa RUWASA pale kwenye Jimbo langu la Kigoma Kusini, pale Uvinza, naye ni mpya, lakini ameanza kazi vizuri. Ameanza kwa kutembelea kata zote na kuhakikisha anaona vijiji ambavyo havina maji aweze kuona namna ambavyo anawapatia maji wananchi wale.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niungane na Wabunge wenzangu waliojaribu kusema namna ambavyo Wizara inaweza ikatengeneza miradi ya maji ya kitaifa. Jimbo langu liko pembezoni mwa Ziwa Tanganyika. Jimbo langu lina kata 16, lakini ni kata tatu tu ndio zina maji, lakini vijiji viko 61, vijiji ambavyo vina maji havifiki 10. Pia ni jambo la kushangaza sana kwamba, maji wananchi wanayaona, lakini uwezo wa kuyachukua hawana.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kama ambavyo Serikali kupitia Wizara ya Maji imeweka utaratibu wa kuchukua maji katika Ziwa Viktoria na kuyafikisha katika mikoa mbalimbali na hapa Dodoma yanakuja. Kwa nini Mheshimiwa Waziri asione namna ya kubuni mpango wa kuanzisha mradi mkubwa katika eneo lile kwa kutumia maji yale ya Ziwa Tanganyika ambayo mradi ule ungeenda mpaka kwenye Wilaya ya Nkasi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi katika jimbo letu, kama nilivyotaja, tuko karibu sana na maji, lakini iko miradi ambayo ilipelekwa ambayo mpaka sasa haijakamilika. Kwa mfano, Lukoma; uko mradi mmoja mzuri sana wa maji ulianzishwa mwaka 2010. Mpaka leo tunavyozungumza mradi ule ulikuwa na asilimia 80, lakini mpaka sasa haujaanza. Kijiji cha Lukoma watu wanasubiri maji hawayaoni, lakini fedha ya Serikali ilikwenda kwa hiyo, unaweza ukaona kwamba, miradi hii ambayo Wizara inaianzisha wakati mwingine ni tatizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri anatakiwa awe na mpango madhubuti, mpango ambao utampelekea kuonesha kwamba, amefanya maamuzi magumu. Miradi ambayo ni ya pesa nyingi, lakini itakuwa na matokeo mazuri kuliko vimiradi vidogovidogo ambavyo vinakuwa na pesa kidogokidogo na mwisho wa siku miradi ile haikamiliki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, fikiria Kata hiyo ya Lukoma ambayo ina mradi wa maji huu wa mwaka 2010 ambao mpaka sasa haujakamilika na kata ile ina vijiji saba. Hivyo vijiji vyote havina maji, ila nashukuru tu kwamba, Mgambazi ndio kijiji kimoja ambacho katika vijiji saba ambacho kina maji. Pia Mwakizega uko mradi ambao ulianzishwa mwaka 2020, lakini mpaka sasa mradi huo haujaanza. Mabomba yapo, lakini tatizo ni viunganishi kama Waheshimiwa Wabunge wenzangu walivyozungumza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mlela pia upo mradi wa maji, kisima kilishachimbwa, lakini mradi ule wananchi wanaendelea kusubiri hawapati maji. Kandaga vile vile ndio kijiji ambacho mimi natokea, kijiji hicho kilichimbiwa visima, lakini bahati mbaya kumbe visima vile vilivyochimbwa inaonekana upembuzi yakinifu haukufanywa vizuri, vile visima havina maji, lakini fedha ya Serikali ilitumika katika eneo lile. Kwa hiyo, leo tunasubiri labda Mradi ule wa Mlela ambao tayari umeshachimbwa kisima na wataalam wale wanasema inawezekana yale maji wakayasogeza pale Kandaga ambapo ni vijiji vinafuatana.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunasubiri hiyo neema kama itapatikana na naomba nimwombe Mheshimiwa Waziri kwa kweli katika eneo hili, tukiweza kumpitishia bajeti yake basi aweze kuniona, atembelee katika jimbo langu aone hiki kilio ninachokitoa kwa uhalisia kule vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile pana mradi pale Ilagala. Ule Mradi wa Ilagala bahati mbaya sana ni mradi ambao haukushirikisha wananchi. Walichimba kisima na bahati mbaya sana kile kisima kina maji ya chumvi wakati Ilagala kuna Mto Malagarasi, mto ambao una maji baridi. Sasa wananchi wanajiuliza, Wizara ya Maji kwa nini watuletee maji ya chumvi wakati sisi tuna maji baridi?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mradi ule ni kama vile hauwezi kufanya kazi kwa sababu, wananchi hawataki kabisa yale maji. Kwa hiyo, tukienda kule Mheshimiwa Waziri nina imani atapata uchungu mkubwa kuona namna ambavyo anaweza kubadilisha ili tuweze kuwatengenezea pump ili wapate maji yale ya Mto Malagarasi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la mwambao mwa Ziwa Tanganyika lina kata nane, lakini katika kata zile ndio kata ambazo kwa kweli, kimsingi mvua zinaponyesha wananchi wanapata shida ya tatizo lile la kipindupindu, kwa sababu ziwa liko bondeni wananchi wanaishi juu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, wakati mwingine kutokana na mazingira yalivyo lazima walazimike kuchota maji ya ziwani ili waweze kujikimu na yale maji yanakuwa yameshachafuka kutokana na vinyesi ambavyo, maana vyoo vipo, lakini vyoo wakati mwingine vikifurika maana yake lazima choo kile kiende kule ziwani. Kwa hiyo, kuondoa tatizo la kipindupindu katika Kata za Sunuka, Sigunga, Helembe, Buhingu ni kuhakikisha kwamba tunapata miradi ya maji mikubwa ambayo inatokana na maji ya kutoka Ziwa Tanganyika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, fikiria Sigunga ina vijiji vitatu lakini hakuna hata kijiji kimoja kina mradi wa maji. Hiyo Sunuka ambayo nimeitaja ina vijiji nane, lakini kuna kijiji kimoja tu kina ndio mradi wa maji.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Kengele ya pili imeshagonga Mheshimiwa.

MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba nirudie kumwomba Mheshimiwa Waziri, tuongozane kwenda Jimboni, ili niweze kwenda kumwonesha matatizo yaliyoko jimboni kule.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)