Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Haji Amour Haji

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makunduchi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. HAJI AMOUR HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa ruhusa yako nami nichangie Katika Wizara ya Elimu. Kwanza namshukuru Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuweza kuondosha ile tozo ya asilimia sita katika mkopo wa elimu ya juu.

La pili nije katika mchanganuo wa hoja zetu ambazo kila mmoja katika kusimama kwetu hapa kwa mujibu wa Wabunge wengi wanacholilia ni vitu viwili. Kwanza, wanalilia mfumo wa elimu ambao tulokuwa nao na la pili wengi wao wanazungumzia suala la curriculum.

Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani nije kwa upande wa kuangalia mfumo wa elimu. Mfumo wa elimu kwa upande wa Tanzania, mie nimetokea upande wa Tanzania Zanzibar. Kule Zanzibar zamani tulikuwa tumeanzia ile base, tulikuwa tuna kitu ambacho tunakiita uzalishaji mali, ambapo kwa zamani uzalishaji mali maana yake ilikuwa imeanzia kuanzia standard one hadi standard seven, maana yake tunajifunza masuala ya elimu ya vitendo kama kulima pamoja kufuma na mambo mengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na kukua kwa leo, kwa sababu tuna uleo, maana yake tunasema kwamba tuna elimu ya ujasiriamali. Sasa katika vitu viwili hivyo maana yake nilikuwa najiuliza huu uzalishaji mali na ujasiriamali sijui tofauti yake ipo wapi. Kikubwa zaidi nijaribu kuzungumza kwamba, ningekuwa naulizwa, ningesema kwamba, tungekuwa tunaanza na ile elimu ya uzalishaji mali kuanzia ile standard one au kuanzia darasa la chini huku maana yake kwenda juu ili kumkuza mtoto katika misingi ya kujua ujuzi. Bila ya hivyo, kwa kusema kwamba tusubiri tu wanafunzi watakaomaliza katika elimu za juu au kuanzia kumaliza darasa la saba wajiunge katika mafunzo ya ufundi maana yake pale tutakuwa kuna kitu tunakipoteza.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ushauri wangu kwa Wizara ya Elimu ni kwamba haya mafunzo ya ufundi hasa ambayo kwa huku tunaita ni mafunzo ya ufundi, tungeanzia huku kwenye standard one tukaanza na huo uzalishaji mali. Tukizungumzia suala la uzalishaji mali maana yake yule mwanafunzi unaanza kumjenga namna ya kuanza kujua kama ni kulima anajua nini maana ya kulima; kama ni kufuma, anaanza kujua nini maana ya kufuma. Sasa tunapokuja katika hatua ya juu, hapo ndio tunakuja katika suala la entrepreneurship, suala la ujasiriamali.

Mheshimiwa Naibu Spika, ningeomba kwa upande wa Wizara ya Elimu, suala hilo lazima wajaribu kuliangalia, mbali na mitaala yetu ambayo tunayo hapa Tanzania, kwa sababu kila mmoja maana yake analaumu mtaala, lakini suala la mitaala hili linakuja kutokana na mfumo wetu na namna ambavyo watendaji wetu wanavyohisi, kwa sababu Tanzania tuna mfumo ule wa kwamba kila mmoja anapokwenda katika nchi fulani kwenda kusoma anarudi na mfumo wake. Anayekwenda China akirudi akija Wizara ya Elimu atakuja na mfumo wa Kichina; anayekwenda Japani atakuja na mfumo wa Kijapani; na anayekwenda Marekani atakuja na mfumo wa Kimarekani.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa bado sisi wenyewe hatujajijua hasa tunachokitaka ni kipi katika mfumo, kama Watanzania ukilinganisha na tamaduni zetu pamoja na silka zetu. Bila kujua hilo maana yake itakuwa ni vigumu sana na kila siku tutasema mtaala sio au tunakokwenda siko, lakini kitu muhimu zaidi, tunapotengeneza hii mitaala yetu, kitu cha msingi tujaribu kuangalia tamaduni zetu zinatuelekeza wapi na mazingira yetu yanatuelekeza wapi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikizungumzia suala la mazingira, Tanzania ina mikoa mingi, kila eneo lina vitu vyake katika masuala ya uzalishaji. Kuna mikoa ambayo inazalisha sana katika kilimo, kuna mikoa ni madini, kuna mikoa ni mambo mengine, maana yake kila mkoa una sifa ya aina yake. Nadhani kwamba tungejaribu kuangalia kuangalia elimu kwa kutazama hasa mifumo ya mikoa pamoja na uzalishaji wao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pale zamani wakati ule ambapo sisi tupo kwa sababu kwa upande wa kule Zanzibar unapoanza primary school, unapokwenda sekondari kulikuwa kuna ile kwamba mtu anapokuja kufauli kutoka darasa la sita au darasa la nane, kwa sababu kulikuwa kuna darasa la nane kwenda la tisa kulikuwa kuna fani maalum ambayo mwanafunzi yule anatoka pale kuelekea katika ile fani. Kwa mfano tuwe na wanafunzi ambao watakwenda kusomea kilimo tangu sekondari, tuwe na wanafunzi…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. HAJI AMOUR HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)