Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Athumani Almas Maige

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tabora Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kuniruhusu nichangie Wizara hii ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kwa kweli lazima nikiri kwamba Wizara hii imefanya kazi kubwa sana jimboni kwangu na nchi nzima. Mimi kwangu nawapongeza sana kwa kunijengea shule za upili wa juu. Tulipoingia madarakani hatukuwa na hata shule moja ya upili wa juu yaani high school tunazo mbili sasa. Pia wananijengea VETA na hii itasaidia sana kupeleka fedha vijijini kwani mafunzo yatakayopatikana watafanya kazi vijijini. Vilevile tumepata fedha za maboma na tumejenga nyumba za walimu na madarasa na tumepata madawati. Hapa pia nilishurukuru Bunge letu, Bunge lilitupa madawati ambayo yamekwenda kuwekwa kwenye shule zangu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo siongelei ufundi kwa sababu Mheshimiwa Manyanya amenigusa sana kwamba ilikuwa hujuma kuua shule za ufundi. Hili lichukuliwe kama ni sababu kubwa sana ya kulegalega kwa elimu ya ufundi hapa nchini, hujuma hii ilitupata sisi Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo nitaongelea suala la lugha ya kufundishia na VETA kuwa chini ya Wizara ya Elimu na Sayansi. Kiswahili mmekigusa kidogo mimi safari hii naomba Serikali ianzishe shule ya mfano itakayoanza kufundisha kwa Kiswahili kuanzia darasa la kwanza mpaka chuo kikuu. Wazo hili lilikuwepo sijui kwa nini Serikali haikuanzisha shule ya mfano. Ichukue shule yoyote ambayo watoto wapo darasa saba waendelee form one Kiswahili, shule moja tu tuone matokeo yake. Maana tunabishana wataalam hawataki kusoma tafiti ambazo zipo pale TATAC na BAKITA. Watu wote waliofanya utafiti kwa miaka 40 wamesema Kiswahili ni lugha mama Tanzania ifundishwe, bado watu hawataki kutofautisha kati ya elimu, maarifa na lugha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali na Mheshimiwa Waziri akija hapa na nitazuia shilingi atuambie tatizo gani lilizuia Serikali kuanzisha shule ya itakayotumia Kiswahili kama lugha ya kufundishia. Tunaandikia mate na wino upo, si tuanzishe tu shule leo iende mpaka form four, form five Kiswahili. Vitabu vyote TATAC vipo, wameshaandaa kitabu cha kwanza mpaka cha pili, wakianzisha shule hii wale watamalizia kidato cha nne na cha tano na watakuwa mbele hivyo wale wataalam wa TATAC na BAKITA kutafsiri kwa lugha la Kiswahili vitabu vyote vya kufundishia. Nawaombe sana tujaribu mfano huo kama itashindikana ndipo wazo la lugha litakufa kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nafikiri watu wana mawazo ya nyuma kwamba Kiingereza au Kifaransa ndiyo elimu. Mimi nashauri tuanzishe shule itakayotumia Kiswahili kama lugha ya kufundishia darasa la kwanza mpaka chuo kikuu. Sasa hivi Chuma chetu Marehemu Magufuli, Rais wetu, alisema tu historia la kwanza mpaka chuo kikuu Kiswahili, asubuhi tumefanya hivyo mbona hawakukataa? Leo tunafundisha historia darasa la kwanza mpaka chuo kikuu kwa kutumia Kiswahili mbona imewezekana, kwa nini masomo mengine ishindikane, tena masomo sasa yamepungua yamebakia machache imebaki historia na kiswahili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Bunge lako linaongea Kiswahili, Serikali inatumia Kiswahili, Mahakama inatumia Kiswahili, mnawachanganya watu, hao waliosoma Kiingereza wanatumiaje Kiswahili huku Mahamani au Serikalini, kumekuwa na mambo ambayo hayaeleweki. Naomba sana Kiswahili kipewe umuhimu na mimi hili kama Mheshimiwa Rais anasikia aliingilie kati, kabisa kabisa. Nashauri hili liamuliwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye suala la VETA. Waajiri wanachangia Mfuko wa Elimu ya Ujuzi kupitia tozo ya SDL kwa asilimia 4 lakini fedha zile haziendi VETA zote. Sababu kubwa ilijulikana siku za nyuma kwamba fedha zilikuwa hazitoshi ndipo Mheshimiwa Kikwete akahamishia VETA Wizara ya Elimu ili ipatikane fedha ya kwenda Bodi ya Mikopo na ndivyo ilivyo sasa. Sasa hivi mantiki hiyo haipo kwa sababu fedha zote zinakwenda Akaunti ya Pamoja ya Hazina. Kwa hiyo, ile mantiki kwamba fedha za SDL ziende Wizara ya Elimu haipo tena. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, VETA maana yake ni kazi ndiyo maana sisi waajiri tunachangia. Tunachangia fedha zinapatikana lakini sasa VETA badala ya kusimamiwa na Wizara ya Kazi na Ajira ndani ya Ofisi ya Waziri Mkuu, chini ya Mheshimiwa Mama Jenista Mhagama sasa anasimamia Waziri wa Elimu, ni vitu tofauti. Sisi huku tunashangaa sana hii Serikali vipi? Mbona sasa ajira inasimamiwa na Wizara ya Elimu na wakati Wizara ya Ajira ipo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nawaombeni sana, waajiri huku wanashangaa. Hatukatai kuchangia na tunawashukuru sana Serikali tulikuwa tunachangia asilimia 6 mpaka imefika asilimia nne tunaomba sasa hii VETA irudi kwa Mheshimiwa Jenista Mhagama ambaye ndiye anayesimamia ajira na kazi na ndiyo kuna mikataba ya kazi, tunataka wafanyakazi wapate ujuzi. Sasa tunasimamiwa na Wizara ya Elimu siyo shule ile; kile ni Chuo cha Ufundi Stadi ya wafanyakazi na ndiyo maana sehemu kubwa ya fedha yake inatoka kwa sisi waajiri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kuniruhusu na mchango huo naomba safari hii ufanyiwe kazi. Naunga mkono hoja. (Makofi)