Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Husna Juma Sekiboko

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Spika, awali ya yote niitumie fursa hii kuipongeza Wizara ya Elimu na Serikali kwa ujumla, kwa maamuzi yaliyofanyika kupitia sera ya elimu ya kuanzisha shule za kata, ambazo zinasaidia wanafunzi wengi hasa wale wanaotoka kwenye familia za masikini. Uamuzi huu ulikuwa uamuzi mzuri sana kwa Taifa letu hili linaloendelea kwasababu, imetoa fursa ya watoto wengi wanaoishi kwenye mazingira ya chini kupata fursa hiyo ya kupata elimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimejaribu kupitia takwimu takribani kwa sasa tuna shule za kata 3,900, shule hizi zimejengwa kwa nguvu za wananchi na kumaliziwa na Serikali kupitia Wizara yetu ya Elimu na Wizara ya TAMISEMI. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hoja yangu leo katika shule hizi ninajaribu kutizama ni namna gani tunaweza tukafanya maboresho na kuzalisha watoto wenye elimu inayostahili, kwa maana ya elimu bora kutoka kwenye shule zetu hizi. Ni mwalimu by professional, shule ili iitwe shule lazima iwe na walimu na wanafunzi lakini lazima iwe na madarasa, maktaba na maabara. Kwa sababu, tunaamini katika elimu, elimu anayopata mwanafunzi darasani ya kufundishwa na mwalimu ni asilimia 25 peke yake zaidi ya asilimia 75 ya ujuzi anaoupata mwanafunzi, inatokana na mazingira yanayomzunguka. Kwa maana anajifunza kutoka kwenye maabara, lakini anajifunza kutoka kwenye maktaba ili kuweza kupata ubunifu na stadi ambazo anastahili kuzipata. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwenye shule zetu hizi zaidi ya 3,900 tunakosa hayo mazingira ya kumuwezesha mwanafunzi kujifunza, kwa maana shule zetu hazina maabara na shule zetu hazina maktaba. Mazingira ya kujifunzia ni magumu sasa nini kifanyike? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe sana Serikali kupitia Wizara ya Elimu na pengine kushirikiana na TAMISEMI ambayo ndio wasimamizi wa hizi shule za kata. Kuangalia sasa namna gani Serikali inaweza kuweka malengo ya makusudi, kukamilisha maabara katika maeneo mengine ambayo zimeshaanza kujengwa. Lakini kuweka maktaba kwa ajili ya kuwasaidia watoto hawa wa wakulima na wanyonge wa Tanzania, waweze kupata elimu sawasawa na watoto wa matajiri na wale wanaoishi kwenye miji mikubwa ambayo ina shule nyingi ambazo zina hali nzuri ya kutolea elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilipenda kulizungumza hili kabla sijakuja kwenye hoja yangu ambayo nilitamani kuizungumza zaidi leo kuhusiana na specialization. Namna ya kupanga michepuo kwenye shule zetu na hii sio tu kwa zile shule maalum zinazosimamiwa moja kwa moja na Wizara ya Elimu, lakini vile vile, kwenye hizi shule zetu za kata. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kipindi ambacho sisi tulikuwa shuleni tunasoma tulikuwa tunaona, ukienda kwenye shule fulani utakuta kuna mchepuo wa kilimo, ukienda shule nyingine utakuta kuna mchepuo wa ufundi, unaenda shule nyingine ni mchepuo wa sanaa. Haikuwekwa bahati mbaya ilikuwa inawafundisha wanafunzi kujiendeleza kutengeneza ujuzi na maarifa tangu wakiwa katika ngazi za chini kabisa za kupata elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na ukiwa mwalimu ukifundisha kidato cha kwanza mtoto anasoma pale kwa takribani mwaka mmoja, akienda kidato cha pili tayari umeshamfahamu kwamba, huyo mtoto anaweza kwenda kwenye mchepuo gani? Na unamshauri kwenda ku- specialize kupunguza mzigo wa masomo ambao mwisho wa siku hauwezi kumsaidia. Mtoto anapangiwa anakwenda kwenye combination za sayansi, mwingine anakwenda kwenye combination za sanaa, mwingine za biashara. Na mwisho wa siku ndio tunakuja tunapata ma-accountants, tunapata hawa madaktari, tunapata na watu wa namna hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niiombe na niishauri sana Serikali hoja hii pia ameizungumzia vizuri Mheshimiwa Charles Mwijage, hatuna sababu ya kuwafundisha watoto wetu general education, tutengeneze specifically tunataka mtoto ahitimu akiwa ameiva kwenye eneo gani mahsusi katika elimu anayopata. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la specialization kwenye elimu ni suala muhimu sana. Hivi tunalalamika leo tunataka kubadilisha mfumo wa elimu, tunataka kubadilisha mtaala wa elimu, kwa mashaka tu kwamba pengine huu mtaala haumsaidii mtoto kuweza kukabiliana na mazingira anayoyaishi. Lakini kiukweli mtaala hauwezi kutusaidia, kama hatujaamua kumuandaa huyu mtoto kwenye mazingira yake tangu mwanzo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi tulikuwa tunasema jana, Mheshimiwa mmoja alizungumza humu ndani, kuna dhambi gani mmasai kuingia darasani na kumfundisha mtoto namna ya kufuga ng’ombe? Kuna dhambi gani kumuita mvuvi, baharia akaingia darasani akamfundisha mtoto namna nzuri ya kuvua samaki? Hata wakati tunasoma walimu walikuwa wanakaa pembeni anamuita traffic anafundisha watoto namna ya kuvuka barabara, ni elimu. Elimu tusiiwekee mipaka kiasi cha kuwafanya wanafunzi wetu kukariri, tutengeneze mazingira ambayo mtoto anaweza kujifunza kadri mazingira yake yanavyomruhusu na kutengeneza ujuzi wa kuweza kuendeleza maisha yake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya jambo hilo nizungumze kidogo kuhusiana na soko la elimu. Tumeingia kwenye mazingira ambayo elimu sasa inakwenda kuwa ni biashara. Tuna shule za private na tuna shule za Serikali. Shule za private Mheshimiwa Waziri pia uje ulitizame vizuri, inawezekana kuna namna fulani inatengenezwa siasa ya kuwaaminisha umma kwamba, shule za private ndio zinatoa elimu nzuri kuliko shule za Serikali. Lakini ukweli ni kwamba, shule za Serikali zina mazingira mazuri, zina walimu wa kutosha, zina maeneo mazuri ya watoto kujifunzia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, ukitaka kumfundisha mtoto masuala ya kilimo shule ya kata ya msingi labda, Kwemakame ina eneo zuri la kuweza ku-practice kilimo kuliko shule ambayo inapatikana pale Dar es Salaam. Kwa hiyo, tuna haja pia ya kuuza na kutoa namna gani shule zetu zina mazingira mazuri ukilinganisha na hizi za private, mwisho wa siku tutakuwa… (Makofi)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa kengele ya pili imegonga.

MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru naunga mkono hoja. (Makofi)