Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Charles John Mwijage

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muleba Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. CHARLES J. P. MWIJAGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipatia fursa ya kuchangia sekta ya elimu, ambayo ni muhimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, nitumie fursa hii kuipongeza Serikali kwa kufanya uamuzi ulioondoa kero katika sekta ya elimu, kero zilizokuwa zinazuia wananchi au baadhi ya wananchi kupeleka watoto shule, hasa hili suala la karo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hizo pongezi, nizungumzie visiwa vya kwetu. Wilaya yangu ya Muleba inazo kilometa za mraba 7,000 ambazo ni maji na ndani yake ziko kata tano ambazo zina watu wanaishi na visiwa karibu 39.

Mheshimiwa Naibu Spika, wazo na pendekezo langu kwa Serikali, Kata za Ikuza na Mazinga wananchi wenyewe wanahangaika kujenga sekondari. Naiomba Serikali kupitia TAMISEMI, Mheshimiwa Ummy na Mheshimiwa Prof. Ndalichako, hawa wananchi wa Ikuza na Mazinga uwasaidie kwa jitihada zao wamalizie sekondari zao. Itatusaidia sisi kuona vifo vya watoto wanaoanguka na mitumbwi wakati wa hali mbaya ya ziwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, unapoondoa Ikuza na Mazinga unabaki na Goziba, Kerebe na Bumbile. Ninalo ombi, na niliwahi kulipeleka kwa Mheshimiwa Rais, Mungu amlazi mahali pema Peponi, najua Mheshimiwa mama Samia atachukua wazo hili alifanyie kazi. Wananchi wa Kerebe, Goziba na Bumbile wana sekondari yao moja iko Bumbile. Tunachoomba, pesa za sekondari ya Kata, mnazotaka kupeleka kwenye kila Kata msizipeleke Goziba, wala Kerebe, zote mzipeleke Bumbile. Mwende Bumbile mtujengee mabweni na madarasa ya ku-accommodate watoto karibu 1,000 ili watoto wa visiwa vyetu 39 wawe wanakaa bwenini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ni mhamasishaji mkubwa wa elimu, lakini huwa nashindwa kuhudhuria misiba watoto wanapozama kwenye mitumbwi. Ukienda pale, watu wanakuangalia wewe, wanakuona ndio mchawi, kwa sababu ndio ulishawishi mtoto aende shule. Sasa mimi siyo mchawi, mnisaidie kwa kujenga mabweni Bumbile na kujenga madarasa watoto wakae shuleni wasome. Watoto wanataka kwenda kusoma, lakini wanatoka kwenye visiwa vidogo vidogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikwambie, Ziwa Victoria kitaalam hubadili hali ya hewa baada ya dakika 25. Unaingia kwenye ziwa liko vizuri, baada ya dakika 25 limebadilika. Mwezi Februari, mimi mwenyewe na wataalam tisa wa Halmashauri tulisalimika kufa maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI, umeniskia rafiki yangu, Mheshimiwa Mama Joyce Ndalichako umenisikia. Naomba Bumbile Sekondari sasa iitwe Prof. Joyce uweke shule ya bweni ya Serikali watoto waache kufa, nami nikaonekana mchawi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye uboreshaji wa sekta ya elimu. Naunga mkono Serikali kuboresha suala la sheria za elimu, ule Muswada wa Sheria ya Elimu uletwe na kuboresha sera. Ninachotofautiana na ninyi, mnasema mlenge mahitaji ya sasa, ushauri wangu ni kwamba; na Waziri wa Fedha ananisikia; Dira ya Taifa inakwisha mwaka 2025, Dira ya Taifa inapaswa ihuishwe sasa. Dira ya Taifa ya 2025 ni outdated, tunapaswa kuangalia miaka 50 mbele.

Mheshimiwa Naibu Spika, leteni Dira ya Taifa ya mbele na sheria za elimu, Sera ya Elimu itakayoundwa iwaandae Watanzania kupambana miaka 50 hadi 60 mbele. Mengine yote yako vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie maboresho yanayoweza kufanyika sasa, nakubaliana na Wizara kwamba wataboresha Shule za Ufundi, wakianzia na Ifunda na Iyunga. Wamezitaja shule tisa, hizo shule zilikuwa maarufu miaka ya sabini nikiwa sekondari.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimweleze Mheshimiwa Waziri ajaribu kukumbuka, Ifunda ilipokuwa maarufu tulikuwa na sekondari hazizidi 200 Tanzania. Hizo tisa zilipokuwa maarufu sekondari Tanzania nzima hazikuzidi 200, leo tuna sekondari zaidi ya 4500, kwa hiyo Shule za Ufundi zitengenezwe proportionally kwa uwiano, kuwe na shule za Ufundi proportionally uwiano wa 9:200 sasa 4,500 itakuwa ngapi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimshauri Mheshimiwa Waziri, wamelenga kuleta masomo ya ujuzi, wasiwachanganye watoto, wawafundishe mazingira, kilimo, biashara, ufundi, hapana. Tuige mfano wa zamani, ziwepo shule za mchepuo wa kilimo, mchepuo wa biashara, mchepuo wa ufundi, waliosoma SHYCOM wanajua. Mwanafunzi aliyesoma SHYCOM alikwenda kusoma Chuo Kikuu akirudi CPA anaipiga per seat. Mwanafunzi wa SHYCOM alikuwa na makali yake hata na Waziri wa Ujenzi wa sasa alisoma Chuo cha Ufundi, ndiyo ma-engineer ambao wanatisha sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuige mfano wa zamani, chenga ya zamani si mbaya ilimradi goli linafungwa. Kwa hiyo naishauri Serikali iende kwa mfano huo. Kwa mfano, shule za michezo, wachukue shule ya michezo, mtoto anayejua kucheza mpira na kukimbia wafundishe Hesabu, Kiingereza na Kiswahili basi, kinachobaki asubuhi na jioni anacheza mpira, Kiingereza na Hesabu. Kwa hiyo aende, aende, hiyo ndiyo specialization. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo haisuburi sera, haisubiri sheria ni kunisikiliza na Mheshimiwa Waziri akiniita, anapaswa kuwa na soda, nitamshauri na mambo yanakwenda. Hakuna haja ya kusubiri kubadilisha dira, ndiyo mkakati huo, watoto wanawachosha, wengine wanasema wasome mazingira, wasome na vitu vingi, watasoma mpaka wapi. Mheshimiwa Waziri apunguze ili watu wawe na umahiri (specialization) ili waweze kuelewa zaidi tuweze kwenda. Maisha ya binadamu ni miaka sabini, msiwafundishe kana kwamba wataishi miaka 900. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie VETA, mtaala wa VETA, VETA yetu inapaswa kurekeā€¦

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Kengele imeshalia.

MHE. CHARLES J.P. MWIJAGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie. Tubadilishe mtaala wa VETA ulenge sekta za kiuzalishaji, the productive sectors. VETA si ya kufundisha udereva, udereva wa magari madogo si kazi waende kwenye productive sectors; kutengeneza chakula, watengeneze maziwa, watu wanakula hawawezi kuacha kula, kwa hiyo VETA ibadilike. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha na naunga mkono hoja. (Makofi)