Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Neema Kichiki Lugangira

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Kwanza kabisa, napenda kuipongeza Serikali kwa kuja na Sera ya Elimu bure na uwekezaji mkubwa katika miundombinu. Napenda niseme kwamba, kama tutaendelea kutotilia maanani suala la lishe shuleni, jitihada hizi zote zipo hatarini.

Mheshimiwa Spika, nasema hivi kwa sababu mtoto anapokuwa darasani lazima aweze kufikiri, kuelewa, kuchakata na kukariri kile anachofundishwa na mwalimu; lakini kama ubongo wake haufanyi kazi vizuri, kama ubongo wake haujapata virutubisho sahihi, basi mtoto huyu hawezi kujifunza ipasavyo na hiyo ni sawa sawa na kutegemea gari lisilo na mafuta liweze kutembea.

Mheshimiwa Spika, wanafunzi wanatoka nyumbani alfajiri, wengi wanakuwa hawajala, wanakwenda shule wanashinda njaa, akiwa darasani tumbo linanguruma, tumbo linanguruma kwa sababu linakosa kitu cha kusaga na kupeleka kwenye ubongo. Kwa hiyo mwanafunzi anakosa umakini kiasi kwamba Mwalimu anaweza kutoka kufundisha, ukamuuliza mwanafunzi mwalimu kasema nini akasema sijui. Mtoto yule ukahangaika kumpiga na kusema kwamba ni mtukutu, hana adabu, hasikilizi darasani lakini kumbe ubongo wake uli-cease kufanya kazi kwa sababu ya njaa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ningependa kuikumbusha Serikali kwamba pia hali ya udumavu nchini inachangia kwa kiasi kikubwa kwa watoto kutoweza kufaulu na kufundishika shuleni. Wenzetu wataalam wa lishe TAMISEMI wanatuambia kwamba katika kila darasa la watoto 45, watoto 15 hawafundishiki. Sasa tupate picha tuna jumla ya wanafunzi milioni 11, kama katika kila 45 15 awafundishiki ina maana pamoja na jitihada zote hizi tunaendelea kufifisha hizi jitihada kutokana na uwelewa na ufaulu ndio maana unakuwa huko chini. Kwa hiyo naiomba Serikali iweke mikakati madhubuti ya kuhakikisha kwamba kila shule hususani za kutwa pia wanazalisha mazao yenye lishe kwa mfano viazi lishe, maharage lishe, mahindi lishe na mengineyo ili kuhakikisha kwamba watoto hawa hawashindi shuleni wakiwa na njaa.

Mheshimiwa Spika, napenda pia kusema kwamba pamoja na jitihada zote za elimu bure pamoja na jitihada zote za miundombinu bora, ikiwa bado tutaliweka pembeni suala la lishe shuleni jitihada hizi zote zitafifisha malengo ya Serikali ya kuhakikisha kwamba elimu yetu inanufaisha watoto wa kitanzania. Kwa hiyo naiomba sana Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ije na mkakati madhubuti tunakwenda kufanya nini ili kuhakikisha watoto wanapata lishe shuleni.

Mheshimiwa Spika, eneo langu la pili ni upande wa hedhi salama. Naipongeza sana Serikali kwa mikakati mbalimbali iliyowekwa kuhakikisha mtoto wa kike anabaki shuleni, kuhakikisha kwamba mtoto wa kike analindwa ili apate elimu. Hata hivyo, mtoto huyuhuyu wa kike kila mwezi anapofika umri wa kubalehe anakosa siku tano mpaka siku saba kwa sababu ya kuwa kwenye hedhi. Kwa hiyo suala hili pia naiomba Serikali ilitilie mkazo. Nafahamu kuna bajeti ndogo kwenye elimu bure ya kupata msaada wa taulo za kike kwa dharura lakini Serikali iweke wazi kwa sababu dharura zinakuwa nyingi, lakini pia Serikali ije na mkakati madhubuti katika eneo hili.

Mheshimiwa Spika, nitoe mfano mdogo tu, kwenye shule za msingi kuna wanafunzi wa kike 5,481,982; kwenye shule za sekondari kuna wanafunzi wa kike milioni 1,284,410; kati ya hawa wote tukichukulia tu asilimia 20 wako kwenye umri wa kubalehe ina maana tuna jumla ya watoto milioni 2,380,806 ambao kila mwezi wako hatarini kukosa shule siku tano mpaka siku saba. Hili ni jambo zito sana ambalo Wizara inabidi iliangalie kwa jicho la kipekee. Wale ambao wanakwenda shule, wanatumia vitu ambavyo ni hatari sana kwa afya zao, wanatumia mabanzi, wanatumia magazeti, wanatumia vitu ambavyo vinapelekea na naamini kwamba vinachangia kwa ongezeko kubwa la kansa ya shingo ya kizazi. Kwa hiyo naiomba sana Serikali ione namna gani itaweza kusaidia na kuhakikisha kwamba mtoto wa kike hakosi shule kwa sababu ya kuwa kwenye hedhi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia naamini kwa sababu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia ni mama yetu Profesa Ndalichako na haya masuala yote mawili lazima yanamgusa moja kwa moja kama mama, naamini kabisa atakuja na mpango madhubuti wa kuhakikisha moja watoto wanapata lishe shuleni, lakini pili, mtoto wa kike hakosi shule kwa sababu ya kuwa kwenye hedhi. Nashukuru sana. (Makofi)