Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Grace Victor Tendega

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuchangia katika bajeti hii ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. Nianze kwa msemo usemao; if education is expensive try ignorance.” Kwa tafrisi ya kawaida tu inasema kwamba, kama elimu ni gharama jaribu ujinga. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nazungumza hivi kwa sababu, tunaangalia jinsi ambavyo elimu ya nchi hii inavyokwenda. Nashukuru sana Kamati ilivyotoa maoni yake kwa ajili ya kujenga na kuboresha Wizara hii ya elimu. Naafiki kabisa maoni na mawazo ya kamati ambayo yametolewa, yatasaidia sana kuboresha katika Wizara hii ya Elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, najikita katika sehemu kubwa kuhusu udhibiti ubora, kwa maana ya kwamba, zamani tulikuwa tunasema ni ukaguzi. Tunazungumza, watu wengi wanazungumza kwamba, ooh, tubadilishe mitaala, tufanye hiki, tufanye vile, ili tuendane na hali halisi ya maisha yanavyokwenda. Ni kweli ni vizuri tukafanya hivyo, lakini kitendo cha kubadilisha, yaani total over hauling ya curriculum inachukua miaka mingi sana. Kwa hiyo, huwa tunakwenda tunabadilisha, labda tunaboresha wakati tuna-plan kubadilisha hiyo mitaala kulingana na haja kamili tunayoitaka ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nchi mbalimbali zinakuwa na targets kwamba, sisi tunataka nchi yetu iwe ya namna gani? Tunataka wananchi wa Tanzania wajikite kwenye mambo gani? Kilimo, muziki ama ni watu wa viwanda sana au kitu kama hicho? Kwa hiyo, lazima kuwe na tafiti ya muda mrefu na wananchi wakubaliane na wadau kujua kwamba, tunataka nchi yetu iendeje na uchumi wetu uweje?

Mheshimiwa Spika, sasa kwa sababu bado hatujaanza huo mchakato, nashauri katika usimamizi ubora wa elimu, udhibiti ubora. Sasa nikianza na hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Elimu aliyoitoa hapa, ukurasa wa tisa na ukurasa wa 15 nimeona kuna contradiction kidogo ya taarifa zake katika namba. Waziri amezungumzia kwamba, katika mwaka huu uliopita walikuwa wameweza, plan yao ilikuwa ni kukagua shule 4,700 za msingi, lakini walikagua shule 2,755, kati ya shule 2,726 ambayo ni asilimia 101.

Mheshimiwa Spika, ujue tuna shule 18,152. Sasa tukiwa tunajipima hivyo kwamba, hapa tumekagua asilimia 100, lakini hali halisi tunaiona, shule zetu hazikaguliwi na usipokagua watu hawafanyi kazi kwa ufanisi, walio wengi. Sasa kwa sababu, hawafanyi kazi kwa ufanisi mtaona kama ile mitaala haifanikiwi, lakini kumbe ufanisi, ukimkagua mtu anaongeza juhudi, anaongeza speed ya kufanya kazi. Sasa kutokuweka idadi kubwa na targets zao za kukagua sana shule zetu wataona changamoto zilizopo kati ya shule za Serikali na shule za private. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, shule za private zinakaguliwa na zinakaguliwa kwa sababu shule zile zinatoa pesa wakaguzi wanakwenda kukagua zile shule. Kwa hiyo, utakuta kwamba, mara nyingi wale wanafanya kazi kwa juhudi kwa sababu, kuna ukaguzi uko pale, lakini shule zetu zinakwenda tofauti na hivyo.

Mheshimiwa Spika, sasa nitajikita katika udhibiti ubora katika shule zenye mahitaji maalum. Katika Ripoti ya CAG amezungumza kwamba, kuna changamoto ya usimamizi wa ubora wa elimu katika hizi shule, unakuta kuna miaka inapita hazikaguliwi kabisa. Na kama hazikaguliwi, lakini tuna uhaba wa Walimu wa kwenda kukagua hizo shule, ni wachache. Katika, anasema ni asilimia nane tu ndio waliopo ambapo tuna mahitaji ya Walimu 1,306, sisi tuna asilimia nane tu.

Mheshimiwa Spika, hawa ni wenzetu, watu wenye ulemavu ni wenzetu. Shule zipo, lakini tuna chuo kimoja tu kinachotoa Walimu wa watu wenye ulemavu ambacho kiko Patandi. Walimu wakisomea pale wanapelekwa katika shule ambazo hazina watu wenye mahitaji maalum. Kwa hiyo, unakuta kwamba, Wizara inaweza ikawa inapeleka watu kusomea hicho kitu, lakini hawapangiwi kule, matokeo yake inakuwa ni changamoto ileile inaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama hiyo haitoshi, imeonesha kwamba, hakuna vifaa vya kufundishia asilimia 68 katika shule 17 kati ya 18 walizotembelea, lakini hakuna utaratibu endelevu wa kugharamia ukaguzi katika hizo shule. Mwaka jana walitenga shilingi milioni 272 katika Wizara ya Elimu kwenda kukagua hizo shule.

Mheshimiwa Spika, kwa kitendo ambacho kinaumiza kabisa badala ya kwenda kukagua, Wizara ilipeleka hizo fedha kwa ajili ya mitihani ya darasa la nne na pia ilipeleka kwenye mashindano ya lugha ya Kiingereza Afrika Mashariki. Sasa utaona jinsi ambavyo zile pesa zilitengwa, lakini hazikwenda kwenye ukaguzi wa hizo shule. Matokeo yake ni nini? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, utaona kwamba, tunapata changamoto kubwa ya kuziendesha hizi shule kwa sababu, hakuna wakaguzi, hatuna Walimu, hakuna uendelevu wowote wa utengaji wa fedha katika hili. Nimwombe Mheshimiwa Waziri aweze ku-consider na hii sekta kwa watu wenye ulemavu.

Mheshimiwa Spika, niende sasa katika mafunzo kwa Walimu kazini. Tulikuwa na kawaida miaka iliyopita Walimu kazini walikuwa wanapata mafunzo wanapelekwa kwenye vyuo; Chuo cha Songea, Butimba, Morogoro na vyuo vingine kwa miezi mitatu, mitatu angalau kunolewa kuona ni nini ambacho watakwenda kufundisha. Mkiboresha mitaala kuwa ya competence-based curriculum hiyo, unachukua Walimu wale wakapate ile knowledge ya kufundisha hivyo, kwa sababu, kila mara kuna mabadiliko yanatokea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hiki kitendo kimekuwa ni cha, kama wanatoa ni kidogo sana, lakini Walimu wanahitaji kupata haya mafunzo ili waweze kunolewa kwenda na wakati. Kama tunavyosema kwamba, tunataka mitaala iende na wakati, lakini tunataka na Walimu waende na wakati, ili waweze kufundisha vizuri wanafunzi wetu tusilalamike kwenye matokeo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia Taarifa ya CAG inaonesha kwamba, hakukuwa na mpango wowote wa kutoa mafunzo kwa Walimu wa sekondari. Walimu wa sekondari hawakupata kabisa mafunzo hayo kazini ambapo ndipo wanaponoa wanafunzi wetu waweze kufanya vizuri katika masomo yao.

Mheshimiwa Spika, pia nakubaliana na Kamati wanavyosema kwamba, tuweze kuwawezesha kutoa mikopo kwa wanafunzi wanaochaguliwa kwenda kwenye vyuo ambavyo vinasimamiwa na NACTE kwa sababu pale ndio tutapata wanafunzi ambao wakitoka ndio watakuja kuwa watenda kazi katika viwanda ambavyo tunavitarajia kuvijenga. Kwamba, tutakuwa na viwanda, watenda kazi watakuwa ni wale wanafunzi watakaokuwa kule, lakini kama hawatakuwa wanapewa mikopo ni changamoto bado inabaki kuwa kubwa kupata hii kada ya chini ambayo ndio ya watenda kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kweli, kwa kutoa ile asilimia ambayo ilikuwa kwenye Bodi ya Mikopo, asilimia sita na pia Mheshimiwa Waziri amezungumza hapa pia, wametoa hata ile asilimia nyingine 10. Nipongeze kwa hilo kwa sababu, hiki kilikuwa ni kitu ambacho kinawaumiza sana vijana wengi na wengi ambao wanasoma elimu ya juu kuona kwamba, wanaweza kulipa namna gani, mishahara ilikuwa inakatwa, walikuwa wanashindwa kufikia malengo. Napongeza kitendo hicho kinasaidia sana, kitasaidia watu kufanya kazi kwa juhudi na kujua kwamba, Serikali yao inawajali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niende sasa kwenye jambo ambalo sio la mwisho kwa umuhimu, tuna wanafunzi wa kike wanaopata ujauzito kwa bahati mbaya. Sihalalishi kwamba, wale wanaofanya hivyo kwamba, ni halali, hapana, lakini kuna wanafunzi kwa mazingira yaliyopo kule vijijini na maeneo mengine wana mazingira magumu ambayo inafikia wanakutwa na hali hiyo. Nakumbuka mwaka 2015 kulikuwa na swali lilitolewa hapa na Mheshimiwa Magreth Sita na Naibu Waziri akaahidi kwamba watatengeneza mwongozo wa namna ya kuwahakikisha hawa vijana wanarudi shule. Kwa hiyo naomba mheshimiwa Waziri anapohitimisha basi tujue wanafunzi wetu watafikia wapi.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa.

MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakumbuka mwaka 2015 kulikuwa na swali lilitolewa hapa na Mheshimiwa Margaret Sitta na Naibu Waziri akaahidi kwamba watatengeneza mwongozo wa namna ya kuwahakikisha hawa vijana wanapata kitu.

SPIKA: Ahsante.

MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba mheshimiwa Waziri unapohitimisha basi tujue wanafunzi wetu watafikia wapi ahsante sana. (Makofi)